Na Ruja Masewa, JamhuriMedia, Iringa

Wakili Msomi na Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Deogratius Mahinyila amedai, Chama cha Mapinduzi (CCM) kinawatengenezea Polisi njia kwenda motoni.

Mahinyila alisema hayo mwishoni mwa wiki kwenye ziara ya Chadema ya No Reform! No Election iliyofanyika Kata Migoli, Jimbo la Isimani Iringa Vijijini.

Akizungumza kwenye Mkutano wa hadadhara uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wao Mstaafu Dkt. Wilbroad Slaa, Askofu Maximilian Mwanamapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa Chadema John Heche, Mahinyila alidai,
“Kitendo cha CCM kuwatumia Jeshi la Polisi, Walimu na Usalama, kuingiza Kura Feki, Kuwateka na kuwaua wakati wa Uchaguzi ili Chama hicho kishinde au kupita bila kupingwa, ni kuwatengenezea njia Polisi na wengine kwenda motoni”.

Akinukuu; Neno la Mungu kwenye Biblia Kitabu cha Luka 3:14 ambapo Yesu aliwaambia Polisi Mambo matatu kwamba, Msimdhulumu mtu, Msimshitaki mtu kwa Uongo, na Toshekeni na mishahara yenu.

Lakini baadhi ya Polisi wa nchi hii, Wanadhulumu Wananchi, Wanawabambikizia kesi za uongo, na Mishahara yenu haitoshi, huku fedha zenu za kufa na kuzikana zikiliwa na wahusika hawachukuliwi hatua!.

Kwa upande wake Askofu Mwanamapinduzi alidai, kila siku watu wanapotekwa na kuuawa, CCM inataka Viongozi wa dini wamsingizie Mungu kwamba waseme, ‘Bwana alitoa na Bwana alitwaa Jina lake lihimidiwe’.

“Nataka niwaambie sasa hatutasema tena ‘Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe’, ila tutasema Bwana alitoa na CCM imetwaa, jina lake lilaaniwe”.

Katika mkutano huo, alipoinuliwa Dkt. Slaa, kwa mara ya kwanza alitoa Siri yake ya moyoni kwa nini aliacha Upadri, ambapo alianza kwa kuuliza, kuna Wakatoliki hapa wanyoshe mkono? Ndiyooo!, Kuna Wakristo hapa? Ndiyoo! Kuna Wa-Islam hapa Wanyoshe Mkono! Ndiyoo?

Alisema, kuna Padre aliiba fedha, nilipotaka achukuliwe hatua mahakamani, Uongozi wa wa Kanisa ulimtetea Padre Mwizi.

“Kama na sisi ni Wacha Mungu wa kweli wa dini zetu, tusitetee Maovu ya CCM. Tuungane kwenye No reform No Election.

“Tukishindwa, Imani ya Ukristo na Uislamu wetu hatuna! Wala tusijidanye kwa kuwa tunatetea Wizi”.alisema Dkt. Slaa.

Aidha Makamu Mwenyekiti Heche alionyeshwa kukerwa na Kauli ya Katibu Mwenezi na Itikadi wa CCM Amosi Maķala aliyedai, Michezo ya Kubeti ni Ajira, ni sehemu ya Ajira kwa sababu inahamisha fedha na kwenda kuwanufaisha wageni (Wachina) wenye michezo hiyo.