Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wahariri wa vyombo vya habari nchini wametakiwa kuchukua hatua katika kupambana na magonjwa ya moyo ikiwa ni pamoja na kula vyakula bora, kufanya mazoezi na kutokunywa pombe kupitiliza.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samuel Rweyemamu wakati akitoa elimu ya magonjwa ya moyo katika mkutano mkuu wa mwaka wa wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Dkt. Rweyemamu alizitaja sababu zingine zinazosababisha magonjwa ya moyo ni pamoja na matumizi ya bidhaa aina ya tumbaku, changamoto za maisha zinazosababisha msongo wa mawazo na mgonjwa kurithi tatizo hilo.
“Ninawaomba mchukuwe hatua ili muweze kupambana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo kwani magonjwa haya ambayo matibabu yake ni ya gharama kubwa unaweza kuyaepuka kwa kufuata ushauri wa kitaalamu”,alisema Dkt. Rweyemamu.
Alizitaja dalili za ugonjwa wa moyo kuwa ni pamoja na kifua kuuma, kubanwa na pumzi, ongezeko la mapigo ya moyo, ukitembea kidogo unachoka, miguu na tumbo kuvimba, kichomi kwenye kifua kwa upande wa kushoto, miguu kujaa, kukosa pumzi, kukohoa kifua kikavu, ganzi mwili mzima, kichwa kuuma na kusikia kizunguzungu.
Dkt. Rweyemamu alisema endapo mtu atapata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo asiache kutumia dawa atakazoandikiwa na mtaalamu wa afya kwani tiba ya magonjwa hayo ni endelevu na endapo mgonjwa ataacha kutumia dawa anaweza kupoteza maisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha Taasisi hiyo Anna Nkinda aliwashukuru wahariri hao kwa kufanya kazi na JKCI ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa ya moyo.
Anna alisema ili kusogeza kwa ukaribu zaidi huduma za kibingwa za matibabu ya moyo JKCI ilianzisha huduma ya tiba mkoba ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan outreach services kwa kufanya kambi maalumu za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi.
“Gharama za matibabu ya moyo ni kubwa ninawaomba tunapotangaza kuwa na kambi za matibabu ya moyo kwa wananchi mtusaidie kutoa taarifa ili watu wengi wafahamu na kwenda kupima afya za mioyo yao mapema kuliko kusubiri wakati wameanza kuumwa”, alisema Anna.