Siku chache baada ya maofisa wanaoendesha Operesheni Okoa Mazingira iliyofanyika katika Kijiji cha Usinge wilayani Kaliua, kutuhumiwa kumuua, Kipara Issa (39), kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume na sheria, baadhi ya wanaume katika kijiji hicho wamelazimika kuzikimbia familia zao kwa hofu ya kukamatwa na maofisa hao.
Hatua iliyochukuliwa na wakazi hao wa Kijiji cha Usinge inatokana kuwapo kwa taarifa ya kuwa kuna orodha ya majina imepelekwa katika kikosi kazi kinachofanya operesheni hiyo na wanatafutwa na kikosi hicho.
Kikosi kazi hicho kinachoundwa na maofisa kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na Maofisa Maliasili na kuanza operesheni hizo Oktoba mwaka huu, kinawasaka watu wanaojihusisha na uwindaji haramu.
Kikosi hicho kinatuhumiwa kufanya ukatili kwa watu wanaotajwa kuhusika na ujangili. Imebainika kuwa wapo baadhi yao wamepata mateso hayo na kuathiri afya zao.
Mzee maarufu katika Kijiji cha Usinge, John Kijiko (65), naye anadaiwa kupigwa na kujeruhiwa vibaya na maofisa hao, jambo lililofanya alazwe katika Zahanati ya Usinge kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Mwingine aliyekutwa na kadhia hiyo ni Ishize Kimbunga (39), ayejeruhiwa vibaya kutokana na mateso makali aliyoyapata na hata kusababisha maumivu katika sehemu ya haja ndogo na kubwa.
Wanaume wakimbia makazi yao
Kutokana na hali hiyo, wakazi wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini kwa sababu ya usalama wao, kwa nyakato tofauti waliiambia JAMHURI kuwa sasa wanaishi kwa hofu.
Hatua hiyo imewafanya wayakimbie makazi yao na kutelekeza familia zao kwa hofu ya kukamatwa na kuteswa.
Lusoleka Daudi ni mmoja wa watu wanaotajwa katika orodha ya watuhumiwa wanaotafutwa na kikosi kazi hicho, ametoweka nyumbani kwake. Familia yake imeingia hofu ya kuwa huenda naye ameuawa.
Katika orodha hiyo yumo Ndiku Yaleli ambaye kwa muda mrefu yupo Jiji Dar es Salaam akimuuguza dada yake aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Wanakijiji cha Kijiji cha Usinge wanaituhumu orodha hiyo kuwa si sahihi kwani majina mengine yameingizwa kutokana na watu kuwa chuki na majungu.
Hata hivyo, baadhi ya watu wakiwamo wanawake ambao waume zao wamelazimika kukimbia kijijini hapo wameyaomba mashirika yanayotetea haki za binadamu kuingilia kati.
Wamesema wanashindwa kuishi kwa amani kutokana na operesheni hiyo ambayo wamedai kuwa kwa sasa inaendeshwa kwa maslahi ya watu binafsi kinyume na malengo yaliyopangwa.
“Yaani huwezi kuamini mimi mume wangu alikamatwa na kupigwa sana, tumefuatilia kumtoa mikononi kwa hao watu maliasili walitaka tuwape shilingi milioni mbili lakini tukawalilia hali kwa muda mrefu tukawapatia laki tano, wenzetu nao wamemtoa ndugu yao kwa shilingi laki nne na elfu sitini,” amesema mmoja wa wanawake walihojiwa na gazeti hili.
Hata hivyo, mwanamke huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amelalamikia hatua hiyo ya kutoa rushwa, kwani imesababisha familia yake ishindwe kupata mlo kutokana na kukosa fedha.
Amesema walipata fedha hiyo baada ya kuuza mahindi waliyokuwa wamehifadhi.
“Sisi ndugu yetu tumemtoa kwa shilingi milioni tatu na hivi sasa bado hali yake si ya kuridhisha, analalamikia zaidi maumivu ya kifua, mgongo, kiuno na miguu lakini baya zaidi alikuwa akijisaidia haja ndogo iliyochanganyikana na damu kidogo,” amesema mmoja wa wanafamilia ya kati ya watu waliojeruhiwa katika operesheni hiyo.
Mkazi mwingine aliyekumbwa na operesheni hiyo ni Mzee Lameck Mbonye (62) aliyekamatwa baada ya kusalimisha bunduki aina ya gbore. Hata hivyo hadi sasa familia yake hajui Mzee Mbonye alipohifadhiwa.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliokamatwa na kupigwa katika operesheni hiyo na baadaye kutozwa fedha ili waachiwe huru kutokana na mazingira ya woga wamekuwa wakiridhika kutoa kiasi cha fedha wanazoombwa huku wakiona kuwa ni haki yao kutoa fedha na pengine kuona kana kwamba kufanya hivyo ni kama kusaidiwa na maafisa wa operesheni hiyo ili waachiwe huru.
Familia ya marehemu Kipara Issa yaingiwa na hofu
Kutokana na mauaji Kipara Issa (39) mkazi wa Usinge familia iliyoachwa na marehemu huyo imeingiwa na sintofahamu na kukumbwa na hofu kubwa dhidi ya wanajeshi wanaoendelea kupitapita katika Kijiji hicho cha Usinge.
Akizungumza na gazeti hili, mama wa marehemu Kipara Issa, Magreth Kajoro amesema licha ya kutopatikana kwa taarifa yoyote kutoka Jeshi la Polisi inayohusu uchunguzi na ufuatiliaji wa kifo cha mwanaye, kinachowatia hofu zaidi ni kuwapo kwa taarifa kuwa maofisa hao wanataka kupoteza ushahidi katika kesi hiyo.
“Kwa kweli Serikali ingejaribu kufuatilia jambo hili maana bado hali inatisha sana, hapa kwetu, mbali na mauaji waliyoyafanya na sisi wengine kupigwa, lakini bado wanahitaji kuwakamata wengine wawili sijui na wao wanataka wakawaue vilevile kama walivyofanya kwa Kipara?” amesema Magreth.
Amesema wanaofuatiliwa kwa ajili ya kukamatwa na maofisa hao ni wanafamilia wawili — Magwese Yusuph (32) na Gayi Said (41) — wote wafanyabiashara wa duka la vifaa vya baiskeli na wakulima wa tumbaku katika hicho.
RPC Tabora
Alipoulizwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi (ACP), Peter Ouma, hatua zilizochukuliwa kuhusu mauaji ya Kipara Issa, pamoja na kujeruhiwa kwa mke wake, Tabu, alisema kwa sasa hana uwezo wa kulisemea hilo.
Amesema operesheni hiyo ina wasemaji wake wakuu licha ya kuwa wapo watu wanaendelea kufanyiwa yale ambayo wanalalamikia yanatendeka kinyume na haki za binaadamu.
“Nimekwambia mimi kwa sasa siwezi kuongelea hilo naomba kama una jambo jingine niulize nitakujibu lakini kwa hilo siwezi,” amesema Kamanda Ouma.
Hata hivyo, aliiambia JAMHURI kuwa atatoa maelezo ya kina na msimamo wa Jeshi la Polisi, baada ya timu ya uchunguzi aliyoiagiza kukamilisha upelelezi wa tukio hilo.
Kauli hiyo ya Kamanda Ouma imechukua sura mpya na kuacha maswali mengi yasiyo na majibu kwa wakazi wa Usinge.
Malalamiko ya wananchi
Siku chache baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tabora kufika Kijiji cha Usinge kufuatilia tukio la mauaji ya Kipara Issa na kudhalilishwa kwa familia yake, Kamati hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, ilipata fursa ya kusikiliza malalamiko ya wananchi dhidi ya maofisa wa operesheni hiyo.
Mambo yaliyobainika katika operesheni hiyo ni kuwa nguvu nyingi ilitumika visivyo halali, hivyo kamati iliahidi kuifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwakamata maofisa waliotenda ukatili huo uliosababisha mauaji.
Ahadi hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa iliwajengea matumaini wananchi wa Usinge. Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa kamati hiyo wananchi hao walishangaa kusikia kwenye kituo kimoja cha televisheni hapa nchini kikitangaza kuwa robo tatu ya wakazi wa Usinge ni wahamiaji haramu.
“Ndugu mwandishi badala ya sisi kuoneshwa jambo kubwa kama hili la mauaji ya wenzetu hapa kijijini na kero tulizomwambia mkuu wa mkoa, leo hii tunashangaa kuziona picha zetu halafu wanasema eti sisi ni wahamiaji haramu, kama ni hivyo basi waje watuue tu ijulikane moja maana hatua sehemu ya kupeleka malalamiko yetu,” amesema mkazi wa kijiji hicho, Samson Michael, na kuongeza:
“Mimi nahisi hata wewe mwandishi ni yale yale si ajabu hata haya tuliyokwambia yataishia hapo hapo kwenye kalamu na hiki kinasa sauti chako, jamani hivi ninyi mkikaa kimya mnatufikiria nini sisi walalahoi, au na wewe utaendea chako halafu ukae kimya?” Samson alisisitiza.
Hata hivyo baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Usinge wamepoteza matumaini ya kurejea kwa hali ya utulivu na amani licha ya kuwa Serikali ya Mkoa wa Tabora kuwaahidi kuwa hakuna tukio jingine litakalojitokeza.
Hata hivyo, kamata kamata bado inaendelea kutokea kwa baadhi ya watu wa kijiji hicho na maeneo jirani, na hata wengine kufanya wakimbie familia zao.