Mshirika mmoja wa mkutano wa uzinduzi wa kitabu kiitwacho Insha Tatu za Kifalsafa za Mwalimu Nyerere amerusha kombora zito dhidi ya wasomi na mijadala yao ya kisomi.

Mama Anna Mwansasu alihoji desturi ya wasomi kuandaa mikutano kujadili masuala mbalimbali muhimu yanayogusa maisha ya mwananchi wa kawaida, lakini badala ya kuwaelimisha wakazi wa vijijini juu ya umuhimu wa masuala hayo, wasomi hubaki mijini na kuweka mijadala baina yao.

Mkutano huo uliandaliwa hivi karibuni na Kavazi la Mwalimu Nyerere, taasisi inayokusanya kumbukumbu za Mwalimu Nyerere na mada ya mjadala uliofuata ilihusu umuhimu wa viongozi wetu kuheshimu na kulinda katiba na sheria katika kutekeleza kazi zao.

Mama Mwansasu namuunga mkono. Labda kwa kuwa mimi pia naishi kijijini na ni mmoja wa wanakijiji wa Kijiji cha Butiama niliyeshuhudia kuwa ninapowaona wasomi kijijini Butiama, ni pale wanapokuja kufanya utafiti juu ya Mwalimu Nyerere au suala ambalo taarifa zake zipo kijijini.

Tatizo ni kuwa wakikamilisha utafiti wao, huchukua uamuzi wa kuzindua taarifa na vitabu mijini, na hasa Dar es Salaam. Alifanya hivyo Dk. Thomas Molony aliyetafiti maisha ya Mwalimu Nyerere na kuchapisha na kuzindua jijini Dar es Salaam kitabu kiitwacho Nyerere: The Early Years, [Nyerere: Miaka ya Awali] na wamefanya hivyo wanazuoni wa Kavazi la Mwalimu Nyerere katika uzinduzi wa Ijumaa iliyopita.

Lakini tukitaka kusema ukweli, sababu za msingi zipo za kwanini wanakijiji wataendelea kujadili masuala yao ya kijijini wakati wakazi wa mjini wataendelea kupata fursa nyingi zaidi za kujadili masuala yanayohusu itikadi na falsafa za Mwalimu Nyerere na mada za aina hiyo. Mimi nazipa jina la mada za kisomi.

Napenda kurudia mfano mmoja, na wasomaji mtaniwia radhi kama naurudia tena, lakini unadhihirisha kwa nini mijadala mingine ni vigumu kuihamishia vijijini.

Wakati wa mjadala wa uundwaji wa katiba mpya, nilimuuliza mama anayeishi Butiama mwenye elimu ya shule ya msingi kama anafahamu maana ya katiba. Kwanza, kutamka tu neno katiba kwa usahihi ilimchukua zaidi ya dakika kumi, na jitihada zangu za kutafiti ufahamu wake wa katiba ziliishia hapo hapo. Unaanzaje kujadili katiba mpya kwa mtu ambaye si tu hawezi kutamka “katiba”, bali hafahamu hata katiba ni nini? Ukishafahamu kuwa mtu anapata tabu kutamka katiba, bado utakuwa na nguvu ya kujadili masuala mengine kama demokrasia shirikishi, kikomo cha uongozi wa rais, mgongano wa masilahi, na hoja ya serikali tatu au mbili?

Wanasiasa na wanaharakati wanapenda sana kusema kuwa Watanzania wanao ufahamu mkubwa wa umuhimu wa masuala mbalimbali yanayogusa maisha yao, lakini mimi naamini kuwa ukweli uko tofauti kidogo. Asiyefahamu kitu huwa haongei, kwa hiyo tusiharakishe kusema kuwa wale tunaowasikia wakipaza sauti kijijini wanaakisi uelewa wa wote. Yule aliyeshindwa kutamka “katiba” hawezi kupata ujasiri wa kusimamia mbele ya mkutano wa hadhara na angalau kuuliza tu maana ya katiba.

Kwa sababu hizi, naamini kuwa kuna kundi kubwa la watu ambalo, ama halifuatilii sana masuala muhimu yanayohusu taifa hili, au halina uwezo wa kielimu wa kuweza kuchangia mawazo yao kwenye mijadala muhimu inayohusu ustawi wa maisha yao.

Lakini Mama Mwansasu ametoa hoja muhimu sana. Wasomi wakiendelea kukaa kwenye mikutano yao ya mjini yenye viyoyozi badala ya kuhamishia mijadala vijijini na kukaa chini na wananchi wa kawaida chini ya miembe na mizambarao, watabaki wanaishi kwenye ulimwengu wao wa kisomi ambao hauwaunganishi na wale ambao hawakupata fursa ya kusoma.

Elimu inapaswa kutumika kuboresha maisha ya wote, pamoja na wale ambao hawakupata fursa ya elimu nzuri.

 Lakini hili siyo tatizo la kuachiwa wasomi peke yao walitatue. Ufahamu na uelewa wa haki za raia, na wajibu wake na wa viongozi kwa jamii, unapaswa kuwa elimu isiyokuwa na kikomo. Hadi leo tunasikia, ingawa ni kwenye redio ya Taifa pekee, tangazo la Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuhusu umuhimu wa kutumia chandarua kila tunapoingia kitandani kulala. Tangazo hilo limeanza akiwa madarakani, na linaendelea wakati huu akiwa mstaafu na tumeanza kumuita Mzee Kikwete.

Majadiliano ya katiba yangekuwa pia yanaendelezwa kwa utaratibu huo huo. Elimu ya katiba si suala ambalo linapaswa kuwekewa mipaka ya muda, kama ilivyokuwa wakati wa kujadili rasimu ya Katiba Mpya. Ni wajibu wa serikali na asasi za kiraia kuendelea kutoa elimu ya katiba na sheria zilizopo wakati wote ili raia waendelee kuelimika siyo juu ya haki tu, bali pamoja na wajibu wao.

Siyo serikali zote ambazo zinaamini kuwa raia anapaswa kufahamu vyema haki zake ndani ya katiba na sheria zilizopo, lakini naamini kuwa kama ilivyo muhimu kwa watoto kusomeshwa kwa gharama za serikali, basi upo umuhimu ule ule – tena labda mkubwa zaidi – kwa serikali kugharimia pia elimu ya uraia kwa wananchi wake wakati wote.

Raia waliokuwa na elimu hiyo watawavutia wasomi kuhamishia mijadala yao vijijini kwa sababu watakuwa na hadhira ambayo imepewa msingi mzuri wa kushiriki kwenye mijadala ambayo sasa hivi huishia mijini zaidi. Haya yakitokea hutawasikia kina Mama Mwansasu wakilalamika tena.