Na Mwandishi Wetu
Chama cha Wakala wa Meli Tanzania (TASAA) kimeunga mkono mpango wa Serikali wa kuleta uwekezaji wa kampuni ya DP World kwenye bandari ya Dar es Salaam, kikisema kuwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza ufanisi wa bandari na kukuza uchumi wa Tanzania.
TASAA imesisitiza kuwa DP World ni moja ya kampuni kubwa duniani za uendeshaji wa bandari ambazo zinaweza kuleta meli nyingi kuja Dar es Salaam, kuongeza idadi ya shehena inayohudumiwa na bandari na kuimarisha ufanisi wa bandari kwenye kuhudumia shehena.
Mwenyekiti wa TASAA, Daniel Mallongo, amesema kuwa kuna changamoto kadhaa za ufanisi kwenye bandari ya Dar es Salaam zinazolikosesha taifa mapato, ambazo zinatarajiwa kupatiwa ufumbuzi na uwekezaji wa DP World.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upungufu wa magati ya kuhudumia mizigo na kukosekana kwa mfumo wa kisasa wa kuhudumia mizigo bandarini kwa kasi.
“Ukosefu wa magati ya kutosha bandarini (Dar es Salaam) unasababisha meli kukaa nje siku 4 mpaka 6. Hii ni gharama kubwa kwa wenye meli kubwa za mizigo kwa sababu gharama ya kukaa pale nje (outer anchorage) ni Dola za Marekani 25,000 (Shilingi milioni 60) hadi Dola 50,000 (Shilingi milioni 120) kwa siku,” alisema Mallongo.
“Ukiangalia meli inakaa siku 6 nje kabla ya kuhudumiwa, hiyo ni gharama kubwa. Na hizo gharama mara nyingi zinahamishiwa kwenye mizigo na kila mwenye mzigo kwenye hiyo meli ni lazima achajiwe gharama za meli kukaa nje.”
Alisema pia kukosekana kwa mifumo inayosomana kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) na uhaba wa nafasi ya kuhifadhia mizigo kwenye eneo la bandari ya Dar es Salaam ni changamoto nyingine kubwa.
“Haya mambo yote DP World ndiyo champion (kinara) wake. Ukimleta matatizo haya utapata ufumbuzi. Kama ni meli itakuja siku moja itandoka na ukipunguza gharama hiyo hata gharama ya kuleta mizigo Tanzania itashuka,” aliongeza katika mahojiano na kituo cha EFM Redio na TV leo jijini Dar es Salaam.
“DP World ni kati ya kampuni kubwa tatu duniani ambazo zinaendesha bandari mbalimbali. DP World inaendesha takribani bandari 64 duniani, unaongelea Afrika, Asia, Ulaya na hata bara la Amerika. Kwa muktadha huo, DP World ina uwezo mkubwa.”
Mwenyekiti huyo wa TASAA alizitaja Antwerp, London Gateway na New Jersey, kuwa miongoni mwa bandari zinazoendeshwa kwa ufanisi na DP World.
“Kwangu mimi niseme kwa uwazi kuwa DP World wana uwezo na wanastahili kuendesha bandari (ya Dar es Salaam),” alisisitiza.
Mallongo alisema faida ya uwekezaji wa DP World kwenye bandari ya Dar es Salaam ni kuwa utapunguza gharama za kupitisha mizigo na kuimarisha huduma na kufanya idadi ya shehena kuongezeka na hiyo itaongeza mapato kwa Serikali.
“Ukitaka kuongeza mzigo Dar es Salaam, lazima wenye meli wawe tayari kuja Dar es Salaam. Kama wenye meli wakiona kuna gharama za ajabu ajabu Dar es Salaam, wataenda kwa washindani wetu kama bandari za Maputo, Mombasa na Durban,” amesema.
Kuhusu upotoshaji kuwa bandari ya Dar es Salaam imeuzwa kwa DP World au kukodishwa kwao milele au kwa miaka 100, kiongozi huyo wa TASAA aliwataka Watanzania wapuuze uongo unaoenezwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati dhidi ya uwekezaji huo.
“Mimi siyo mwanasheria lakini najua kusoma. Unapoambiwa IGA au Intergovernmental agreement (illiyopitishwa na Bunge) ni framework (makubaliano tu ya msingi), mikataba yenyewe bado haijasiniwa,” alisema.