Wahasibu wanawake nchini wametakiwa kusimamia vizuri fedha za umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.


Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo kwa niaba ya Katibu Mkuu, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, katika ufunguzi wa mafunzo kwa Wahasibu Wanawake kutoka kwenye Mafungu na Halmashauri.

Bi. Omolo alisema Serikali inatarajia wahasibu hao watazingatia mafunzo yanayotolewa ili kuleta tija na kufikia lengo la Serikali la kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.

Alisema katika mafunzo hayo wahasibu watajifunza kuhusu mawasiliano, masuala ya fedha na uwezeshaji wa kiuchumi, usimamizi wa wakati, namna ya utatuzi wa matatizo na maadili pamoja na afya ya akili.

“Mafunzo haya yatawaongezea uwezo mzuri katika mawasiliano kwa maandishi, mawasiliano ya kibinafsi na majadiliano kwa kukuza ujuzi wa kusikiliza na kuelewa mitazamo ya wengine. ujuzi wa mawasiliano kwa wanawake wahasibu itasaidia kujenga uhusiano mzuri, kukuza uwazi na mshikamano na kutatua migogoro mahali pa kazi na kwenye jamii”, alibainisha Bi. Omolo.

Bi. Omolo alisema elimu hiyo itawafanya wahasibu hao wawe na ujuzi stahiki wa usimamizi wa kifedha binafsi, kupangilia bajeti na matumizi, kuona fursa za uwekezaji na namna ya kuzitumia.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi Bw. Ayoub Banzi kwa niaba ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leonard Mkude, alisema mafunzo hayo yatatolewa kwa wahasibu wanawake takribani 300 ambao ni sehemu ya wahasibu wanawake kutoka Mafungu na Halmashauri zote za Tanzania Bara.

Alisema mafunzo hayo ni ya kwanza kutokewa katika mafunzo mengi ambayo wanatarajia kufanya ili kuendeleza na kuunga mkono juhudi za kumnyanyua na kumuwezesha mwanamke.

Baadhi ya Wahasibu wanawake walioshiriki mafunzo kwa Wahasibu Wanawake kutoka kwenye Mafungu na Halmashauri ili kuwajengea uwezo wa usimamizi wa fedha za umma yaliyofanyika jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – WF, Dodoma)
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, akifungua kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, mafunzo kwa Wahasibu Wanawake kutoka kwenye Mafungu na Halmashauri ili kuwajengea uwezo wa usimamizi wa fedha za umma yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bw. Ayoub Banzi, akizungumza kwa niaba ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bw. Leonard Mkude, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Wahasibu Wanawake kutoka kwenye Mafungu na Halmashauri ili kuwajengea uwezo wa usimamizi wa fedha za umma yaliyofanyika jijini Dodoma.