Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah amewataka wahariri kuzingatia matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili ili kukikuza zaidi duniani.
Hayo ameyabainisha leo Julai 4, 2023 wakati akifunguwa kongamano lililowakutanisha wahariri wa habari kutoka Tanzania Bara na Visiwani kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdull Wakil visiwani Zanzibar yenye kauli mbiu ‘Kiswahili Chetu , Umoja Wetu’
Amewataka wahariri wa vyombo vya habari kuchukuwa nafasi ya kulinda lugha ya kiswahili ili kuhakikisha hakuna upotoshaji unaofanywa ambao utaathiri maendeleo ya lugha hiyo kwa kizazi kijacho.
Amesema ni wakati wa kuweka mikakati kuona lugha ya kiswahili inatumika vizuri na kuepusha matukio ya uharibifu wake unaotokana na upotoshaji wa makusudi.
Amesema matumizi sahihi na sanifu ya lugha ya Kiswahili kwa kiasi kikubwa yatafungua nafasi na fursa kwa vijana mbalimbali kujiajiri katika lugha hiyo nje ya nchi.
Aidha amepongeza juhudi zinazochukuliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) pamoja na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) kuona utafiti zaidi unafanyika katika kukuza lugha ya kiswahili ikiwemo matayarisho ya matumizi ya kamusi sanifu ya lugha hiyo.
Amesema utafiti huo ni muhimu kwa ajili ya kukiendeleza kiswahili na kuwa miongoni mwa lugha maarufu inayotumiwa na watu wingi duniani kote.
“Tayari jumla ya vyombo vya habari vya utangazaji redio 38 duniani zinarusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili hivyo ni vyema waandishi wa habari kuitumia fursa hiyo”amesema.
Naye Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita, amesema wakati umefika kwa vyombo vya habari kukitumiya kiswahili kama ni bidhaa itakayoleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi ikiwemo ajira.
Amesema matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili yatasaidia kupatikana kwa ajira kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya nje ya nchi pamoja na kufanya kazi katika taasisi za elimu ya juu.
Naibu Waziri wa Utamaduni sanaa na michezo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Khamis Mwijuma amewataka wahariri kukipa hadhi na nafasi lugha ya kiswahili ambayo imekuwa ikipata umaarufu siku hadi siku duniani.
Amesema zipo fursa nyingi za lugha ya kiswahili katika ngazi ya kimataifa kwa sababu wageni wingi wamekuwa na hamu ya kujifunza lugha hiyo katika kiwango cha kimataifa zaidi”alisema.
Akiwasilisha mada nafasi ya wahariri wakuu katika kusimamia matumizi sanifu katika vyombo vya habari na kulinganisha na vyombo vya habari vya nje, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Charles Hilary, amesema wahariri wanapaswa kufuatilia na kusimamia matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili.
Amesema baadhi ya vyombo vya habari watangazaji wake wingi wanachanganya lugha ya kiswahili pamoja na Kiingereza na hivyo kuwepo kwa upotoshaji mkubwa.
Akizungumza katika kongamano hilo katibu mkuu wa Baraza la Kiswahili BAKIZA Consalate Mushi amevitaka vyombo vya habari kuchukuwa juhudi za kusambaza kiswahili ili kuingia katika miongoni mwa lugha bora duniani.