Baadhi wananchi wa Kata ya Kalemawe Wilayani Same (Jimbo la Same Mashariki) wameiomba Serikali kuboresha Sheria ya kiwango cha fidia (kifuta machozi) kinachotolewa kwa waathirika wa uvamizi wa Wanyama wakali na waharibifu (Tembo) ambao wamekuwa kero kubwa kwenye maeneo yao.
Wameeleza hayo kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Wilaya ya Same Kailda Mgeni na wananchi hao ambapo wamesema kiwango kinachotolewa kwasasa hakiendani kabisa na athari zitokanazo na wanyamapori hao pindi wanapovamia mashamba yao.
Akitolea ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi hao mkuu huyo wa wilaya amesem “Habari njema ni kwamba sheria hiyo imebadilishwa tayari na kwa wale Wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa kwa kipindi cha mwaka 2023/24 Serikali ikija kuanza kulipa fidia (kifuta machozi) itaanza kutumika sheria mpya na siyo ile ya zamani, sambamba na hilo katika mwaka wa fedha 2024/25 kuna kituo cha kufuatilia mwenendo wa Wanyama hao pindi wanapotoka kwenye hifadhi ili askari waweze kuwadhibiti kabla ya kuleta madhara kwenye jamii”
Adha alisisitiza wananchi kuwa, Serikali imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kukabiliana na Wanyama hao ikiwemo kutoa mafuzno kwa vijana (Askari wa Wanyama pori vijijini VGS) ya matumizi ya vifaa vya kufukuzia Tembo kwenye kila jamii zinazozunguka Hifadhi hivyo utaratibu huo unapofika kwenye jamii zao wajitokeze kwa wingi kupata hiyo elimu itawasaidia kujikinga na madhara yatokanayo na uvamizi wa Wanyama hao.
Pia DC Kasilda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maliasaili na Utalii kwa jitihada zake za dhati za kutatua changamoto ya Wanyama pori waharibifu wa mazao ya binadamu yaani Tembo ambao wamekuwa kero kubwa kwa Wananchi wa Same wanaozunguka hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, pamoja na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki mama Anne Kilango, akisema matokeo ambayo yanaonekana leo hii ju ya changamoto hiyo ni jitihada zake ambazo amezifanya akiwa Bungeni kusimama vyema kwenye nafasi yake ya uwakilishi wa wananchi kulisemea jambo hilo hali ambayo imefanya Serikali kusikia hoja zake na kuzifanyia kazi kwa vitendo.