Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Iringa
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepata msaada wa vifaa vya michezo kutoka kwa Wakili wa kujitegemea na mdau wa maendeleo, Jimbo la Kalenga, Sosten Mbedule ambaye ametoa seti sita za vifaa vya michezo na mipira minne.
Wakili Mbedule ametoa msaada huo baada ya ombi lililowasilishwa na Halmashauri hiyo kwa wadau mbalimbali ili kuwezesha timu yao kushiriki mashindano ya watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), yanayofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini kilipokea barua ya ombi hilo na kufanikiwa kupata msaada kutoka kwa Wakili Mbedule, ambaye alijitolea kutoa vifaa vyote vilivyohitajika.
Mashindano ya SHIMISEMITA yanajumuisha Halmashauri za Wilaya, Manispaa, na Majiji kote nchini, yakiwa na lengo la kukuza afya na kubadilishana uzoefu miongoni mwa watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa.
Akizungumzia msaada huo, Afisa Utamaduni na Michezo wa Halmashauri hiyo ya Iringa, Sakina Mgaya, ameshukuru juhudi za Wakili Mbedule, akisisitiza kuwa msaada huo utawawezesha kushiriki kikamilifu katika mashindano hayo muhimu.
Kwa upande wake, Mdau wa Maendeleo Jimbo la Kalenga Wakili Mbedule amesema ni jukumu la jamii kushiriki katika shughuli za kimaendeleo pale inapowezekana.
Amesema, mchango wake utasaidia kuimarisha ushiriki wa Halmashauri katika mashindano hayo ambayo yanakutanisha watu wengi na ni rahisi kuhimarisha undungu na ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta ya michezo nchini.
“Tunaona Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyokuwa pamoja katika masuala ya michezo, hivyo ni bahati sana kuona kiongozi wa juu kushiriki michezo kwa kiwango hicho,nikiwa kama mdau wa maendeleo wa Jimbo la Kalenga, nimeona ni muhimu kuunga mkono juhudi hizi za Mheshimiwa Rais, michezo ichezwe kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka taifa,”amesema Mbedule.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Iringa, Robert Masunya, ametoa shukrani kwa msaada huo, akisema kuwa vifaa hivyo vitawapa motisha watumishi kushiriki vizuri katika mashindano hayo.
Tayari watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini wameanza mazoezi kwa ajili ya mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kuanza Agosti 24 na kumalizika Septemba 5, 2024, jijini Mwanza, yakiwa na kauli mbiu “Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Taifa Endelevu.”