url-1“Tekelezeni wajibu wenu bila ya woga. ( Makofi ) Katekelezeni wajibu wenu bila ya woga kwa kuzingatia sheria. ………Niwaombeni sana, vyeo vyetu tuviweke pembeni na sheria tusiweke pembeni. …….Mimi Rais wenu nipo pamoja na nyinyi.”

Ni tamshi lenye upendo na msisitizo  wa kufanyakazi kwa Manaibu Makamanda na Makamishina Wasaidizi Waandamizi wa Polisi, wakati wa kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Binafsi natoa pongezi kwa Makamanda na Makamishina wote waliopanda vyeo. Pamoja na hayo nina machache ya kuzungumza kuhusu hotuba ya Rais John Pombe Magufuli aliyeitoa kwa polisi hao wakati wa kula kiapo, ambayo imebeba maneno Tekeleza, Wajibu, Woga, Sheria na Umoja.

Naamini kila mtu hapa nchini anatambua umuhimu wa Jeshi la Polisi katika kuweka usalama wa raia na mali zao. Unapokosekana usalama iwe ndani ya familia au hata kwenye jamii hakuna shughuli za kazi, au sherehe au maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Polisi ni chombo maalum kinachoshughulikia ulinzi na usimamizi wa sheria za nchi pamoja na usalama.  Maana ya askari polisi ni watu wanaoendesha chombo hicho. Watu hao wasipofanya kazi zao ipasavyo ni sawa tu kuwa na dude nchini.

Wananchi hatuhitaji kuwa na dude. Tunahitaji sana jeshi la polisi ambalo askari wake wanatekeleza majukumu  waliyoyataka, waliyopewa na waliyoyakubali ya kuweka jamii ya watanzania katika hali ya usalama, amani na utulivu. Kinyume chake ni kuwa na dude tu !

Utekelezaji wa jambo lolote huwa na thamani mtu au watu wanapotambua wajibu wao. Polisi hao wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kutudhihirishia wamekubali na wanatambua majukumu yao mbele ya jamii hii inayohitaji amani, utulivu na haki sawa kwa wote.

Daima utekelezaji wa wajibu huambatana na sheria. Ni katika kanuni zinazoendesha taratibu za maisha zilizokubaliwa na jamii husika. Polisi wetu chini ya uongozi wa Makamanda na Makamishina wazitumie sheria kihalali kurejesha heshima yao mbele ya wananchi.

Iwapo sheria hazitasimamiwa itakuwa ni vigumu kuwa na ushirikiano baina ya viongozi hao na wanaowaongoza katika madaraka bila ya kuwapa mamlaka ya kutimiza wajibu. Ndipo dude hupata fursa ya kulea uonevu, uhasama, chuki n.k.

Woga ni adui wa maendeleo. Ni hofu inayojengwa ndani ya moyo kuhofia kufikwa na taabu au jambo la msukosuko. Kwa mtaji huu kiapo walichokula hakitaweza kuleta tija katika Jeshi la Polisi kwa sababu dhana “ Sheria ni msumeno “ haikupata kinge chake.

Wananchi wana matumaini makubwa kuona Jeshi la Polisi linarudisha na kutunza heshima yake. Polisi msikubali kuwa kama wanasesere kila mtu au kiongozi  ana hamu ya kuwachezea kwa zake jeuri au matakwa yake.

Ni kweli Jeshi la Polisi ni chombo cha mabavu. Lakini mabavu hayo kutumika kwa nani ?  Kwa kila mtu au kwa kila mtu mnyonge ? Hapana. Mabavu yatumike kwa mtu fedhuli, anayejitapa mbele ya jamii au dola kuwa yeye ni mbabe.

Nawaomba wananchi wenzangu tuwape Polisi ushirikiano  na kutoa taarifa sahihi zenye dalili au kusudio la kuvunja usalama wetu. Polisi mzingatie sheria, kanuni na kiapo mlichokula, kuwalinda na kuwahifadhi watoa taarifa. Usalama wao na mali zao ziko mikononi mwenu.

Madhali serikali imekiri hadharani kuboresha hali ya maisha na makazi yenu kuwa bora zaidi, raha iliyoje kwenu kuwajibika mchana na usiku kudumisha usalama. Kumbukeni Rais Magufuli alipowanasihi, “ Mimi Rais wenu nipo pamoja na nyinyi. “

Niwatakie kila la kheri katika utekelezaji wa kazi zenu na hasa katika kipindi hichi cha mpito cha kurejesha utu na heshima yenu na ya Wananchi; pamoja na uboreshaji wa uchumi wa nchi kuwa imara.

“ Mungu ibariki Jeshi la Polisi, Mungu ibariki Tanzania “