Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Kaliua

WAKAZI 359,577 wanaoishi katika vitongoji, vijiji na kata mbalimbali Wilayani Kaliua Mkoani Tabora wamenufaika na miradi ya maji iliyotekelezwa na serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Hayo yamebainishwa jana na Meneja wa RUWASA Wilayani humo Mhandisi Mapambano Boniface alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji miradi ya maji safi na salama kwa wananchi katika kikao cha madiwani wa halmashauri hiyo.

Amefafanua kuwa wakazi wanaopata huduma ya maji safi hadi sasa ni zaidi ya asilimia 53 ya wakazi wote wa Wilaya hiyo wapatao 678,447 na maeneo yote ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo kuna miradi inayoendelea kutekelezwa.

Meneja ameeleza kuwa mahitaji ya maji katika Wilaya hiyo yanakadiriwa kufikia lita za ujazo mil 14.4 kwa siku na hali ya upatikanaji huduma hiyo Kiwilaya sasa imefikia asilimia 53 ambayo ni sawa na uzalishaji wa lita mil 7.6 kwa siku.

‘Miradi zaidi ya 13 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika maeneo mbalimbali na mingine mipya inayogharimu zaidi ya sh bil 2.6 inatarajiwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2024/2025’, amebainisha.

Mhandisi Boniface amedokeza kuwa miradi hiyo itakapokamilika upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Wilaya hiyo utaongezeka hadi kufikia asilimia 79 ifikapo mwezi Juni mwakani.

Katika kukabiliana na changamoto ya maji kwa baadhi ya vitongoji, vijiji na kata katika Wilaya hiyo amesema wanatarajia kutekeleza miradi ya uchimbaji visima na mabwawa ya maji ikiwemo kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi.

‘Tumepokea kiasi cha sh mil 598.9 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji katika kata ya Ichemba ambalo linatarajiwa kufikisha huduma ya maji safi kwa wakazi wa vijiji 28, kupitia mradi huu wakazi zaidi ya 143,000 watanufaika,’ ameeleza.

Ametaja baadhi ya miradi iliyopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kuwa ni wa Kijiji cha Usimba, Kombe, Selelii, utafiti wa maji chini ya ardhi sambamba na uchimbaji visima 25 katika vijiji zaidi ya 20 unaogharimu sh mil 550.

Mingine ni upanuzi mradi wa maji katika Kijiji cha Kashishi kwenda Kagera, Kijiji cha Kazaroho kwenda Nsimbo, ukarabati visima 70 kwa kubadilisha vipuri, usanifu wa Bwawa la Maji katika Kijiji cha Zugimlole na utafiti na uchimbaji visima 10 katika Majimbo ya Kaliua na Ulyankulu.