Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
WAKAZI wa Lulanzi pamoja na Hospital ya Wilaya ya Lulanzi, Kata ya Pichandege ,Kibaha , mkoani Pwani wanakabiliwa na kero kubwa ya ukosefu wa maji na kukosa huduma ya nishati ya umeme wa uhakika .
Kero hasa ya maji imekuwa kilio kikubwa katika Hospital ya Lulanzi ambayo imekuwa ikitoa raslimali fedha sh 180,000 kila mwezi ,kiasi ambacho ni kikubwa .
Hayo yalijiri wakati Mkuu wa Wilaya ya Kibaha ,Nikkison Simon alipomwakilisha Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge ,kusikiliza na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa Kata ya Pichandege,Sofu na Kisabi wilayani Kibaha.
Mwenyekiti wa Lulanzi Ally Mkimwe na mkazi wa eneo hilo ,Josephat Methew walieleza , changamoto ya maji na umeme imekuwa kilio kikubwa .
“Wakati mwingine inakuwa mgao lakini mgao wenyewe haueleweki ,cha kushangaza kuna kubambikiwa bili ,watu hawana maji lakini unakuta unaletewa bill kubwa ya maji wakati maji yenyewe hatuna ya uhakika” amesema.
Josephat alitoa kilio kingine cha kiwanda cha KEDS ,ambacho kinatiririsha maji machafu ,na kuchoma moto taka zilizotumika kiwandani hali inayosababisha moshi mkubwa unaleta athari za kiafya kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo .
Awali Diwani wa Kata ya Pichandege, Karim Mtambo alifafanua ,ni kweli kero hiyo ipo na ameifikisha mara kadhaa katika vikao vya Halmashauri na kuchukua hatua lakini wahusika wa kiwanda hicho cha KEDS hawana majibu ya kuridhisha.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kibaha ,Dkt. Peter Nsanya alikiri kuwepo kwa changamoto ya maji ,ambapo wananunua maji ya kwenye maboza .
Kuhusu nishati ya umeme Hospital ya Wilaya Lulanzi alieleza ,umeme upo ila changamoto inajitokeza wakati umeme unapokatika ambapo kwasasa changamoto hiyo itakwisha kwani wameshapata jenereta (milioni 50).
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nikkison Simon alisema, licha ya kuwepo changamoto hizo lakini Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kupigania kutatua kero ya maji na umeme nchini.
Nikkison ,alisema tatizo la maji Lulanzi linakwenda kuwa historia baada ya mradi wa maji Pangani kukamilika.
Akijibu kuhusu tatizo la kiwanda cha KEDS kulalamikiwa kutiririsha maji na kuchoma moto taka zinazosababisha Moshi mchafu kwa afya ya binadamu , Nikkison alieleza atafika kiwandani hapo kujionea hali halisi.
“Wawekezaji wanatusaidia katika ajira ,Keds imetoa ajira kwa wananchi, inasaidia jamii lakini isiwe chanzo cha kuwaumiza watu, tutakaa nao kutatua kero hizi zinazolalamikiwa “
Nikkison alibainisha kwamba ,matarajio ya wilaya ni kuwa na viwanda 500,vipo 12 vinaendelea kujengwa na matarajio ni kupata ajira zaidi ya 100,000″ kwahiyo wawekezaji hawa wanasaidia jamii ila waondoe vikwazo vinavyosababisha kero kwa wananchi wanaowazunguka.
Meneja wa DAWASA Kibaha ,Alpha Ambokile alieleza , Changamoto ya maji Lulanzi inakwenda kujibiwa na mradi wa maji wa Pangani ambao utanufaisha wananchi takriban 14,868 wa maeneo ya Kibaha -Msufini, TAMCO na Pangani na Lulanzi.
“Awali ilipangwa kujenga tanki dogo la kunyonyea maji mtaa wa River road, kupitisha bomba la inchi 12 kwenye barabara ya kuelekea hospital ya wilaya Lulanzi na kuelekea Pangani linajengwa tanki la kuhifadhia maji la ujazo wa lita milioni sita”
Ambokile alieleza, hadi sasa Mkandarasi ameshapitia eneo la mradi ili aanze kazi wakati wowote na malipo yatafanyiwa kazi na wizara ya maji.
Kwa upande wake ,Meneja wa TANESCO mkoani Pwani, Mahawa Mkaka alisema kuwa, lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata umeme.
“Tumeingiza kwenye mpango kwa mwaka wa fedha unaoanza zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya eneo la Lulanzi”alisema Mkaka.
Kuhusu kukosa umeme wa uhakika eneo la Kosovo alieleza, kwasasa wanafanya maboresho ya miundombinu wanabadilisha nguzo za miti na kuweka za zege, wanabadilisha nyaya ,na baada ya wiki mbili tatizo litakuwa limeisha.