VIONGOZI wa dini ya Kikristo katika Ibada ya Ijumaa Kuu wamewataka waumini kutafakari maisha yao kwa kina, kusimama katika ukweli, haki na kutubu dhambi kwa moyo wa toba ya kweli.

Viongozi hao waliyasema hayo katika Ibada za Ijumaa Kuu zilizofanyika katika makanisa na mikoa tofauti nchini jana.

Katika Parokia ya Changanyikeni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Askofu Mkuu Yuda-Thaddaeus Ruwa’ichi aliwataka viongozi wa dini, serikali na waumini kwa ujumla kujiuliza kama kweli wanatetea haki na ukweli, au ni sehemu ya mfumo wa dhuluma, unyanyasaji na upotoshaji.

Akihubiri katika Ibada ya Ijumaa Kuu, Askofu Ruwa’ichi alisema simulizi ya mateso ya Yesu Kristo ni funzo kwa kila mtu, ikionesha namna hata baadhi ya wafuasi wake walitetereka kwa udhaifu wa kibinadamu, lakini walijirekebisha na kuonesha ujasiri na imani mwishoni.

“Pilato, aliyekuwa mwakilishi wa Kaisari na msimamizi wa sheria, alitambua kuwa Yesu hana kosa, lakini kwa kukosa uthubutu, alimtoa auawe, jambo linalotufundisha kuhusu aina ya uongozi tunaopaswa kuwa nao usioyumbishwa na hofu wala shinikizo,” alisema Askofu Ruwa’ichi.

Aliwataka waumini kujihoji nafasi yao katika kutetea haki na wanyonge, badala ya kuwa wepesi kuwanyooshea vidole viongozi pekee. “Kila mmoja ajitazame mwenyewe na ajiulize: Je, ninasimama upande wa haki, ukweli na huruma?” aliongeza.

Katika Parokia ya Isidori Mkulima, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padri Emmanuel Shija alihubiri kuwa mateso na kifo cha Yesu Kristo msalabani ni mpango wa Mungu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi.

Padri Shija aliwataka waumini waache tabia ya usaliti kama wa Petro na Yuda Iskarioti, waepuke wivu na chuki, na wajifunze kutoka kwa Yesu aliyestahimili dharau, mateso na hatimaye kufa msalabani kwa ajili ya wokovu wa wanadamu.

“Wayahudi walimwonea Yesu wivu kwa sababu ya matendo yake ya huruma na uponyaji. Lakini pamoja na yote hayo, Yesu alikubali kifo kama njia ya kutimiza mapenzi ya Mungu,” alisema Padri Shija.

Katika Jimbo Katoliki la Musoma, Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Padre Chukwuemeka Anyanwu alisema Ijumaa Kuu ni siku ya kutafakari kwa kina uzito wa dhambi za mwanadamu na jinsi Yesu alivyokuwa sadaka ya upendo wa Mungu. Ibada hiyo ilihusisha sehemu tatu kuu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba, na Ekaristi Takatifu.

Waumini walivaa mavazi mekundu kama ishara ya damu ya Kristo na mateso aliyoyapitia.

“Somo la Isaya linatufundisha juu ya Mtumishi wa Bwana aliyedhulumiwa lakini hakulipiza. Somo la Waebrania linatukumbusha kuwa Yesu ni Kuhani Mkuu aliyepitia mateso kama sisi lakini hakutenda dhambi. Yote haya yanatufundisha utii na imani,” alisema Padre Anyanwu.

Aliwataka waumini kutumia siku hiyo kama fursa ya kusameheana, kuondoa chuki na kutafakari maisha yao upya katika mwanga wa mateso ya Kristo.

Naye Askofu Anthony Lagwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu, alisema Ijumaa Kuu ni siku ya kujitafakari na kuacha usaliti, dhambi na uzembe wa kiroho. Aliwataka waumini kuiga mfano wa Yesu aliyebeba msalaba mzito na kuupokea kwa upendo kwa ajili ya wanadamu.

“Tufikirie ni upendo wa aina gani huu mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya wengine. Hili ni agizo kwetu sisi pia kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya wengine, kuachana na hali zetu zinazotutenga na upendo wa Mungu,” alisema Askofu Lagwen.

Msaidizi wa Askofu wa Kanisa Kuu la KKKT Azania Front Dar es Salaam, Mchungaji Chediel Lwiza aliwataka waumini wa dini ya kikrisro kutafakari juu ya kumbukumbu ya Ijumaa Kuu inawasaidia katika maisha yao.

Alieleza kuwa waumini wote wanapaswa kujua kifo cha Yesu Kristo na kumbukumbu ya Ijumaa Kuu inamchango gani katika kuwafundisha kuwakumbusha na kuwajenga katika maisha yao ya kiimani.

“Umekuja kanisani alasiri ya leo (jana) kukumbuka kifo cha Yesu Kristo umeondoka nyumbani umekuja kanisani kukumbuka kifo cha Yesu imekusaidia nini, ni jambo gani leo ukiona kifo cha Yesu tunachokizungumza limekujenga, limekufundisha, Mungu atusaidie tunapokiona kifo chake na kufa kwake anamadai na sisi, hawezi kufa msabani hivi hivi anamadai na wewe.”

Ibada ya Ijumaa Kuu katika makanisa yote pia ilihusisha utoaji wa sakramenti ya kitubio na mpako wa wagonjwa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kiroho kuelekea sikukuu ya Pasaka siku ya ufufuko wa Yesu Kristo.