* Ni yule wa FC Lupopo
Kuna kila dalili kuwa safari ya usajili wa golikipa wa namba moja wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja, kujiunga na timu ya soka ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kukayeyuka, kufuatia taarifa kuwa huenda wakala wake, Ismail Balanga Bandua, akatimuliwa nchini muda wowote.
Wakala huyo kutoka DRC alikuja nchini kufanya mazungumzo na Kaseja ili akaichezee timu ya FC Lupopo ya huko.
Awali, Agosti 14, mwaka huu, Bandua alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mkazi Kisuti, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka ya kuishi nchini bila kibali kinyume cha kifungu cha 31 (1) (i) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji, Sura 54 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Bandua alikiri makosa hayo ambapo Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, alimhukumu kifungo cha miezi mitatu jela ama kulipa faini ya Sh 150,000. Alilipa faini hiyo na kujinusuru kwenda jela.
Taarifa za uhakika kutoka Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam zilizolifikia gazeti JAMHURI zinasema kwamba baada ya Bandua kulipa faini hiyo, alirudishwa tena mikononi mwa Idara ya Uhamiaji na kuwa kuna taratibu nyingine zinafanyika kati yake na idara hiyo.
Lakini pia kuna taarifa kuwa Mkongo huyo huenda akatimuliwa nchini kwa kile kinachodaiwa kuwa ana rekodi mbaya.
“Huyo jamaa tunaye hapa baada ya kulipa faini mahakamani, tunamfanyia mahojiano ila inaonekana ana rekodi mbaya, ni mtu mwenye mtandao mkubwa, kwa hiyo kuna kila sababu ya kumtimua hapa nchini,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Baada ya kupata taarifa za awali, Agosti 7, mwaka huu, askari kutoka kikosi cha Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam walifanya doria ya kawaida jijini Dar es Salaam na kumkuta Bandua akiwa katika moja ya nyumba za kulala wageni eneo la Magomeni Kondoa.
Baada ya msako alikutwa na hati tatu za kusafiria ambazo ni mali ya raia watatu wa DRC na moja ya raia wa Tanzania. Raia wa Tanzania ni Amani Simba, mchezaji wa kandanda aliyepata kukipiga na Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club ya Jijini.
Hali kadhalika, inasemekana kuwa Bandua aliwatapeli vijana wa kiume wawili, raia wa Nigeria waliopo hapa nchini kwa kisingizio cha kuwatafutia timu za soka ili wasajiliwe. Raia ambao mmoja wao alisema kuwa ana umri wa miaka 21 aliiambia JAMHURI kuwa yeye na mwenzake walikutana na Bandua wakiwa mazoezini katika moja ya viwanja vya mpira eneo la Kinondoni, Dar es Salaam.
“Alikutana na sisi pale tunapofanyia mazoezi eneo la Kinondoni, akasema kuwa sisi ni wachezaji wazuri kwa hiyo anaweza kututafutia timu ya kuchezea mpira na tukasajiliwa. Mimi nilimpa dola 650 za Kimarekani na mwenzangu alimpa dola 700,” alisema mmoja wa vijana hao (jina linahifadhiwa kutokana na taratibu za kisheria).
Kijana huyo aliendelea kusema kuwa baada ya hapo Bandua alikuwa akiwakwepa kila mara na kuwapa ahadi za ‘uongo na kweli’, na kuwa yeye na mwenzake wamekuwa wakiishi katika maisha ya shida bila kujua hatima ya fedha zao na usajili kama walivyoahidiwa.
“Tunachohitaji ni pesa zetu ili sisi twende zetu, maanake shida zote tunazozipata hapa ni kwa ajili ya huyu jamaa, kuna mambo mengine ambayo siwezi kuyataja kwa sababu ya kiusalama lakini ukweli ni kuwa kwa sasa hivi tunaishi kwa msamaria mmoja ambaye ameamua kutusitiri,” alisema kijana huyo ambaye anaongea kwa lafudhi ya Kinigeria.
Bandua alifika nchini hivi karibuni kwa lengo la kukamilisha taratibu za timu ya FC Lupopo ya DRC kumsajili kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Juma Kaseja. Lakini hadi anakumbana na mikasa hiyo hiyo alikuwa hajakamilisha mchakato huo.