Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni na kutoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo/ tahasusi/ kozi kwa njia ya mtandao (online).

Aidha zoezi hilo la kubadilisha tahasusi na vyuo litaanza rasmi tarehe 31 Machi, 2025 hadi tarehe 30 Aprili, 2025. Wanafunzi, wazazi na walezi wanakumbushwa kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au Kozi.

Waziri wa TAMISEMI Mohammed Mchengerwa ameeleza hayo leo April 2,2025 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2024 kuhusu fursa ya kubadilisha machaguo ya Tahasusi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Kati na Elimu ya Ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Tano na Vyuo.

Hatua hii imekuja ikiwa ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali Mwaka, 2025 na ambapo ameeleza kuwa baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao.

“Itakumbukwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (combination) na Kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform.) Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani, “ameeleza.

Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa Ofisi hiyo inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya sekondari Kidato cha Nne, mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi zaidi kwa mwanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomwandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadaye.

Amesema zoezi hilo litatoa fursa zaidi ya wanafunzi kuongeza machaguo na kufanya machaguo mapya ya Tahasusi na Kozi huku akiwasihi wazazi/ walezi kushiriki katika zoezi hili kwa kushauriana na watoto wao katika kufanya machaguo sahihi kulingana na ufaulu wao.

“Nawahimiza wahitimu wote kufanya marekebisho ya machaguo ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao, kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS) unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz., maelekezo kwa wahitimu na jinsi ya kufanya mabadiliko watayapata kwenye mfumo kupitia user manual pamoja na video ya youtube zilizopo kwenye mfumo huo, “amesema.

Sambamba na hayo Waziri huyo ameeleza kuwa ili kuingia kwenye mfumo itabidi mhitimu atumie Namba ya Mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2024, Jina lake la Mwisho, Mwaka wa Kuzaliwa na Alama ya Ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa.

“Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha Tahasusi na Kozi kulingana na ufaulu waliopata. Pia wataweza kusoma tahasusi/kozi ambazo wamefaulu vizuri ama wana malengo nazo zaidi, ” amesisitiza Waziri Mchengerwa na kuongeza;

Ninawasisitiza wanafunzi, wazazi/ walezi kutumia muda huo vyema ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza mara baada ya matokeo ya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa, “amesema.

Kadhalika waziri huyo ameeleza kuwa ni muhimu kuzingatia muda uliotolewa wa kufanya marekebisho ili ratiba ya kuwachagua na kuwapangia shule na vyuo iweze kuendelea kwa muda uliopangwa na kwamba baada ya matokeo ya kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo kutangazwa, Ofisi haitashughulikia changamoto hizo kwa kuwa fursa ya kufanya mabadiliko hayo imeshatolewa.

“Huduma hii ya kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi watapata changamoto, wawasiliane na Dawati la Huduma la Mteja kupitia barua pepe: [email protected] au kuwasiliana moja kwa moja na Kituo cha Huduma kwa Wateja kwa simu +255 262 160 210 na +255 735 160 210,kwa mwanafunzi, mzazi/mlezi atakayekuwa na suala linalohitaji maelezo au ufafanuzi zaidi aende katika Ofisi za Elimu za Mikoa na Halmashauri, “ameeleza.