*Walionyanyaswa na Savile walikuwa wapi akiwa hai?

Mwaka uliopita nilikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliokuwa mitaa ya Roundhay, Leeds, baada ya kifo cha Jimmy Savile.

Watu wengi walijipanga mtaani kwake na kusema ukweli machozi yaliwatoka wakubwa na wadogo, bila kujali alikufa akiwa na umri mkubwa. Miaka 84 si umri mdogo leo, na kwa mtu aliyekuwa tayari mgonjwa ungeweza kusema afadhali amepumzika, bali kwa wanadamu hata siku moja huwezi kusema hivyo.


Mheshimiwa huyu ni mtunukiwa wa malkia, ndiyo maana hadi anazikwa aliitwa Sir James Wilson Vincent Savile, OBE, KCSG na umaarufu wake mkubwa ameupatia kwenye televisheni ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).


Mwaka mmoja baada ya kifo chake, mengi yamesemwa hadi dola imeshindwa kukaa kimya na kuanzisha uchunguzi juu ya tuhuma za nyanyaso za kingono alizokuwa anafanya bwana huyu. Wakati wa uhai wake, ugonjwa, kifo hadi tunamlaza kaburini, hakuna aliyetoa tetesi hizo nje ya kifua chake.


Uendeshaji wake wa vipindi katika BBC ulikuwa murua kwa wengi; kwa mfano, shoo yake kubwa ya ‘Jim’ll Fix It’ imebaki kama alfa na omega. Vipindi vyake vilipendwa nyumbani hapa na ng’ambo ambako mamilioni walimjua kupitia runinga zao na pia maisha katika jamii.


Katika salamu za rambirambi za zaidi ya wengi, alipewa sifa ya kutokuwa na makuu na kufanya mambo kwa kujitolea kusaidia wengine. Hakuna aliyekuwa na wasiwasi kwamba Jimmy alishafika peponi, sasa hizi tuhuma mpya zimekuwa kama kufukua kaburi lake na kuutoa mwili wake kuuchunguza upya.


Watu hawa walikuwa wapi alipokuwa hai wakaacha kudokeza kuhusu kiu yake ya ngono, inayodaiwa kupitiliza aliyoitibu kwa nyanyaso? Maana watu wamemjengea picha nzuri wakati wote akiwa hai hadi anakufa. Na sababu moja ya mambo makubwa aliyofanya ni kuchangishia taasisi za misaada zaidi ya paundi milioni 40.


Kuna watu sasa hivi hawaelewi chochote juu ya hizi tetesi za unyanyasaji wa kingono, maana wanamwita Saint Jimmy kwa jinsi alivyowasaidia wao, watoto wao, wazazi wao na hadi taasisi za misaada.


Sasa, Scotland Yard imeanzisha uchunguzi rasmi juu ya unyanyasaji wa kijinsia aliofanya na kusema BBC inaweza kuanzisha wa kwao wa ndani na kwenda nao sambamba. Hakuna anayesema uchunguzi huu usifanywe, lakini wahusika wanaodaiwa kufikia zaidi ya 200 walimuogopa nini akiwa hai?


Angekuwa na umbo kubwa na sura ya kutisha kama Idi Amin aliyeiteka Mutukula, tungesema waliogopa, lakini kwa udogo wake wa umbo na sura isiyokuwa na chembe ya kitisho, walikaa kimya kwa lipi? Wamesubiri hadi amepoteza uhai kwa ugonjwa na kujitokeza kusema walinyanyaswa. Hawezi tena kujitetea, labda miujiza itokee na hii si haki kwake wala familia yake.


Halafu ushahidi ukishapatikana kwamba alifanya unyanyasaji wa kingono, watalichapa fimbo kaburi lake au kulifunga minyororo kama adhabu kwa miaka kadhaa? Isijekuwa huu ni uchu wa watu wachache wanaotaka kuanza kudai fidia, kwa sababu wanajua BBC ni shirika kubwa na marehemu aliacha akiba kubwa sasa wafidiwe. Kama ni watoto walinyanyaswa kijinsia, ina maana hawakuwaeleza wazazi au walezi wao hadi huyu mtu amepoteza uhai wake?


Si jambo zuri kwamba habari nzima inajengwa juu ya marehemu huyu, asiyeweza tena kuinua mkono wake wala mdomo kujitetea. Tunajua kwamba kituo cha televisheni cha ITV cha Uingereza, ambacho ni mshindani wa BBC, kilianzisha mada na kurusha kipindi cha ‘uchunguzi’ kuhusu tabia ya Savile, kikikiita upande wa pili wa Jimmy Savile.

 

Inawezekana kabisa huku ni kutafutana jinsi ya kuharibiana hadhi, kuvuruga biashara kuonesha kama vile BBC ilikuwa na mambo hayo kwa ujumla na ITV hakuna.

Lakini kwa vile hii ni kazi ya polisi, acha waendelee nayo, ila haitakuwa ni kupata ukweli wa Savile mwenyewe, na yanaweza kubumburuka mambo kuhusu hao hao wanaochunguza na pia vyombo tofauti kabisa vya habari.


Mara nyingi Upinzani huwa na malengo ya kukosoa, kujenga hoja na kutoa mbadala wa mambo. Lakini katika hili la Savile, nilimwona Kiongozi Mkuu wa Upinzani, Ed Miliband, akimtaka Waziri Mkuu, David Cameron, aanzishe uchunguzi haraka na akamtupia lawama.

 

Wala hili halikuwa la Cameron, maana Waziri Mkuu kwa nafasi yake hahusiki na mambo hayo hata kidogo, ndiyo maana alikaa kimya hadi sasa Scotland Yard wameanza kazi.


Mimi nasema wachunguze, lakini watu wajenge tabia ya kujitokeza mapema kusema pale mambo yanapochafuka kwenye jamii, na wasisubiri hadi mtu afe au televisheni itangaze kipindi kuwasisimua.