Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakandarasi wanaokiuka mikataba ya ujenzi kwa kuchelewesha miradi.
Kunenge alitoa agizo hilo ,wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa kilichofanyika Kibaha, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati ili kuepusha hasara kwa serikali na mateso kwa wananchi kutokana na ubovu wa barabara.
“Shirikianeni na wanasheria wenu ili kuwabana wakandarasi wasiozingatia mikataba yao, Ni muhimu kuhakikisha hawaisababishii serikali hasara,” alisema Kunenge.
Aliongeza , serikali inatoa fedha kwa lengo la kuboresha miundombinu na kutatua changamoto za wananchi, hivyo miradi ya barabara lazima ikamilike kwa wakati.
Kunenge alisema pia ni muhimu kuangalia mbinu za kuwadhibiti wakandarasi bila kuchelewesha utekelezaji wa miradi.
“Ikiwa kuna namna ya kuwabana ili wamalize miradi kwa wakati, fanyeni hivyo. Kutengua mikataba mara nyingi huchukua muda mrefu, na wakati huo wananchi wanaendelea kuteseka,” alifafanua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, alieleza kuwa baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakisababisha changamoto kubwa, akitolea mfano mmoja ambaye ameshindwa kusambaza kifusi cha tope hali inayoweza kuathiri zaidi barabara kipindi cha mvua.
“Mkandarasi asiyekuwa na uwezo wa kutekeleza mradi ni vyema aondolewe na nafasi yake apewe mtu mwingine mwenye uwezo,” alieleza Magoti.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage, alithibitisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya mkandarasi aliyekiuka masharti ya mkataba.
Mwambage alifafanua ,tayari wamebaini dosari na taratibu za kisheria zinaendelea ili kufuta zabuni yake.
Hatua hizi zina lengo la kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma bora za miundombinu kwa wakati.