Sisi zaidi ya wakazi 2,500 wa maeneo ya Kwembe Kati, King’azi, Kisopwa na Mloganzila katika Kata ya Kwembe tunakuomba Rais Samia Suluhu Hassan utusaidia kulipwa fidia zetu.
Kwa mara ya kwanza tulivunjiwa nyumba zetu na serikali tangu Septemba, 2008 baada ya kututaka tupishe eneo hilo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lakini hadi sasa hatujalipwa fidia na hatujaelekezwa sehemu ya kuishi na kupata mahitaji yetu.
Kwa niaba ya wakazi wenzangu (mimi Gilbert Lutwaza), tumekuwa tukitangatanga kutafuta fidia hiyo kwa miaka kadhaa bila mafanikio na kutufanya tuishi kwa shida.
Kimsingi, tuliamriwa na serikali kutolima mashamba yetu, kutojenga nyumba kwa ajili ya makazi/biashara na kutofanya shughuli yoyote ya maendeleo kwa maisha yetu katika maeneo tajwa hapo juu tangu wakati huo.
Kibaya zaidi, ni kutoelekezwa makazi yetu mapya yatakuwa wapi na tutajikimu vipi? Na sasa hivi unakaribia mwaka wa 14 2008 – 2022!
Jambo la kusikitisha na kukatisha tamaa ni kuona tangu maeneo yetu yafanyiwe tathmini mwaka 2008/2009 na kutuamuru tuondoke tumeathiriwa na mradi wa upanuzi wa MUHAS, tumekwama kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kushindwa kujipatia riziki kwa kutumia ardhi tuliyojaliwa na Mungu kutokana na kupisha ujenzi huo.
Baadhi yetu tumeishi zaidi ya miaka 40 katika maeneo niliyotaja kama Mzee Nkongogolo wa Kisopwa, Hamidu Busanga wa Kwembe Kati / King’azi, Wilfred Mwabulambo wa Kwembe, Mzee James Bwana wa Mloganzila Kibamba na wengine wengi wamekwisha kufariki dunia kwa sababu ya kutoamini kilichotokea, kwa kutuondoa katika makazi yetu yaliyobaki kama tegemeo letu la kujikimu.
Hawa wote na wengine tuliobaki na kama binadamu wa kawaida, tulihitaji na bado tunahitaji makazi yanayoeleweka. Badala yake tuliachwa barabarani na kutojua la kufanya ili tuendelee kujikimu na kuishi.
Hadi sasa serikali haijatueleza hatima yetu katika kuendelea kusubiri bila kufanya shughuli za kutuletea kipato wakati miaka inazidi kwenda.
Hakika, hali hii imetuweka katika msongo wa mawazo na ni wazi kwamba hatuwezi kuendelea kusubiri bila kikomo juu ya kupatikana kwa haki yetu ya makazi na kuishi.
Pia hali ilivyo sasa inadhihirisha kwamba ardhi yetu inanajisiwa na tumeachwa barabarani bila makazi kwa sababu ya kupisha ujenzi wa taasisi za serikali, barabara, hifadhi za wanyamapori na kadharika.
Katika hali hii, haki ya kuwa na maisha yenye utu, ubinadamu na kuheshimika inaendelea kutoweka chini ya baadhi ya viongozi wetu wa sasa.
Pia ikumbukwe na kuzingatiwa kwamba binadamu ni mtaji mkubwa unaostahili uwekezaji stahiki (i.e affected persons in the areas taken over for MUHAS expansion, like any other human beings, deserve special respect for life).
Wananchi tuliokuwa tunaishi katika maeneo niliyotaja, baadhi yao wakiwa wastaafu wanaendelea kuteseka tu na wana matumaini na kutarajia viongozi wao, ukiwamo Rais Samia ututendee haki na kuonyesha moyo wa huruma katika kupata haki zetu na kututoa katika mateso tunayopata kwa sababu hakuna kitu kibaya maishani kama kukosa chakula na makazi kwa wananchi walioathirika.
Hadi sasa hakuna asiyejua kama wananchi tuliokuwa tunaiishi maeneo yaliyochukuliwa na serikali kwa ajili ya upanuzi kwa kisingizio cha kufanya utafiti wa kutumia miti shamba kwa matumizi ya MUHAS tunahitaji na kustahili fidia kwa maeneo yetu yaliyochukuliwa kinyemela.
Pia sote tunatambua kwamba mamlaka waliyopewa viongozi wetu na Mungu ni kwa ajili ya kuwastawisha wananchi na isiwe kuwatesa kama ilivyo sasa.
Katika kuhangaika sehemu mbalimbali kwa njia ya uwakilishi, wananchi wa maeneo niliyotaja, tunakiri kupokea sehemu tu ya fidia tunayostahili katika maeneo yetu ambayo ni mazao yetu, majengo na mali kidogo iliyokuwa juu ya ardhi.
Ila malipo kwa ajili ya ardhi hayajafanyika hadi sasa. Leo miaka mingi imepita na ikumbukwe kwamba Juni, 2009, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, akiwa bado madarakani na wakati huo akiwa ziarani mkoani Tanga, aliahidi wananchi wa maeneo yanayohusika walipwe fidia wanazostahili ikiwamo kwa ardhi yetu.
Pia katika ziara hiyo hiyo, Kikwete, aliahidi kwamba serikali itawapa chakula wananchi waliokumbwa na janga la njaa Oktoba19, 2010.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana (kabla ya Ubungo kuwa wilaya mpya) wakati huo akiwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano aliofanya na wananchi na viongozi wa Kibamba mbele ya Ofisi ya Serikali ya Mtaa Kwembe, alitubainishia kwamba serikali imekubali na iko tayari kutulipa fidia ya ardhi kwa kila mmoja wetu aliyeguswa na mradi wa MUHAS ya kiwango cha Sh milioni tisa kwa ekari moja, pia thamani hii ilishatamkwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Rugimbana alituahidi kutoa ushirikiano kwa kamati teule iliyokuwa ikiwakilisha wananchi kufuatilia na kuhakikisha kufanyika kwa malipo kama inavyostahili baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010 kwa sababu fedha kwa madhumuni hayo zilikuwa tayari zimepatikana.
Wakati huo huo Serikali ya Korea Kusini ilikwishatoa dola milioni 76 za Marekani kwa Tanzania kwa ajili ya mradi huo kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Katika hili, wananchi tulioguswa na mradi huo hatuoni sababu ya msingi ya kutolipwa fidia kwa ardhi yetu hadi leo.
Muda ulivyoendelea kwenda, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alishindwa kutusaidia waathirika wa mradi huo, badala yake alielekeza nguvu na juhudi zake kujitafutia maeneo mengine ya kumiliki kwa lengo lake binafsi, kama eneo ilipo shule yake ijulikanayo kwa jina la Barbro Johansson Model Girls-Kwembe.
Pamoja na mambo mengine, sisi tuliokuwa wakazi wa maeneo yaliyochukuliwa kwa ajili ya mradi huo tulionekana hatuna thamani machoni mwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Ndiyo maana hadi leo tuliobaki hai tunaendelea kuteseka huku na huko barabarani, na hii inasikitisha na kutuongezea kiwango cha msongo wa mawazo.
Rais Samia, Katiba ya nchi yetu inaturuhusu kumiliki ardhi pamoja na mali iliyo juu yake na utaniwia radhi kwa kukuchosha kwa maelezo marefu, lakini natambua hauna hata nafasi ndogo ya kupumzika na nia yetu kubwa ni kukupa picha kamili katika kutafuta msaada wako kwetu tulioathirika kwa upanuzi wa mradi huo.
Nia yetu ya kuleta maombi kwako ni kuomba utusaidie waathirika wa maeneo niliyotaja kwa jicho la huruma. Ni vema pia utambue kwamba tuliondolewa katika makazi na mashamba yetu kwa ajili ya kupisha upanuzi huo bila maelekezo tutaishi wapi na kwa sasa tunasononeka na tuko katika hali ya kukata tamaa.