Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kukutanisha wadau zaidi ya 1000 kujadili na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Septemba 9-10 jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 26, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk Ashatu Kijaji amesema mkutano huo viongozi watakaoshiriki mkutano huu ni mawaziri na makatibu wakuu kutoka Wizara za Kisekta; wakuu wa mikoa; wakuu wa wilaya; na wakurugenzi wa halmashauri.

Aidha amewataja wadau wengine kuwa ni pamoja na wizara na taasisi za serikali; mashirika ya umma, Sekta binafsi, vyuo vya elimu ya juu na asasi zisizo za serikali, wakurugenzi kutoka katika mashirika ya umma na wataalamu; Sekta Binafsi.

Dk Kijaji amesema Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali za mazingira ikiwemo uharibifu wa ardhi; uharibifu wa vyanzo ya maji; ukataji miti ovyo na uharibifu wa misitu; upotevu wa makazi ya wanyamapori na bayoanuai ambazo zimechangia kufifisha ustawi wa jamii na uchumi.

“Kwa kutambua mchango wa wadau katika kuhifadhi na kusimamia mazingira na mabadiliko ya tabianchi nchini, Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu Mkutano wa viongozi, wataalamu na wadau wa hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Septemba 9-10 jijini Dodoma,” amesema Waziri Kijaji.

Ameongeza Mkutano huo unalenga kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na fursa zilizopo katika biashara ya kaboni; usimamizi wa taka; mabadiliko ya tabianchi; nishati safi ya kupikia; upandaji miti na usimamizi na uzingatiaji wa Sheria nchini.

Please follow and like us:
Pin Share