Utandawazi kama mfumo unaoongozwa na kuongoza uchumi wa soko, hutumia mawasiliano ya haraka na mepesi katika shughuli zake. Mfumo huu ulipoingia duniani, ulitishia na kuhatarisha uwepo wa mambo mengi tuliyoyazoea. Dhana ya utandawazi ni somo pana, pekee na mahususi kulizungumzia. Bila kulifahamu hilo kwa undani, ni rahisi kujiingiza katika ugomvi usiokwisha. Nachelea kusema, hata uchaguzi wa mada yenyewe kutumia neno “chanya” ni kiashiria kuwa kuna ugomvi unaoendelea.
Tishio kubwa linaloendeleza ugomvi usiokwisha linatokana na mambo makuu mawili kwa kutaja tu bila kufafanua: kwanza, ujinga juu ya dhana nzima ya mawasiliano kwa njia ya mitandao, na pili ni kumomonyoka kwa madaraka na nguvu ya ushawishi kutoka kwa waliozoea kuwa nayo kwenda kwa wasiozoea kuwa na madaraka hayo. Hapo baadaye, labda, tutapata fursa ya kujadili haya mambo mawili yaani UJINGA na KUNG’ANG’ANIA madaraka yasiponyoke.
Kibonzo
Mwalimu wangu wa somo la utandawazi mwanzoni mwa miaka ya 1990, aliitambulisha dhana ya utandawazi kwa kutumia kibonzo. Kibonzo hicho kinaonyesha majambazi wawili, usiku wa manane, wamebeba jiwe kubwa liitwalo “Fatuma” (siyo Shangazi Fatuma”).
Majambazi hao, wanaiendea nyumba usiku ili watumie jiwe lile kubomoa mlango wapate kuingia ndani na kuiba. Kibonzo kinaonyesha mwenye nyumba yuko macho kule ndani na anaona kila hatua ya majambazi yale kupitia tundu dogo lililo mlangoni. Majambazi wanapofika mbele ya nyumba, wanabeba lile jiwe kwenye gunia na “kulibembeza” lile jiwe wakihesabu “…moja, mbili, tatu”. Mwenye nyumba kwa uangalifu mkubwa analegeza komeo zilizo ndani ya mlango. Majambazi wanapohesabu neno “tatu” na kusema “twende” kwa kurusha lile jiwe, mwenye nyumba anafungua mlango haraka kabla jiwe halijaugonga na kuupasua. Lile jiwe linaangukia sebuleni, na mlango unapona. Majambazi kuona vile, yanakimbia. Hayakuingia ndani. Matokeo yake, mali hazikuibwa, walio ndani hawakujeruhiwa, na mlango haukuharibiwa.
Fundisho la kibonzo
Kwamba, utandawazi hauepukiki. Kinachotakiwa ni watumiaji kuchagua wanachohitaji kwa uangalifu kwa sababu, ukikataa kuruhusu utandawazi, utasababisha matumizi ya nguvu ya utandawazi na kuingiza uharibifu wa mali, mila na desturi za kijamii. Kinachotakiwa ni jamii kuingia katika maridhiano na nguvu hii isiyoonekana ili kuishi nayo pasipo kutekana, kutesana wala kupotezana.
Matumizi ya nguvu katika kuzuia utandawazi ni hasara kwa jamii, si kwa utandawazi wenyewe. Kama nilivyosema, utandawazi upo – tuutake au tusiutake. Tunahitaji kuishi nao bila manung’uniko.
Matumizi ya nguvu, sheria kandamizi, na mawazo hasi dhidi ya utandawazi ni sawa na kusimamisha saa ili kuwahi tunakokwenda. Utandawazi una nguvu ya kudhibiti na uwezo wa kutodhibitiwa. Tunahitaji kuufungulia ili upite salama. Kuudhibiti utandawazi, inabidi utumie utandawazi pia.
Matumizi chanya mitandao ya kijamii
Kwa kuwa kuna “chanya”, bila shaka kuna “hasi”. Nimeombwa kuchokoza mawazo kuhusu matumizi chanya ya mitandao ya kijamii. Naelewa, maadui wa mitandao ya kijamii wana orodha ndefu sana ya matumizi hasi ya mitandao hii. Ninaelewa. Mimi ni mhanga [mwathirika] wa matumizi mabaya ya mitandao hiyo kama walivyo wengi katika jamii.
Kwa hiyo, busara hapa ni kujifunza kuishi na hali tusiyoipenda bila kuiumiza wala kuumizwa nayo. Tukumbuke daima, anayekuuzia vazi la kuzuia risasi (bullet proof), ndiye huyo huyo anayekwenda kutengeneza risasi ya kupenya vazi alilokuuzia jana yake.
Tulipopata uhuru mwaka wa 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius alitangaza maadui watatu wakubwa wanaolikabili taifa letu: Umaskini, Ujinga na Maradhi. Nimeweka ujinga katikati ya umaskini na maradhi kwa makusudi. Sehemu kubwa ya umaskini wetu na sehemu kubwa ya maradhi yetu, vinabebwa na ujinga wetu.
Tukifanikiwa kupunguza ujinga wetu, sehemu kubwa ya umaskini na maradhi yetu, vitashughulikiwa kwa urahisi zaidi. Matumizi chanya na sahihi ya mitandao ya kijamii ni njia “isiyoepukika” ya kuuondoa au kuupunguza ujinga wetu ambao ni msingi mkuu wa maradhi na umaskini wetu. Kwa uchache, zifuatazo ni faida chanya za matumizi chanya ya mitandao ya kijamii:
Kwanza, uhuru wa kujieleza: Wajinga wengi hujulikana wanapojieleza. Ili kuwasaidia hao, inabidi kuwaruhusu waseme ndipo tubaini ujinga wao na kuutafutia tiba. Kuzuia au kudhibiti uhuru wa kujieleza, ni kuuwekea mbolea ujinga ambao ni adui wa taifa na utaifa wetu. Naelewa hoja za wanasiasa na watawala wengi katika eneo hili kuwa “uhuru una mipaka”.
Kimsingi uhuru ukiuwekea mipaka inayoonekana, unakuwa si uhuru tena, bali “utumwa mstaarabu” au “uhuru wenye mipaka” – si uhuru kamili. Tunaweza tusipende sana maoni yangu haya, lakini ujinga si tusi, na kila mtu ni mjinga kwa jambo asilolijua. Wanaosisitiza mipaka katika uhuru wa kujieleza ni ‘wajinga’ katika dhana nzima ya uhuru kama mimi nilivyo mjinga wa kutoelewa wanaogopa nini.
Pili, maendeleo ni uhuru: Tulipopata uhuru tulikuwa na kauli mbiu ya UHURU NA MAENDELEO. Hivi sasa dunia nzima inakubali kuwa tafsiri sahihi na endelevu ya maendeleo ni UHURU, yaani, mchakato wa kila siku unaopunguza “vidhibiti uhuru” (unfreedoms). Ndiyo maana “kasi” ndicho kipimo cha awali kinachoeleza dalili za uwepo wa maendeleo. Magari yakienda pole pole, tunaongeza nguvu ya injini, tunaongeza barabara za juu na chini ya ardhi ili kasi iongezeke. Kwenda pole pole au kuongeza urasimu si dalili za maendeleo. Matumizi chanya ya mitandao ya kijamii yanachochea utamaduni wa kupenda kasi katika kutafuta suluhu za matatizo yetu.
Tatu, kufaidi uchumi wa soko: Soko ndilo kichocheo cha matumizi ya mitandao. Dunia nzima bila kutumia ngoma wala baragumu kuita watu wakutane chini ya mbuyu, inakutanishwa na mitandao ya kijamii. Katika uchumi wa soko kuna wauzaji na wanunuzi. Hata Kiafrika, anayenufaika na soko (gulio) ni yule anayepeleka bidhaa sokoni, siyo yule anayeenda kununua. Matumizi ya mitandao ya kijamii yamebadili kanuni hii kwa kuwafanya wanunuzi kuwa na nguvu kuliko wauzaji. Wanunuzi wanapanga bei na wauzaji wanakuwa wanyonge mikononi mwa wanunuzi. Ili kuleta uwiano katika soko, ni LAZIMA kuwezesha kizazi kipya kubobea katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Nne, uwanja wa kubadilishana ujinga: Kupitia mitandao ya kijamii, kunatokea biashara ya kubadilishana ujinga (exchange of ignorance). Asiyeenda katika uwanja huo, anabaki na ujinga wa aina moja kwa muda mrefu. Katika uwanja huu, hakuna anayemiliki ukweli, bali wote ni wamiliki wa ujinga na wanaenda kuuza ujinga wao ili wanunue ujinga mpya. Kuna aina za ujinga ukizipata kwenye ubongo zinageuka kuwa kinga ya kudumu dhidi ya maadui wengine wa hatari. Mchakato huu unaitwa “global learning au cross learning. Hivi sasa watu hatari kuliko magaidi ni wale wanaodhani wanamiliki ukweli na kudhani wao ndiyo kipimo halisi cha uzalendo, usahihi, uadilifu, na mamlaka ya mwisho. Ni mitandao ya kijamii tu inayoweza kuiepusha dunia na watu hawa hatari wa kizazi hiki na kijacho.
Tano, muungano usio na hati ya muungano (union without articles of union): Mitandao ya kijamii inaunganisha na kuondoa mipaka yote bandia. Ni muungano wa rika zote, rangi zote, itikadi zote, jinsia zote na hali zote za kiuchumi. Mipaka katika matumizi inakuza mgawanyiko na kuchochea chuki katika jamii. Hivi sasa tuna watumiaji wengi wa mitandao wanaotumia majina bandia. Hii si afya hata kidogo. Kundi hili linaficha utambulisho wake na kubaki na ujinga wao. Dawa ya ujinga si kuufunga jela, kuuteka, kuutesa, kuukemea, wala kuutungia sheria. Dawa ya ujinga ni kuelimisha. Kinyume chake, unaweza kufunga watu wajinga, lakini usiweze kufunga ujinga wao. Tuna idadi ya kutisha, tena ya watu wenye madaraka, wanaodhani ujinga unamalizwa na kifungo, au wanaodhani ukipata madaraka, umepata chanjo ya kufuta ujinga kichwani mwako. Hata hivyo, kuna watu si wajinga, lakini pia si werevu. Hawa nao, dawa yao si kuwapuuza. Ni kuwaelemisha kupitia shule isiyo na kuta za madarasa wala kengele, bali kupitia matumizi chanya ya mitandao ya kijamii.
Sita, utetezi na udhibiti: Matumizi chanya ya mitandao ya kijamii ni nyenzo nzuri ya utetezi katika jamii. Wasioliona hili ni wale wanaodhani kwa nafasi zao, hawahitaji kutetewa. Lakini pia, mitandao ya kijamii ina nguvu ya udhibiti wa matumizi mabaya ya madaraka na madhambi mengine katika jamii. Taifa letu chini ya serikali ya awamu ya tano, limetangaza vita kali dhidi ya ufisadi, rushwa na wizi wa rasilimali za taifa. Ili kushinda vita hii, serikali inahitaji msaada wa makomandoo wazoefu katika vita ya namna hii. Makomandoo hao ni mitandao ya kijamii (social media), vyombo huru vya habari, asasi za kiraia, taasisi zisizo za kiserikali, vyama vya wafanyakazi, wanaharakati, vyama vya upinzani, Bunge huru na Katiba nzuri. Kuwapunguzia uhuru makomandoo hawa au kugombana nao badala ya kugombana na ufisadi, ni kutangaza kushindwa kabla ya mapambano kuanza.
Hitimisho
Nihitimishe mada hii kwa kuweka misisitizo miwili. Kwanza, “Change Tanzania” kwangu mimi ni mkakati wa kukubali kuwa kuna kitu hakipo sawa. Kitu hicho kinatokana na uwepo wa ujinga katika viwango mbalimbali. Ili kuuondoa ujinga huo ni sharti tuujue. Ili tuujue, ni lazima tukubali waongee ili tuujue ujinga wao. Tukiujua ndipo tunautibu. Mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu ya tiba hiyo.
Pili, maendeleo si bidhaa inayoletwa katika makontena. Uhuru si zawadi inayotolewa kwa gharama ya utii na unyenyekevu. Ni tunu inayotolewa na muumba. Katiba, serikali na mihimili yake ni watekelezaji wa agizo la Muumba katika kutii matakwa yake ili viumbe wake wawe huru daima.
Mada ya Askofu Benson Bagonza ilitolewa Usa-River Arusha katika Kongamano la “Change Tanzania Forum” Mei 24, 2019. Mwandishi anapatikana kwa namba 0754 742 423.