URI limethibitishiwa.

KAPS ilizishinda kampuni kadhaa za Kitanzania zilizoshiriki kuwania zabuni hiyo ambayo uamuzi wake ulitangazwa Septemba 13, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, tayari ameiandikia KAPS Ltd barua ya kuwataarifu ushindi wao kwenye zabuni hiyo.

Kampuni hiyo itatakiwa kulilipa Jiji la Dar es Salaam kiasi cha Sh bilioni 54 kwa mwaka katika eneo lake la makusanyo ya ushuru wa magari ambalo ni Kanda ya Ilala.

JAMHURI imeelezwa kuwa KAPS walishinda baada ya kuonesha kwamba walikuwa tayari kulilipa Jiji kiasi cha Sh 229,166,667 kwa siku kutokana na ada ya maegesho katika Kanda ya Ilala.

Wakati makusanyo hayo yakionekana makubwa, habari za uhakika kutoka ndani ya Jiji zinaonesha kuwa ada ya maegesho ya magari itapanda kuanzia Januari, 2017 kutoka Sh 300 kwa saa kama ilivyo sasa hadi Sh 500 kwa muda huo.

Endapo Jiji litafanikiwa kuingiza Sh milioni 229.1 kwa siku, kiasi hicho cha fedha kitakuwa ni cha juu mno ikilinganishwa na kiasi cha Sh milioni 100 pekee kwa mwezi, kwa jiji zima la Dar es Salaam kilicholipwa na moja ya kampuni ya mwanasiasa maarufu nchini.

Barua ya Liana inaonesha kuwa ada ya maegesho kwa Kanda ya Kinondoni itakusanywa na kampuni ya Ubapa Company yenye makazi yake jijini Dar es Salaam. Kampuni hiyo itatakiwa kulilipa Jiji Sh bilioni 14.377 kwa mwaka.

Mshindi wa zabuni kwa kazi hiyo kwa Kanda ya Temeke ni kampuni ya Hepautwa Investment and General Brokers Limited yenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

Kampuni ya Hepautwa itatakiwa kulilipa Jiji kiasi cha Sh bilioni 5.644 kwa mwaka kutokana na ada hiyo ya maegesho.

Kampuni ya KAPS imekuwa ikikusanya ada za maegesho katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo Mlimani City, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Msemaji wa Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe, alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu zabuni hiyo anasema hakuna sheria yoyote iliyokiukwa katika mchakato wa kumpata mzabuni huyo na kwamba jiji limefuata sheria kama inavyotakiwa.

“Zabuni ilitangazwa na waliojitokeza kuchukua fomu za zabuni hiyo walikuwa 34, lakini waliorudisha ni 17 tu, maombi yalipitiwa na wakapatikana waliopatikana ikiwa ni pamoja na hiyo kampuni unayoisema, mchakato ulikuwa wa wazi, ni vema kutambua kuwa hakuna mahali sheria inapozuia kampuni ya nchi ya kigeni kupata zabuni ndiyo maana zinatangazwa mpaka kwenye mitandao,” anasema Makwembe.

Anasema baada ya kupatikana kwa kampuni hizo, ulitolewa muda wa siku 7 kwa yeyote mwenye malalamiko kuhusiana na zabuni hiyo kuanzia Septemba 14-20 na hakuna mtu au kampuni yoyote iliyojitokeza kulalamikia ushindi huo, hivyo Jiji litaanza mchakato wa kuwapatia mikataba ya kazi.