Na Magrethy Katengu, JamuhuriMedia Dar es Salaam

Mtu mmoja ajulikanaye kwa jina la Mussa Khamis Bakari maarufu ‘buda ‘ (30) , Wakala wa Forodha, mkazi wa Temeke anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Twahir Selemani ambaye alikuwa rafiki yake na baada ya kumuua alimwibia pesa marehemu Tsh milioni 61 kutoka kwenye akaunti yake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 11,2024 Kamanda Kanda Maalumu Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro amesema walipokea taarifa Mei 1, 2024 majira ya saa 10:20 asubuhi huko maeneo Mbutu Kichangani, Kigamboni pembezoni mwa barabara itokayo Cheka kuelekea beach ya Kichangani ambapo uliokotwa mwili wa mtu mmoja mwanaume akiwa ameshafariki na baadae mwili huo ulitambuliwa kuwa ni Abdallah Twahir Selemani mkazi wa Chanika.

Kamanda Muliro amebainisha kuwa baada ya ndugu kumtafuta marehemu Mei 4, 2024 walipokea taarifa kutoka kwa mama wa marehemu Abillah Twahir Selemani ya kuwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha na Jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi na baadae iligundua kuwa Aprili 30, 2024 mtuhumiwa Mussa Khamis Bakari @Buda alikuwa na marehemu wakitumia gari namba T.928 DFY Suzuki Kei wakitokea Magomeni kuelekea Temeke, Kijichi mpaka eneo ulipokutwa mwili wa marehemu.

“Uchunguzi wa vitu mbalimbali umebainisha mtuhumiwa alimuua na baadae kwenda kutupa mwili huo pembezoni mwa barabara ulipookotwa na baada ya kutekeleza mauaji alichukua kadi ya benki ya marehemu na kwa nyakati tofauti tofauti alianza kutoa pesa kiasi cha shilingi Milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya marehemu” amesema Kamanda Muliro.

Hata hivyo imeonekana chanzo cha mauaji ni tamaa ya kutaka kuiba pesa kutoka kwa rafiki yake ambaye sasa ni marehemu na hivyo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi limefuatilia matukio ya unyan’ganyi na wizi wa pikipiki katika Jiji la Dar es Salaam na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 23 na pikipiki 39 zilizoibwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.

Kamanda amebainisha kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia mbinu ya kujifanya abiria na wakifika njiani hujitokeza watu wengine ambao humtishia dereva kwa mapanga na kumjeruhi kisha kumuibia pikipiki hiyo, wakatii mwingine pikipiki zinazokuwa zimeegeshwa nje hutumia mbinu ya kuunganisha waya, kuwasha na kuiba.

Sanjari na matukio kutokea ufuatiliaji wa Jeshil la Polisi umebaini watuhumiwa hao baada ya kuziiba pikipiki wamekuwa wakiziuza kwa gharama nafuu mikoa mbalimbali ikiwemo Mikoa ya Dodoma na Singida na ufutiliaji huo umefakiwa kukamata risiti za kugushi 18 za kusafirishia pikipiki za wizi, kadi 11 za usajili wa pikipiki za kugushi, kadi (03) za usajili wa magari za kugushi, vyeti mbalimbali vya kuzaliwa na kimoja cha ndoa vya kugushi, plate number (03) za pikipiki, kitabu kimoja cha bima ya magari, nyaraka mbalimbali za TRA.

Pia barua mbalimbali zenye nembo za jeshi la Polisi Tanzania, mihuri mbalimbali ya Manispaa ya Kinondoni,Temeke, IIala, Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, RITA, Mamlaka ya Bandari na mhuri mmoja wa moto ulioandikwa “United Republic of Tanzania” wenye nembo ya bibi na bwana, leaf 56 za kutengenezea kadi za vyombo vya moto, leaf 86 za kutengenezea vyeti vya vizazi na vifo vyenye nembo ya msajili wa vizazi

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam pia katika kusimamia mifumo ya kisheria ya haki jinai limeendelea kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya kihalifu na hatimaye kupatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu.

Pia Jeshi la Polisi limekuwa likichukizwa sana na vitendo vya ubakaji na ulawiti na katika hatua hiyo mwaka 2023 Juni, mshtakiwa Hussein Shomvi (50) fundi ujenzi, mkazi wa Chanika Zogoali alikamatwa na baadae kufikishwa Mahakama ya Kinyerezi na baada ya mashauri yake kusikilizwa tarehe 10 Juni 2024 alipatikana na hatia ya kosa kulawiti watoto wawili wa kiume wa shule ya msingi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

Washtakiwa wengine Shamim Hamadi @dj mush (30) Mkazi wa Kimara Mwisho, na Waziri Ramadhani (26) Mkazi wa Mbezi Luis na Seif Salum (19) mkazi wa Manzese wote kwa pamoja mwaka 2022 walifikishwa Mahakama ya Kinondoni mbele ya Hakimu Mkazi Nabwike Mbaba na baada ya mashauri yao kusikilizwa terehe 10 Juni 2024 walipatikana na hatia ya Unyangayi wa kutumia silaha na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Aidha Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mbalimbali, zitatunzwa na wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Please follow and like us:
Pin Share