Na Thompson Mpanji, Mbeya
 
KUIBUKA kwa kundi kubwa la vijana wanaofanya uhalifu bila woga huku wakijiamini kutenda makosa ya jinai hata kutishia maisha na mali za wakazi wa Jiji la Mbeya wanaojiita “Wakorea Weusi”, limezidi kutia hofu na kuwalazimisha wananchi walio wengi kujiuliza maswali yasiyo na majibu kuwa ni akina nani hao? Wametumwa au ni wao wenyewe waliojiunga kwa kutumia zana ya hali ngumu ya maisha?
Wapo wanaojiuliza kuwa, je, inawezekana vijana hawa ambao kwa historia ya Jiji na Mkoa wa Mbeya  hawajawahi kusikika uwepo wao zaidi ya kuyasikia Dar es salaam na kwingineko yakiwamo Makomando Yoso, Panya Road na mengineyo sasa ndiyo wameibukia mkoani Mbeya?
Lakini bado kumeendelea kuwepo maswali mengi ya kujiuliza yanayojaribu kuunganishwa na matukio mbalimbali ya kisiasa huku wengine wakihusianisha kushikiliwa kwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, almaarufu Sugu, na hatimaye kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela kwamba labda wafuasi na wapenzi wake waliokuwa wakimuunga mkono na hata kumbandika jina la ‘Rais wa Mbeya’ ndiyo wanaotekeleza hayo?
“Kwakweli hali ya amani imetoweka kabisa jijini Mbeya baada ya kuibuka hili kundi la watu wasiojulikana na tunaomba vyombo vya ulinzi na usalama viendele na majukumu yao ya kawaida badala ya kupangiwa majukumu mengine,” amesema mmoja wa wananchi.
Wakati hayo yakiendelea kuumiza vichwani vya wananchi wakiwemo na viongozi, hali imebadilika na JAMHURI limebaini kuwa wananchi sasa wanawahi kurejea nyumbani mapema kuliko kawaida.
JAMHURI limepita mitaa ya Uyole, Nsalaga, Isyesye, Igawilo na Itezi na kukuta ukimya wa kutisha nyakati za usiku kutokana na maeneo ya starehe kufungwa mapema katika wiki yote iliyoisha. Mahitaji muhimu kama maduka, magenge, vilabu vya pombe za asili na maeneo ya viwanyaji baridi na moto yanafungwa mapema kwa madai ya kuhofia maisha yao endapo watakutana na kundi hilo.
“Umeona hata usafiri umekuwa wa shida muda huu wa saa 3 usiku kinyume na ilivyo kawaida kutokana na kila mtu kuhofia maisha yake kuogopa ‘Wakolea Weusi’, maana siyo vijana wa kawaida kutokana na kuingia hadi katika baa na kufanya unyang’anyi bila woga,” kimesema chanzo chetu.
Mmoja wa waendesha Bodaboda katika maeneo ya Stendi ya Mabasi ya Uyole, ameliambia JAMHURI kuwa kumekuwepo na taarifa  baadhi ya vijana hao kutoka nje ya Mkoa wa Mbeya na kuungana na vijana wengine wa jijini Mbeya.
Katika mitandao ya kijamii mtu aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Mwaipasi, ameweka picha inayoonyesha akiwa ameumizwa kwa kiasi kikubwa, huku yeye akisema: “Duuuuuuu namshukuru Mungu japo ninamaumivu makali lakini uhai upo. Asanteni kwa maombi yenu. Hawa wanaojiiita Wakorea Weusi ndo kazi wanayoifanya Mbeya.”
JAMHURI limewasiliana na Mwaipasi ambaye amethibitisha kuvamiwa na kujeruhiwa na mtu hasiyejulikana kwa kupigwa na kitu kizito kichwani mita chache na nyumbani kwake katika Pipeline, maeneo ya Mwangonela, Kata ya Iyela.
“Ilikuwa ni Januari, 24 nikitokea kazini majira ya saa 3 usiku na nilikutana na bwana mdogo mmoja ninamfahamu ni mwendesha Bodaboda nikamuuliza mbona leo umewahi kupaki pikipiki? Akasema ‘ninawaogopa Wakorea Weusi’, lakini nyuma yetu kulikuwa na mtu ambaye akajibu ‘Mbona Wakorea weusi wameshakamatwa?’ Kwa kweli alikuwa mbishi sana na tuliendelea na safari huku wale wenzangu wakijua labda nipo naye na huku mimi nikijua labda wapo naye,” amesema Mwaipasi na kuongeza:
”Baada ya kuagana na wale akina dogo na ilibakia kama mita chache sana kufika nyumbani nikashtukia nimepigwa na kitu kizito kichwani na nikapoteza fahamu na baadaye nikajikuta nipo Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, lakini majirani waliniambia nilipiga yowe kama mara mbili ndipo wakaja kunibeba na nilichukuliwa simu na waleti iliyokuwa na Sh 62,000, lakini waleti ilikutwa kwenye pagale imetupwa ikiwa na vitambulisho vyote. Kwa kweli hawa watu tutakuwa tunaishi nao kikubwa ni kuimarisha ulinzi na maeneo ya Airport, Mwakibete na Ivumwe imekuwa ni hatari sana.”
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya wakizungumza kwa nyakati tofauti na JAMHURI wameliomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama  kulishughulikia kwa kina suala hili kulikomesha wanannchi na mali zao waendelee kubaki salama kama ilivyokuwa awali.
Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishna Mohamed Mpinga amesema hadi Jumamosi jioni walikuwa wamekamata vijana 48 wanaotuhumiwa kuhusika na matukio haya ya wizi. Amemtaja kiongozi wa watuhumiwa hao kuwa Kelvin Raphael (22), mkazi wa Mwakibete, Bombambili aliyedai kuwa asili ya jina hili ni upinzani wa timu mbili za soka za Korea na Marekani. Vijana hao wamekutwa na bisibisi, nyundo, mkasi na vifaa vya muziki.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Gabriel Makalla ameliambia JAMHURI kuwa Mbeya zamani ilikuwa na wapiga nondo, lakini walitafutwa mpaka shina lake likang’olewa. “Kumeanza kuonekana dalili, wameanzaanza tena. Diwani wa Mbalizi ameniambia. Nimetangaza rasmi kufanyika kwa operation, ambayo imeanza kuzaa matunda. Nalipongeza jeshi la polisi na nawapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano kwa polisi. Vijana hao wamekutwa na vifaa kama mikasi na nondo,” amesema Makalla.
Alipoulizwa kwa nini Mbeya inakuwa na matukio mengi ya kutisha ikiwamo wachuna ngozi, akasema: “Nilipokuja [baada ya kuteuliwa] nilizungumza na viongozi wa dini na viongozi wa mila, maana kuchuna ngozi kulikuwa kunafanyika kwa sababu ya mambo ya kishirikina, lakini pia kulikuwa na imani zilizopitiliza kwamba mtu akifa asizikwe watamwombea atafufuke. Hizo nimezipiga marufuku na hazipo tena. Sasa hata hili nalimaliza la ‘Wakorea Weusi’. Watafute kazi nyingine uhalifu haulipi,” amesema Makalla.
JAMHURI limeelezwa kuwa watu hao wangefikishwa mahakamani muda wowote kuanzia jana na msako mkali unaendelea ambapo polisi wamepanga kupita nyumba kwa nyumba kufahamu nani anafanya nini na anashughulika na kazi ipi.