Siku kadhaa zilizopita nilikuwa miongoni mwa wale tuliotoa wito kwa wapendwa ndugu zetu Waislamu, kuwapuuza kina Sheikh Ponda na mwenzake Kundecha – ambao kila mara wamekuwa vinara wa migogoro na kuibua mambo yasiyo na tija kwa Waislamu na Watanzania.
Tulikuwa na msimamo huo baada ya kuona wanaibua chokochoko za kuikwamisha Sensa ya Watu na Makazi nchini itakayofanyika mwezi ujao. Hoja yao ni kwamba kipengele cha dini lazima kiwemo kwenye dodoso. Watu wazima, katika dunia ya leo, kung’ang’ana kujua idadi ya watu kwa madhehebu yao ni kufilisika.
Wakati wenzetu wanang’ang’ana kuwa na maisha bora, sisi tumebaki na mambo ambayo hata Mungu hawezi kutusamehe kwa kupoteza muda mrefu kuyajadili.
Nashukuru kwamba kiongozi wa kwanza kuitikia maoni yetu alikuwa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba. Mara baada ya kutoa wito kwa Waislamu kushiriki sensa, walijitokeza wachochezi wengine kumpinga. Inakuwa vigumu sana kuamini kuwa kuna waumini wanaweza kumpinga kwa kejeli kiongozi wao mkuu.
Bahati nzuri, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania imeunga mkono kauli iliyotolewa Mufti Simba ya kuwataka Waislamu na Watanzania kote nchini, kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 26, mwaka huu.
Kwa niaba ya mwenyekiti wa jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania , Sheikh Hamis Mattaka, akasema hatua hiyo inatokana na kuwapo kwa baadhi ya makundi yanayowahamasisha waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi kutoshiriki sensa.
Akasema wao kama jopo la wanazuoni hawaoni tatizo la sensa kutokana na umuhimu wake kwa taifa. Akasema kuwa Sensa ya Watu na Makazi ipo kwa mujibu wa sheria za nchi na imepitishwa na Bunge.
“Tunajua kuwa serikali ilikuwa na nia njema kukiondoa kipengele cha dini katika sensa, hapana budi nia njema hiyo ya serikali ilindwe kwa kuweka sheria itakayozuia kutoa takwimu zinazohusu dini za Watanzania,” amesema Sheikh Mattaka.
Amefafanua kuwa Sensa ya awali ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilihusishwa, na baadaye kuondolewa katika sensa zilizofuata kwenye madodoso ya kukusanyia takwimu za kaya.
“Sisi kama jopo kila siku tunasema ili twende salama kama wananchi wa nchi hii, ni wajibu wetu kuheshimu na kufuata sheria kwa maana ya kutii sheria bila shuruti, kwa hiyo tunasema Sensa ya Watu na Makazi ni jambo la kisheria si jambo la mitaani, hatuwezi kulumbana na kujadili jambo ambalo liko wazi kisheria na limepitishwa na wabunge tuliowachagua sisi wenyewe,” amesema.
Akasema sensa itaiwezesha serikali kupanga maendeleo kwa kuwa na takwimu sahihi za watu na makazi, hali ya kipato cha kaya, vizazi na vifo na pia kuiwezesha serikali kuwapatia huduma bora wananchi wake. Pia jopo la masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania limewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya Katiba.
“Tunawataka Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla kuitumia fursa hii muhimu kwa kutoa maoni yao, ili hatimaye nchi yetu ipate Katiba itakayokidhi matakwa ya wananchi kwa miaka mingi ijayo,” amesema Sheikh Mataka kwa niaba ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Nimeyarejea maneno ya wanazuoni hawa ili kuonyesha kuwa si Waislamu wote nchini wanaopenda vurugu. Kama nilivyosema katika makala yangu iliyotangulia, usalama na amani katika taifa ketu ni dhima ya kila mmoja wetu. Amani haiwezi kudumishwa na Waislamu, Wakristo au wapagani pekee. Ni jambo linalohitaji nguvu na mshikamano wa pamoja bila kujali tofauti zetu.
Kujitokeza kwa viongozi hawa kuweka bayana msimamo wao, si tu kwamba wamesaidia kuondoa hofu na upotoshaji miongoni mwa Waislamu, lakini ni ukweli kwamba wametekeleza wajibu wao wa msingi wa kuhakikisha chokochoko zisizo za msingi zinavunjwa kwa nguvu ya hoja.
Kama wengi wetu, wakiwamo Waislamu walivyopata kusema, kipengele cha dini kwenye dodoso hakina maana wala ulazima kushinda maana ya kweli ya kujua idadi ya Watanzania, na namna ya kuweka mipango ya maendeleo kwa uwiano. Kama kweli Waislamu wanataka kujua wapo wangapi, ni jambo la kutoa maagizo katika misikiti yote nchini ili iweze kutoa orodha ya waumini wake.
Kama kuna Wakristo wanaona kujua idadi yao ni jambo la maana sana, wanachopaswa kukifanya ni kufanya sensa kwenye makanisa yao yaliyoenea nchi nzima. Kuhusisha suala la idadi ya waumini katika jambo la kitaifa kama hili hakuna maana yoyote.
Aidha, wapo wanaotaka tuhesabiwe hadi makabila yetu. Nimepata kumwuliza rafiki yangu kwamba kwa hali ya sasa ya kuwapo yatima wengi wanaotupwa na wazazi wao, tutatambuaje makabila ya hao yatima?
Kwenda kulala katika nyumba ya wageni na kutakiwa kujaza dodoso la kabila langu kunaisadia nini nchi hii? Tanzania ambayo watu wameoleana kuanzia kwenye makabila hadi dini, kweli leo unaweza kumtambua mtu kwa kabila lake?
Polisi kumtaka mtuhumiwa ataje kabila lake kunasaidia nini? Ninachojaribu kukisema hapa ni kwamba kama tumekataa dodoso la dini na kabila kwenye sensa, vivyo hivyo sasa tujielekeze kwenye madodoso ya polisi na nyumba za kulala wageni. Hakuna sababu ya mtu kutaja kabila lake katika kitabu cha nyumba ya kulala wageni. Sana sana kitu cha maana ni kueleza utaifa, mahali alipotoka na kadhalika.
Leo hii huwezi kumpata mhalifu kwa kutumia kabila lake kwa sababu karibu kila Mtanzania anazungumza Kiswahili. Ofisini kuna watu wengi tunafanya nao kazi kwa miaka mitano hadi 10 lakini hatujui makabila yao. Hakuna mwenye shida ya kumwuliza mwenzake anatoka kabila gani. Watanzania wamekuwa wakijitambulisha kwa maeneo wanayotoka, JKT, shule walizosoma na kadhalika.
Polisi kwa kutumia kipengele cha kabila hawawezi kumpata mtuhumiwa wanayemtafuta. Haya mambo tuliyoyarithi kutoka kwa wakoloni ni lazima tuachane nayo. Hayana faida.
Nirejee tena kuwashukuru sana viongozi wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania kwa weledi wao wa hali ya juu, kuhusu umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya taifa letu.
Walichokifanya wanazuioni hawa kinapaswa kifanywe pia na madhehebu mengine nchini. Watu wenye akili ni lazima wawe wanajitokeza kukemea vikundi na watu wachache wanaojaribu kuvuruga amani na mshikamano katika taifa letu.
Watanzania tunakabiliwa na changamoto nyingi na kubwa kimaendeleo zaidi ya madodoso ya dini na kabila kwenye sensa. Tunaibiwa dhahabu, tunapokwa ardhi, watoto wetu wanasoma katika mazingira magumu mno, mishahara ya watumishi wa umma haitoshi, wakulima wanakopwa, vijana hawana ajira na ongezeko la idadi ya watu halilingani na ukuaji wa uchumi wetu.
Mbali na hyo tuna wezi wanaojilimbikizia mali walizopata kwa njia zisizo halali, tuna changamoto ya kufukuzana na wenzetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki huku tukikabiliwa na mtihani mzito wa kulinda Muungano wetu. Tuna dhima nzito mbele yetu ya kujipatia Katiba mpya itakayokidhi matakwa ya makundi yote katika jamii yetu.
Haya na mengine ndiyo yanayopaswa kuwa mambo ya kutufikirisha kwa sasa na kwa siku zijazo.
Juzi waliokuwa masikini wenzetu – China – waliweza kutuma wanaanga wao kwenda katika anga za juu kabisa. Wamekwenda na kurejea salama duniani. Sisi badala ya kuwaza mambo makubwa ya maana kama haya, tunamaliza pumzi na muda tukijadili dodoso la udini kwenye sensa!
Tukipumzika kujadili hili, tunabeba bakuli kwenda kuhemea misaada ikiwamo ya wafadhili kutujengea vyoo! Shule zinafungwa kwa kukosa vyoo. Kujua idadi ya Waislamu na Wakristo kutaondoa unyonge huu? Aibu tupu!