Wakimbizi 21 kutoka kambi hiyo jana wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kuunda kundi la uhalifu na kufanya maandamano kinyume cha sheria.
Wakati mvutano ukiendelea baina ya polisi wa Rwanda na wakimbizi kutoka Congo katika kambi ya Kiziba magharibi mwa Rwanda, mwendesha mashtaka anataka wapewe kifungo zaidi cha siku 30 ili kumpa muda wa kukusanya ushahidi zaidi.
Wao wanasema wanazuiliwa kinyume cha sheria na kutaka waachiliwe mara moja.
Ni kesi iliyodumu kwa muda mchache katika mahakama ya Muhanga kusini mwa nchi, ikihusisha wakimbizi 21 kati ya 22 waliokamatwa miezi 2 iliyopita kutoka kambi ya Kiziba.
Wakimbizi hawa wanashitakiwa kuunda kundi la kighaidi na kukaidi sheria za Rwanda.
Kesi yao inahusu wao kupewa kizuizi cha muda kama ilivyoombwa na mwendeshamashitaka huku upande wao wakitaka kuachiwa kwa dhamana.
Hoja ya mwendesha mashtaka imekuwa kwamba anataka waendelee kuzuiliwa kwa siku 30 zaidi ili kumpa muda wa kukamilisha upelelezi dhidi yao.
Watuhumiwa na mawakili wao wameiambia mahakama kuwa hawana hatia na kwamba kuzuiliwa kwao hakujafwata sheria na kutaka waachiliwe mara moja,hoja yao ya msingi ikiwa ni kwamba wao ni wakimbizi wanaoishi katika kambi na ambao hawawezi kutoroka na kurudi nchini mwao Congo.Mwendeshamashtaka yeye anasema ana wasi wasi wa wao kutoroka ikiwa watapewa dhamana.
Tuhuma dhidi ya wakimbizi hao zimetokana na maandamano yaliyofanywa na wakimbizi kutoka kambi ya Kiziba magharibi mwa Rwanda nje ya ofisi za shirika la wakimbizi duniani huku wakipinga kupungua kwa msaada wao wa chakula na kutishia kurejea nyumbani.katika purukushani na polisi wakati polisi ikivunja maandamano hayo wakimbizi 11 walifariki.
Kesi dhidi yao itaendelea mwishoni mwa mwezi huu.