Umoja wa Mataifa (UN) umeitenga Oktoba Mosi ya kila mwaka kuwa Siku ya Wazee Duniani, ambapo mataifa mbalimbali huiadhimisha kwa namna tofauti, ikiwamo kukumbushana haki za wazee.
Kaulimbiu ya siku hii kwa mwaka huu ni ‘Safari ya kuzeeka kwa usawa’, ambayo imewekwa mahususi na UN ikitambua kwamba Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yatafikiwa pale tu watu wa umri wote watakapokuwa wamejumuishwa.
Kwa kawaida maadhimisho ya siku maalumu hufanyika kwa furaha, huku wahusika wakifurahia matunda ya kazi zao, lakini kwa hakika hali haipo hivyo kwa wazee wa Tanzania.
Wakati wakiungana na wenzao wengi duniani katika maadhimisho hayo, wazee wa Tanzania wameendelea kulalamika, japo bila sauti kubwa, kwamba mchango wao kwa jamii na kwa taifa zima hauthaminiwi; au kwa maneno mengine wametelekezwa.
Hakuna shaka kwamba taifa letu lipo hapa lilipo kutokana na mchango mkubwa uliofanywa na wazee wetu ambao idadi kubwa tayari wamekwisha kutangulia mbele ya haki.
Udugu, upendo, umoja, amani na kila aina ya tunu ambazo kizazi hiki kinaogelea ndani yake kwa furaha na vicheko, zimetengenezwa na kulindwa kwa umoja na upendo wa hali ya juu na wazee hawa ambao sasa wamebaki kama watazamaji tu.
Sera mbalimbali zimetungwa kuhusu wazee na namna ya kuwahudumia, lakini hazitekelezwi au hazitekelezeki! Zimesalia kwenye makabrasha na kusababisha idadi kubwa ya wazee kuaga dunia wakiwa na kinyongo mioyoni.
Kwa mfano, tujiulize, sera ya matibabu bure kwa wazee wenye zaidi ya miaka 60 inatekelezwa kwa ufanisi? Ni wazee wangapi wanafurahia huduma bure na bora ya afya wanapokwenda kwenye vituo vya afya au hospitalini?
Ni wazee wangapi wanaorudishwa majumbani kwao bila kupata matibabu kwa sababu hospitali hizo hazina dawa? Hali hii inawanyong’onyeza sana wazee waliotumia nguvu na ujana wao kulitumikia taifa katika kilimo, machimbo ya madini, uvuvi au kazi za kuajiriwa.
Wazee wamekuwa wakipiga kelele kuomba serikali iwasaidie japo kupandisha pensheni yao kutoka Sh 50,000 ya sasa. Ni ukweli kwamba fedha hizi ni chache sana kwa uhalisia wa maisha ya leo.
Kuna wakati pensheni ilipandishwa hadi Sh 100,000, lakini kuna wazee ambao walistahili nao kupandishiwa pensheni hii hawakufanyiwa hivyo hadi wameaga dunia! Hii ni laana kwa taifa.
Bunge ambalo ndilo hutunga sheria, haliwakumbuki wazee na bahati mbaya wazee wenye kipato cha chini hawana wawakilishi huko.
Tunaamini kuwa wakati umefika kwa serikali kujipanga katika kuzitekeleza sera zote zinazoyagusa masilahi ya wazee, tukiamini hawa ni asilimia ndogo sana ya Watanzania wa leo.
Bajeti ya mwaka ujao wa fedha inapaswa kutenga fungu la fedha kwa ajili ya kuwapa pensheni wazee wote, si waliokuwa wameajiriwa pekee; na pensheni yenyewe ikaribie walau kima cha chini cha sasa cha mshahara wa mtumishi wa umma.