Baada ya Japan kuibuka kwa kasi kimaendeleo, iliitamanisha sana Marekani kiasi cha kuwafanya wanauchumi wengi wa Marekani kuwa na kiu ya taifa lao kuiga mfumo wa kiuchumi wa Japan.
Bila ajizi wakataka kudurufu mfumo ulioiinua Japan ujulikanao kama ‘Japanese Business and Management System’ au ‘JABMS’ kama unavyofahamika katika anga za uchumi wa kimataifa. Kutokana na ugumu wa mfumo huo ukilinganishwa na mazingira ya Marekani, iliwawia vigumu Wamarekani kuuiga.
Baada ya kutolewa jasho wakijaribu kuigiza mbinu za Japan kukua kiviwanda, walinyoosha mikono na kutangaza wazi kuwa kinachofanyika huko Japan ni kama ahadi hewa za kimiujiza. Inafahamika kuwa Japan, kwa miaka mingi, imeendelea kupata sifa kwa kuwa taifa kubwa na lililoendelea kiviwanda.
Kutokana na maendeleo ya kiviwanda, hasa katika eneo la teknolojia ya kielektroniki, Japan imekuwa ikihesabiwa na kuonekana kama taifa linalowajali watu wake, lililostawi kidemokrasia na linalolinda maslahi ya ulimwengu mzima.
Pamoja na Japan kuonekana kuwa ni ya kidemokrasia, mfumo wake wa kisiasa unatajwa kuwa ni wa kibwanyenye (semi-feudal). Katika mfumo huu kunaonekana makundi machache ya wenye nacho wanaowatawala wengine kiuchumi. Baadhi ya wataalamu akiwamo, Profesa Prakash Sethi, wanasema kuwa pamoja na maendeleo hayo makubwa, Japan haijaweza kuleta mageuzi katika fikra za watu.
Utafiti ulioendeshwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 ulionesha kuwa Wajapani wengi hawahisi kuwa serikali ni mali yao. Ingawa katiba yao ya mwaka 1947 inaonesha kutoa ramani kwa serikali inayozingatia demokrasia na utawala wa kisheria, bado kuna tatizo kubwa la ukiritimba.
Ukiritimba huu umesababisha umma kutohusishwa moja kwa moja na kikamilifu katika ushiriki wa siasa za nchi hiyo. Kwa maana hii wananchi wengi wanaona kuwa katiba iliyopo haitofautiani na ile iliyotengenezwa wakati wa utawala wa kiongozi mkorofi, Meiji mwaka 1889.
Navyo vyama vya siasa nchini Japan vinashutumiwa kuwa havina muda na usimamiaji wa programu na sera, badala yake vimejikita katika utafutaji, ukusanyaji na ulindaji wa maslahi kwa ajili ya makundi madogo ila yenye nguvu ndani ya vyama hivyo.
Kwa mfano, chama cha the Liberal Democratic Party (LDP) kinaelezwa kuwa ni muungano usio imara wa makundi-maslahi (factions) zaidi ya nusu dazani. Makundi haya kikawaida huwa na nguvu na uwezo wa kumuinua ama kumwangusha yeyote katika siasa za Japan.
Hili linaweza kuthibitishwa na kilichowahi kumpata mmoja wa mawaziri wakuu, Tanaka. Waziri huyu aliwahi kukumbwa na kashfa ya rushwa iliyobatizwa jina la Lockheed. Pamoja na kufikishwa mahakamani aliweza kuhimili na kubakia na nguvu yake kwa sababu alikuwa anaongoza sehemu kubwa ya makundi-maslahi ndani ya LDP.
Siasa za Japan zimeunganishwa na biashara kubwa zenye uhusiano wa moja kwa moja na viongozi wa vyama vya siasa. Uhusiano huu unaratibiwa na klabu zijulikanazo kama Itsukakai ama ‘Fifth-Day-of-the Month’ kama wakurugenzi wa kampuni wanavyoziita. Vikao hivi hufanyikia katika migahawa na hoteli za gharama kubwa, na kiutamaduni hutumiwa na wanasiasa wa juu kuimarisha uhusiano na wamiliki pamoja na wakurugenzi wa kampuni ya nchini humo.
Wanasiasa wengi katika taifa hili hawana namna ya kuzikwepa ‘Itsukakai’ kwa sababu kuna wakati kampuni huweza kuamua ni nani awe waziri mkuu ama kiongozi katika ngazi nyinginezo. Kampuni ikipitisha kuunga mkono mgombea fulani, basi wafanyakazi nao hushawishiwa kumpigia kura mgombea huyo.
Licha ya kwamba katiba yao inafafanua na imetoa nguvu ya utungaji sera na uibuaji wa mipango ya kimaendeleo kwa mabaraza maalumu, yasiyokuwa na ubavu wa kuamua ama kupitisha jambo lolote, pasipo kupata baraka kutoka kwa ‘miungu watu’ (inayojumuisha wakongwe wa siasa za Japan, matajiri na makundi-maslahi) wajulikanao kama ‘Diet’.
Lipo kundi jingine lijulikanalo kama ‘Zaikai’ linalojumuisha viongozi matajiri kutoka katika taasisi mbalimbali wenye ushawishi wa ajabu katika siasa za Japan. Ndani ya ‘Zaikai’ kuna wakuu wa taasisi nne na moja yenye nguvu kubwa ni ile ya Keidanren ama ‘Federation Economic Organisation’. Bodi ya wakurugenzi ya ‘Zaikai’ imejazwa na marais wa taasisi nyeti, viongozi wa kitaifa wa biashara, viwanda na wale wanaohusika na masuala ya kifedha.
Ndani ya ‘Zaikai’ nako kuna makundi mengine madogo madogo kutokana na maslahi yanayojikita katika matakwa maalumu, matakwa ya kidini, mitazamo kuhusu siasa na mwenendo wa nchi za Magharibi, uungwaji mkono wa kisiasa na kubwa kuliko yote ni umuhimu wa ukaribu kati ya matajiri hawa na upatikanaji wa viti na mamlaka ya kisiasa.
‘Zaikai’ wana nguvu zaidi ya Itsukakai, wakipinga ama kuunga mkono kitu/jambo hakuna mwenye jeuri ya kufanya kinyume nao, si serikali, bunge wala umma. Kitu cha kufurahisha ni kuwa ushawishi wa makundi haya unafanyika katika masuala mbalimbali bila kificho!
Mbali na ‘Zaikai’, kuna kundi jingine kubwa la kiuchumi lijulikanalo kama ‘Zaibatsu’ au ‘Keiretsu’, linalojumuisha kampuni zile tu zilizohodhi biashara katika maeneo mbalimbali.
Unapotaja Zaibatsu unakutana na madaraja mawili – moja likihusisha lundo la kampuni kama Mitsui, Mitsubishi na Sumitomo. Mitsui na Mitsubishi katika kuungana na kujifilisi (liquidation) yameshazalisha kampuni nyingine zinazofikia 200! Daraja jingine ni mkusanyiko wa benki kubwa zikiwamo Fuji, Daiichi na Sanwa.
Siasa za namna hii nchini Japan zilikuwa dhahiri kutoka miaka ya 1980, licha ya kuwapo mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayotokea kila siku nchini humo, lakini utaona kuwa suala la wenye nacho kutawala siasa na mustakabali wa taifa hilo bado limeota mizizi.
Pamoja na kuwa LDP iling’olewa madarakani miaka ya hivi karibuni baada ya kushika hatamu kwa miaka takribani hamsini, ukweli ni kuwa makundi ya wenye nacho yangali yanacheza na upepo wa kisiasa nchini humo ili kulinda maslahi yake.
Suala la watu wachache matajiri kutikisa siasa za nchi halipo katika taifa la Japan pekee, isipokuwa ni takribani katika mataifa yote duniani, hasa yale yanayoegemea mfumo wa uchumi wa kibepari. Mahali pote wenye nacho ndiyo wanaokuwa na sauti ya kuamua nani awe Rais, nani awe waziri mkuu ama kiongozi wa jimbo kwa maslahi ya wenye nacho.
Ukitafakari harakaharaka unaweza kuyachukia makundi ya wenye nacho, (wafanyabiashara wakubwa, watu maarufu, na wenye ushawishi katika siasa) lakini kuna kitu cha kuangalia na kukichukulia kwa umakini mkubwa. Ukweli ni kuwa asilimia hii ndogo ya wenye nacho, ndiyo wanaoshikilia sehemu kubwa ya uchumi wa nchi.
Maana yake ni kwamba hawa wakikasirika wanao uwezo wa kuyumbisha kabisa uchumi wa nchi na wakifurahi wanaweza kuboresha uchumi wa nchi. Ingawa hili linauma sana (hasa kwa wanaharakati wa usawa wa kiuchumi kwa jamii), lakini ukweli unabaki pale pale kuwa hawa wenye nacho wanayo nguvu ya kuamua mustakabali wa uchumi wa nchi kuliko hata wanasiasa tunaowachagua kwa kura!
Kwa kulijua hili kwa kujifunza ya Japan na hali ya Tanzania yetu; ikizingatiwa kuwa asilimia mbili tu ya Watanzania ndiyo wanaomiliki asilimia karibu 90 ya uchumi wetu; kunakuwa na ama wito au sheria madhubuti au ‘maombi kwa Mungu’, kwamba hawa wafanyabiashara (au niseme wenye nacho); wawe na maadili ya kijamii na kibiashara. Kinyume cha hapo, tumekwisha!
Wasilipeleke taifa wanakotaka, wasiingize nchi katika biashara ama mikataba kichaa na tena wasiuhujumu uchumi wa taifa letu kwa makusudi. Hakuna nguvu (nasema tena narudia, hakuna) ya kuyazuia makundi ya wenye nacho duniani pote kuhujumu ama kuendeleza uchumi wa mataifa husika zaidi ya dhamira zao wenyewe!
Sifahamu ‘Zaikai, Itsukakai, Zaibatsu’ ya Tanzania yanaitwaje, lakini yapo. Kimsingi kuwapo kwake (tena kama yapo kwa kificho bora yawepo hadharani) hautakuwa na athari za kutisha kwa mustakabali wa taifa letu, ikiwa ‘yatawahurumia’ wanasiasa na kuwaacha wawe huru kututumikia wananchi huku maslahi ya taifa letu yakilindwa kwa wao kuwa na maadili ya kibiashara na kijamii (social-business ethics).
[email protected]; 0719 127 901