Katika kile kinachoonekana kama hatua kubwa ya kidiplomasia na kisheria, wakili maarufu wa kimataifa, Robert Amsterdam, ametangaza kuingilia kati na kutetea haki za Tundu Lissu, mwanasiasa mashuhuri na mpambanaji wa demokrasia nchini Tanzania.

Hii inafuatia kukamatwa kwa Lissu na viongozi wengine wa CHADEMA katika mkutano wa amani uliofanyika Mbinga hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kampuni ya sheria ya Amsterdam & Partners LLP yenye makao yake Washington, DC na London, Robert Amsterdam amelaani vikali kitendo cha kukamatwa kwa Tundu Lissu, akikitaja kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uhuru wa kisiasa.

Ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Tanzania kwa kile alichokiita mateso ya kisiasa dhidi ya upinzani.

“Kukamatwa kwa Lissu ni kinyume na Katiba ya Tanzania na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za kisiasa. Tunataka serikali kumuachia mara moja bila masharti yoyote,” alisema Amsterdam kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Mbali na wakili huyo, mashirika ya haki za binadamu kama Amnesty International yameiomba serikali ya Tanzania kuacha ukandamizaji wa haki za upinzani na kuhakikisha uhuru wa kujieleza na kushiriki siasa unaheshimiwa.

Hatua hii imewapa matumaini wafuasi wa CHADEMA na Watanzania wengi wanaotaka mageuzi ya kisiasa nchini, huku wengi wakiamini kuwa msaada wa kimataifa unaweza kusaidia kuokoa jahazi la demokrasia lililokuwa linaelekea kuzama.

“Kwa mara nyingine tena dunia imesimama pamoja na Watanzania wanaotafuta haki na uhuru wa kweli. Lissu siyo peke yake,” ameongeza Amsterdam.

Je, hatua hii itazaa matunda? Watanzania wanabaki na matumaini huku wakifuatilia kwa karibu kinachoendelea katika uwanja wa kisiasa na kisheria.