Kwa karibu miaka miwili sasa nimejiepusha kuandika mada zinazohusiana na masuala ya dini, hasa Uislamu. Niliacha kuandika si kwa sababu nyingine bali kujipa muda niweze kupima upepo, kuangalia mustakabali wa taifa hili na hatimaye kuwa na mawazo muwali yatakayoniwezesha kutoa ushauri wa dhati kwa lengo la kulisaidia taifa letu.
Napata shida kidogo kuandika makala hii, si kwa sababu nyingine, bali Ukristo wangu. Mimi ni Mkristo na wala sioni aibu kutamka hivyo jana, leo na kesho. Nimezaliwa nikakuta familia yangu yote ni Wakatoliki, nimelelewa katika maadili ya Kikatoliki na kufundishwa Katekisi, kisha nikabatizwa, nikakomunika, nikapewa kipaimara (Komunio ya Pili) na hatimaye nikafunga ndoa.
Mungu ananipenda, katika ndoa hii takatifu kati yangu na mpendwa mke wangu Dafrosa tumejaliwa watoto wanne, kati yao akiwa wa kike mmoja na wa kiume watatu. Sitawataja majina watoto hawa lakini kwa furaha ya pekee niseme tu kuwa wote majina yao yanaanza na D. Ni kwa mantiki hiyo wapo wenye kuitania familia yangu wanaiita ‘The D Family’.
Nimejaribu kuyasema haya si kwa sababu nyingine bali kutokana na mwenendo ninaoushuhudia. Naaminia kuwa kwa kuyasema kila anayesoma makala haya atachukulia kuwa sina ajenda iliyojificha au iliyoambatana na hila za aina yoyote, hivyo inanipa fursa kwa wewe msomaji wangu kuyapa uzito unaostahili unayoyasoma na ikiwezekana yatusaidie kuleta tija katika taifa hili.
Binafsi nimezaliwa zaidi ya miaka 40 iliyopita na nimebahatika kuikuta Tanzania ikiwa nchi salama. Katika kijiji nilichozaliwa cha Nyanga, Bukoba Mjini, tuliishi kama ndugu bila kujali dini zetu. Leo kama taifa tunalo tatizo la kiimani. Tanzania kama nchi sasa kuna mwelekeo wa kutothamini AMANI.
Nimekuwa nikisikia (kwa masikio yangu) baadhi ya wanasiasa wakitamka kuwa utulivu na amani umezidi, hivyo yatupaswa tuchapane kwanza kisha tupate akili ya kuiletea maendeleo nchi hii. Wanaosema haya wanatumia mfano mbaya wa mauaji ya Rwanda. Wanasema Wanyarwanda baada ya kuuana wamepata akili na sasa wanapata maendeleo kwa kasi ya ajabu.
Hapa si nia yangu kufungua mjadala mpya katika hili. Nalisema hili kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, kuwa utulivu na amani unaoonekana Rwanda ni bomu linalosubiri wakati. Rais wao, Paul Kagame, anatawala kwa mkono wa chuma na ndiyo maana hadi leo unasikia viongozi wenzake wanalikimbia taifa hilo na kuishi uhamishoni. Mungu apishie mbali, lakini ili Rwanda iweze kudumisha maendeleo haya, inahitaji Kagame wa kudumu. Kagame asiyefariki dunia, wala kuugua mafua.
Ndugu wa wale watu tunaoshuhudia mafuvu yao kwenye makumbusho ya mauaji ya halaiki Rwanda – Mungu anisamehe milele – hawatakaa waridhike na mauaji hayo. Ni lazima wakati wote Rwanda iwe tayari kwamba unyasi tu, unaweza kuchoma nyumba. Kinachotokea Rwanda ni matumizi ya jeshi kuweka nidhamu ya woga wala si utawala wa sheria.
Sitanii, wakati Rwanda walipigana kwa ukabila hapa kwetu nadhani ukabila, umajimbo au umikoa hautakuwa chimbuko la ugomvi wetu. Watanzania tutapigana vita kwa sababu tu ya imani za kidini. Na hapa ndipo ninaposema ndugu zangu Waislamu na Walokole naomba mnielewe. Leo sisi Wakristo Wakatoliki tuna wakati mgumu haijapata kutokea.
Ukiacha makanisa yaliyouacha Ukatoliki miaka ya 1500 kama Anglikana, Lutherani na mengine, leo kuna tishio la makanisa mapya dhidi ya Ukatoliki kuliko wakati wowote duniani. Wapo wanaoitwa Mashahidi wa Yehova, hawa si tu wanawahukumu wakatoliki kuwa si wana wa Mungu (kwa maana wanadai sisi ni wana wa shetani) bali hawataki hata kuimba wimbo wa taifa.
Yapo makanisa ya walokole yenye kukusanya waumini wengi ajabu. Hawa wana upako kama wanavyosema. Waumini wanaogoma kutoa sadaka hata Sh 500 kwenye Kanisa Katoliki wakienda kwenye ulokole wakahubiriwa wanatoa hadi nyumba zao. Wanauza mali za familia na kumtolea Mungu. Hawa wanatoa ushuhuda mbele ya kadamnasi kuwa walikuwa kondoo waliopotea kabla ya kumjua Bwana Yesu.
Nakiri kati ya makanisa haya mapya, yapo yenye viongozi wenye upako wa kweli, ambao wanaombea wagonjwa, wenye mapepo, wahitaji na wengine wakapona au wakapata waombacho. Hawa sipingani nao na nawashukuru kwani lipo kanisa moja ambalo watu karibu wanne ninaowafahamu kuwa walikuwa majambazi wa kutupwa, leo ni waweka hazina wa kanisa hili na wanaendesha harambee, wanasimamia ujenzi wa kanisa bila kuiba hata senti tano.
Ikiwa nguvu ya Mungu inaweza kufanya kazi hii nzuri ya kumuongoa jambazi akawa mtunza sadaka, hili ni jambo jema. Tatizo ninalopata na makanisa haya (yaliyo mengi si yote) ni kuamka kila kukicha kushutumu, kushushua na kutukana Ukatoliki kana kwamba sisi tu waumini wa shetani. Nasema wote tunamtaja Yesu katika mahubiri yetu, tunaomba kwenda mbinguni na sote maombi yetu tunayaelekeza kwa Mungu, hivyo busara inanituma kuwa tuheshimiane.
Sitanii, nimeanza na makanisa kwa nia ya kueleza wazi kero inayonisumbua moyoni. Ningependa kuwa shuhuda wa historia hii, kwamba katika hili Watanzania angalau nimepata fursa ya kuwaasa. Nimetangulia kusema hapo juu kwamba kijijini kwetu katika kijiji chote, familia za Waislamu ilikuwa moja tu; Omary Kongwa.
Baadaye Emmanuel Kaiza alisilimu akaitwa Rashid. Basi katika Kijiji cha Nyanga zikawamo familia mbili. Lipo eneo la Rwaigurwe, ambalo kimtazamo linachukuliwa kuwa ni Nyanga wakati uhalisia ni Kata ya Buhembe, huko nako ilikuwapo familia nyingine moja ya Mwislamu – Mzee Said, baba wa akina Majid.
Tulikuwa tunashirikiana na familia hizi kila kitu. Mimi nilipata kujua kwamba hawa ni Waislamu kwa sababu tu walikuwa hawanywi pombe wala kula kiti moto na mara zote sikuwaona kanisani kwetu. Kwamba walikuwa wanakwenda msikitini Ijumaa, hili lilikuwa jambo la kawaida wala halikupata kutushitua. Si hilo tu, hata hapa Dar es Salaam ninapoishi, marafiki zangu wengi ni Waislamu.
Nenda Zanzibar na hata mikoani kama Iringa, Tanga, Mbeya, Mwanza na mikoa karibu yote ninao marafiki wakubwa wa dini ya Kiislamu. Tumesaidiana katika shida na raha kama Watanzania na si kwa dini zetu. Hata nilipokuwa katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Kambi ya Oljoro, nilipata marafiki wengi kutoka Zanzibar na kwa wanaokumbuka mmoja tulikuwa tukimwisha ‘Big O’.
Leo tunalo tatizo kubwa litakalotupiganisha vita ya udini. Zimeanza kuibuka lugha za kushindanisha wingi wa waumini kati ya Waislamu na Wakristo. Zimeibuka lugha za kwamba Waislamu wanakatwa maksi kwenye mitihani. Zimeibuka lugha kwamba Sensa ya Watu na Makazi iwe na kifungu cha kutanabaisha idadi ya Waislamu ni wangapi hapa nchini.
Kila wakati najiuliza maswali mengi. Hivi tukijua idadi hii itatusaidia nini kama Watanzania? Lakini pia kuna mfumo wa kutoiamini Serikali. Je, hivi ikitokea utafiti ukaonyesha kuwa Waislamu ni asilimia 80 ya Watanzania wote au kinyume chake, hizi takwimu zitaaminika? Je, zitasaidiaje kuharakisha maendeleo? Lengo la Sensa ya Watu na Makazi ni Serikali kupata takwimu za kusaidia kuandaa mipango ya maendeleo kwa mujibu wa idadi ya watu.
Kwamba Sensa haipo kutambua makabila au dini, vitu vinavyoweza kuwa chimbuko la ubaguzi, bali ipo kueleza wilaya au mkoa upi una wananchi kiasi gani fedha za maendeleo zigawanywe kwa idadi sawa na wingi wa watu waliopo.
Yupo rafiki yangu Mwislamu amefikia hatua ananiletea ujumbe eti msikiti wa eneo fulani umechomwa moto nichapishe, binafsi nilipokwenda katika eneo uliko msikiti nikakuta Waislamu ndani wakiswali. Nilipomuuliza akaanza kuuma midomo. Hali hii inanisikitisha.
Ukurasa huu unazidi kuwa mfupi, ila nihitimishe kwa kusema nchi yetu inaweza kuendelea kwa kasi kama tu tuaenzi Utanzania wetu zaidi kuliko dini na makabila yetu. Mkondo tunaotaka kuuchukua si muda mrefu tutakuwa kama Kenya na tukifikia hapo, maendeleo tuyasahau.
Tutauana hapa duniani na tukifika mbinguni tutakuwa hatuna la kujieleza. Mungu apishie mbali na sote tuione hatari inayotunyemelea tujiepushe na udini, kwani madhara yake ni makubwa kuliko faida tarajiwa. Amani kwanza.
Mungu ibariki Tanzania.