Mwenendo wa takwimu za kuzaliwa watoto duniani zinaashiria kuwa Bara la Afrika litakuwa na vijana wengi zaidi kuliko maeneo mengine ya dunia ifikapo mwaka 2050. Ni suala ambalo linatoa fursa na wajibu mkubwa kwa Bara la Afrika katika uhusiano wa kimataifa.

Wastani wa ongezeko la watu barani Afrika ni asilimia 2.5; ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 1.2.

Ipo hofu kuwa kuendelea kushuka kwa wastani wa ongezeko la watu duniani ni tishio kwa uwepo wa binadamu duniani. Na mfano rahisi kabisa wa kuona hatari hii ni itakapotokea vifo vinavyotokea duniani vikizidi jumla ya watoto wanaozaliwa. Kimahesabu wanawake waliopo duniani wanapaswa kuwa na watoto wasiopungua wawili ili kuepuka athari hii.

Idadi hiyo inaposhuka chini ya watoto wawili na ikiendelea hivyo kwa muda mrefu itafika muda watu wataisha duniani.

Tayari yapo maeneo ya dunia ambako wastani huu umeshuka chini ya 2. Katika nchi wanachama za Umoja wa Ulaya (EU) wastani ni 1.58 kwa mwaka 2014. Japan, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, ina wastani wa 1.4.

Kwa kawaida, kila suala linakuja na uzuri na ubaya wake. Mipango mingi inayoambatana na uzazi wa mpango inajenga hoja kuwa wazazi wenye familia ndogo wanaongeza uwezo wao wa kutunza watoto wao na kuwapa elimu, pamoja na huduma za msingi kwa urahisi zaidi kuliko wanapokuwa na familia kubwa. Huu ni uzuri wa kuwa na familia ndogo.

Hata hivyo, jambo zuri likifanyika kwa muda mrefu linaweza kuleta athari mbaya. Kupungua kwa wastani wa uzazi duniani kunaleta changamoto kubwa zaidi kuliko ile inayokabili familia yenye watoto wengi.

Hivi karibuni tumesikia habari juu ya uteuzi wa waziri nchini Uhispania ambaye ana jukumu la kupanga mikakati ya kuhimiza raia wenzake kuzaa watoto wengi zaidi.

Nchi inapopunguza kasi ya kuzaa, inajiongezea raia kwenye kundi la wazee ambao, si tu wanakuwa hawachangii katika huduma na uzalishaji, bali pia wanabebesha taifa gharama za kuwatunza. Baadhi ya gharama hizi ni pamoja na huduma za afya na malipo ya pensheni kwa wazee.

Mzigo wa kodi zinazotozwa kuchangia gharama za serikali unabebwa na kundi la vijana wafanyakazi, na waajiri wanaochangia pato la taifa. Ni mzigo ambao utaongezeka mwaka hadi mwaka kwa sababu ya kukosekana kwa vijana watakaoingia kushika nafasi za wazee wanaofikia umri wa kustaafu na wanaokuwa wategemezi kwa familia zao na kwa taifa.

Baadhi ya sababu za kupungua kwa kasi ya uzazi duniani ni mabadiliko ya kitamaduni katika nchi ambazo zilianza kutoa fursa kwa wanawake wengi zaidi kutoka jikoni na kuanza kuajiriwa au kufanya shughuli za kiuchumi ambazo, kwa desturi, zilifanywa na wanaume. Kutokana na ajira wanawake walijiongezea uwezo wa kujitegemea, na kuanza pia kuchukua uamuzi wa kutozaa watoto wengi au kutozaa kabisa.

Suala la elimu pia ni chanzo kingine cha kupunguza kasi ya uzazi. Muda mrefu uliotumika kwenye masomo umesababisha baadhi ya wazazi, ama kuchelewa kuzaa, au kuamua kutozaa kabisa. Na hili lina ukweli kwa wanawake na wanaume wanaotumia muda mrefu wa maisha yao kusaka elimu.

Kwa kuendelea kuwapo kwa zile tamaduni ambazo zinamweka mwanamke nyumbani na jikoni inaaminika kuwa Bara la Afrika litaendelea kuwa na msingi unaolinda kuwapo kwa familia zenye watoto wengi. Hali kadhalika, taarifa zinaeleza kuwa upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya kiwango cha kuelimika kwa raia, na kasi ya kuzaliana. Elimu inavyozidi kuongezeka, basi kasi ya kuzaliana inazidi kupungua.

Maana yake ni kuwa bado kwa muda mrefu Bara la Afrika litaendelea kuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu wake wakati maeneo mengi ya dunia yakipungukiwa na idadi hiyo. Lakini ni hali ambayo itabadilika kadiri elimu inavyoongezeka, na kadiri huduma za afya zinavyoboreshwa.

Pamoja na kelele na jitihada zilizopo kwenye nchi nyingi zilizoendelea kudhibiti wahamiaji kutoka nchi masikini, pamoja na zile za Afrika, itafika wakati kuwa hali hii ya kukabiliwa na ongezeko la wazee katika nchi zao itawalazimu kugeukia Afrika itakayokuwa na idadi kubwa zaidi ya vijana watakaoweza kuziba nafasi za ajira.

Mwaka 2015 viongozi wa Bara la Afrika waliohudhuria kikao cha Umoja wa Afrika (AU) walipitisha mkakati wa maendeleo, Agenda 2063, unaokusudia kuimarisha Bara la Afrika kimaendeleo na kiteknolojia ndani ya miaka 50 ijayo.

Ni mkakati wenye madhumuni ya kuleta maendeleo endelevu, kuimarisha umajumui wa Afrika, kuimarisha uhuru wa kisiasa na kiuchumi, kujenga misingi ya utawala bora na uzingatiaji wa utawala wa sheria, kudumisha amani, kudumisha kwa mila na desturi zetu; na la muhimu sana kwa maoni yangu, ni kufanya Bara la Afrika kuwa mshiriki muhimu katika masuala ya ulimwengu. Afrika haitakuwa mtazamaji tu, bali itakuwa mshiriki aliye sawa na washiriki wengine.

Kama Uhispania wameona umuhimu wa kuteua waziri wa kusimamia mkakati wa kuongeza kasi ya kuzaa miongoni mwa raia wake, sioni kwanini Bara la Afrika lisiweke mikakati yake ya kuhimiza Waafrika kuendeleza mkakati wa aina hiyo. Tamaduni ya kuzaa watoto wengi imeshapotea katika mabara mengine, na ikitufikia sisi tutaanza kushuhudia mwisho wa uwepo wa binadamu. Waliocheka kusikia hiyo wizara mpya ya Uhispania hawawezi kuona kichekesho wakitafakari suala zima kwa kina.

Matatizo ya dunia ya miaka 100 kutoka sasa yatakuwa tofauti na matatizo tunayoyatarajia miaka 50 kutoka sasa. Agenda 2063 ikitekelezwa kama ilivyokusudiwa, tunatarajia kuiona Afrika moja, imara kiuchumi na kisiasa, yenye nguvukazi iliyosheheni vijana, na ikiwa imezungukwa na mataifa ulimwenguni yenye nguvukazi iliyozeeka.

Viongozi wa Bara la Afrika wanao wajibu wa kulinda watu na rasilimali za Bara hili kwa manufaa ya Waafrika, na pia kwa manufaa hapo baadaye ya watu wote ulimwenguni.