Leo ninapenda tuperuzi nafasi ya uelewa wetu sisi wajasiriamali na Watanzania kwa jumla, linapokuja suala la uchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Unapotaja Afrika Mashariki ni kwamba kuna mambo ya msingi yanayoushikilia uhusiano huu.

Pamoja na mambo mengine, nguzo kuu ya uwepo wa Jumuiya hii ni suala la uchumi. Ndiyo maana tunaongelea soko la pamoja, kuunganisha sarafu zetu, kusafiri kwa mitaji na rasilimali watu.

 

Mambo mengine yanayojadiliwa na kushughulikiwa katika ushirikiano huu yanasaidia tu kuboresha lengo kuu la msingi; ambalo ni kuboresha uchumi wa ukanda huu. Kwa tafsiri ya mkato ni kwamba lugha ya Afrika Mashariki ni uchumi.

Ili kunufaika na Jumuiya hii lazima kuijua lugha hii, lazima kuyajua matendo ya kiuchumi, lazima kuelewa mwenendo wa kiuchumi na lazima kutambua nafasi ya mtu mmoja mmoja katika uchumi.

Wakinga wana msemo usemao, “Kama wewe sio mchawi, hakikisha unamfahamu mganga mzuri”. Si lazima uwe mjuzi ama mtaalamu wa mambo ya uchumi na lugha za uchumi wa darasani ili kuijua lugha ya Afrika Mashariki; bali unaweza kujifunza na kujizoesha kutoka kwa ‘waganga’ (wataalamu) na baadaye nawe ukawa ‘mchawi’ (mtumiaji).

Je, Watanzania tunaijua kwa kiasi gani lugha inayotumika Afrika Mashariki? Je, tunaelewa maana na matendo ya kufanya tunaposikia viashiria vya masoko ya hisa, masoko ya mitaji, sarafu ya pamoja, ushirikiano wa kodi na ushuru, au tunapoambiwa mtiririko wa rasilimali watu?

Kwa bahati mbaya ni kuwa kutojua lugha hizi hakutoi msamaha wa kuhurumiwa linapokuja suala la utekaji wa fursa zilizopo kwenye Jumuiya hii.

Hebu tuangalie mifano michache ya lugha ya Afrika Mashariki: Unaposikia masoko ya mitaji na hisa kichwani kwako, lazima kuje maneno kama DSE (Dar es Salaam Stock Exchange), USE (Uganda Stock Exchange) na NSE (Nairobi Securities Exchange). Haya ni masoko ya ununuzi wa hisa na ubadilishanaji wa mitaji pale.

Hapo kuna kampuni zinazopeleka sehemu yake kuwa miliki ya umma, hivyo unaweza kununua ama kuuza sehemu za kampuni hizo. Kujua kuhusu DSE, NSE, na USE hakuhitaji mpaka uwe unamiliki hisa ama mtaji pale isipokuwa mwenendo wake unaathiri sana uchumi wa eneo hili, hivyo kuathiri ustawi wako binafsi kiuchumi.

Nikisema habari za hisa na mitaji, mtu anaweza kudhani ninaongelea masuala ya kitaalamu sana. Kumbuka ninaongelea lugha ya Afrika Mashariki. Namna kampuni zinavyojiandikisha na kuuza mitaji kwenye masoko ya hisa na mitaji,s kunaonesha mtiririko na mwelekeo wa mitaji katika ukanda mzima.

Nasi tunajua kuwa ulipo mzoga ndipo wakutanikapo tai. Tai wanajuaje kuwa sehemu fulani kuna mzoga? Jibu ni rahisi, wanatumia harufu kutambua. Je, unajuaje kuwa Uganda ama Rwanda kuna fursa za kuwekeza?

Ni kwa kuangalia mwenendo wa mitaji na hisa kama moja ya viashiria kati ya vingi vilivyopo. Ubaya ni kwamba hata kama wewe usipoijua harufu ya “mzoga wa uwekezaji” wenzako kutoka nchi nyingine za Jumuiya wataijua harufu iliyopo hapa Tanzania nao watakusanyika.

Ninapozungumzia habari za DSE, USE na NSE naelewa kuwa si rahisi sana kwa wengi kuelewa fursa zilizopo ndani yake, pengine kutokana na historia ya uchumi na mazoea yetu. Wenzetu Kenya NSE ilianza (japo siyo rasmi) mwaka 1954 wakati sisi DSE ilianza mwaka 1996.

Wenzetu wana uzoefu mkubwa na lugha hii wameizoea kwa kiasi kikubwa. Pale NSE kampuni zilizojiandikisha ni zaidi ya 50 wakati hapa kwetu DSE kuna kampuni pungufu ya 20 tena nyingine zikiwa ni zile zile za kule Kenya (Cross listing).

Kwa upande wa Uganda hawana tofauti na sisi kwa maana ya kuanza, kwani USE ilianza 1997, lakini kasi yao ya kuijua lugha hii ni kubwa. Mwaka 2010 USE ilikuwa ni kinara wa masoko yote ya hisa kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutumia kipimo cha ALSI (All Shares Index) ikiwa na mrejesho wa faida ya asilimia 74 kwa hisa zinazonunuliwa na kuuzwa.

Sina lengo la kukupitisha porini katika takwimu za kitaalamu, lakini kuna kitu nataka tujifunze; Kenya walitangulia miaka mingi, Uganda ni wapya kama sisi, lakini wanajifunza kwa kasi ya jabu. Wenzetu walishatangulia na wengine wanakimbia, lakini sisi tunazinduka polepole mno!

Nikiri wazi kuwa mambo kama haya ya hisa na mitaji kiasili yaliibuka kutokana na ubepari, lakini kwa kuwa tumeamua “kuchanganyika” hatuna ujanja zaidi ya kuungana nao. Kumbuka “Kama wewe sio mchawi hakikisha unawajua waganga wazuri”, hatuna ujanja, inatakiwa tujifunze na kuizoelea lugha hii tuweze kuelewana na wenzetu wa hapa ‘jumuiyani’.

Katika robo ya mwaka jana kampuni nyingi za umma na binafsi katika nchi zote tano za Afrika Mashariki zimeendelea kutoa ripoti zao za kifedha na kiutendaji kwa mwaka ulioishia Desemba 2012. Hapa napo tunaweza kuitathmini hali yetu tuliyonayo katika lugha ya Afrika Mashariki kwa kuangalia namna tunavyozipokea ripoti hizo.

Nianze na namna jirani zetu Kenya wanavyozipokea ripoti hizo. Wakati kampuni 20 kubwa (zilizopo kwenye 20 Shares Index) zikiachia ripoti zao nchini Kenya; kulikuwa na  gumzo mitaani kila mmoja akihaha kuzifuatilia, kuzisoma na kuzitafsiri. Wanahisa na wasio wanahisa wanataka kujua kampuni gani imefanya vipi, ipi imeizidi ipi, ipi ina fursa na gawio zuri kwa kuwekeza, ipi ina mikakati gani ya muda ujao na mengine mengi.

Gazeti moja la nchini Kenya lilipiga picha inayoonesha watoto wa shule ya sekondari katika mji wa Naivasha wakisoma ripoti ya mojawapo ya benki za biashara nchini Kenya. Watoto hao walipoulizwa mmoja wao alijibu, “Mama ana hisa kwenye benki hii nataka nijue mwenendo wake”. Hapo ni Kenya! Hadi watoto wa shule za sekondari wanaongea lugha ya Afrika Mashariki!

Hali ni tete kwa Tanzania kwa sababu ripoti za kampuni za ndani ama za wawekezaji huwa hazipokewi kwa hamasa yoyote. Kwanza ni wachache wanaofuatilia ripoti hizo, achilia mbali uwezo wa kutafsiri maana na athari za ripoti hizo kwa Afrika Mashariki na watu wake.

Kule Rwanda na Burundi wenzetu ndiyo kwanza wanajenga upya nchi zao; hivyo si rahisi sana kutoa hitimisho la moja kwa moja kuhusu hisia zao katika lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi, lakini kiu yao ya kuinuka kiuchumi na kijamii inaonesha namna wanavyoweza kutupita.

Unaposoma ripoti za kampuni hizi (Financial Statements) kuna ishara zinatoa ikiwamo, “Nenda katafute ajira sehemu fulani”, “Nenda kawekeze kitu fulani mahali fulani”, “Ondoka mahali fulani kwa sababu pameharibika”, na kadhalika. Kwa kutozijua lugha hizi tunabaki tumeduwaa tusijue cha kufanya wala kwa kuelekea. Kwa kuwa wenzetu wanaelewa lugha na matendo ya Kiafrika Mashariki ni rahisi na itaendelea kuwawia rahisi kunufaika na lugha hii.

Tatizo letu Watanzania wengi tunatumia malalamishi kama silaha ya kujiokoa na hatari za Afrika Mashariki. Juhudi zetu katika kuteka fursa za Jumuiya hii zimeota matege na tumekuwa na mtazamo mdogo mno kuhusu mambo tunayotakiwa kufanya.

Kwa mfano; kitendo cha kukazana kujifunza Kiingereza ama kukazana kununua ardhi kwa ajili ya fursa za Afrika Mashariki si kibaya, lakini ni mtazamo mdogo sana. Tukiijua lugha ya Afrika Mashariki kiuchumi; tutaona na kuoneshwa mambo mengi sana yatupasayo ndani ya Jumuiya hii.

Wajasiriamali tuliopo Afrika Mashariki tusipokazana kujifunza lugha ya Afrika Mashariki tutajikuta tunaishia kulalamika na kuhisi tunaonewa. Hatuna sababu ya kunung’unika ama kusubiri upepo wa mabadiliko utugaragaze.

Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi Afrika Mashariki!

 

[email protected]

0719 127 901