Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imewataka wahandisi nchini kubuni teknolojia rahisi zitakazoweza kutatua changamoto za maisha ya wananchi vijijini na kuongeza kasi ya maendeleo nchini.
Hayo yamesemwa Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi, Godfrey Kasekenya ,wakati akifunga maadhimisho ya 19 ya siku ya Wahandisi yaliyomalizika jijini Dodoma.
Mhandisi, Kasekenya amesema maendeleo ya kimkakati nchini yatafikiwa endapo ubunifu na teknolojia zitawanufaisha wananchi wengi hususan waishio vijijini.
“Hakikisheni teknolojia hizi nzuri mnazoonesha mwaka hadi mwaka zinaweza kutumiwa kikamilifu na wananchi waishio vijijini na wenye kipato cha chini ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kuleta maendeleo kwa taifa zima” amesema.
NHata hivyo ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kuwasilisha mapendekezo yote yaliyotolewa katika mkutano huo wa siku mbili Wizarani ili yaweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuleta tija kwa kada ya wahandisi nchini.
”Kuna umuhimu wa Wahandisi kuungana ili kunufaika kwa mitaji, uzoefu na hivyo kuwa na nguvu ya pamoja itakayowawezesha kukua na kukuza teknolojia ndani na nje ya nchi.”amesema Mhandisi, Kasekenya
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Mhandisi,Balozi Aisha Amour amewataka washiriki wa mkutano huo kutumia maarifa waliyoyapata katika utekelezaji wa majukumu na kutoa elimu waliyoipata kwa wahandisi wengine ili kujenga uelewa wa pamoja katika jamii ya wahandisi nchini.
Naye Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Mhandisi Bernard Kavishe amesema zaidi ya makampuni 70 yameshiriki kuonesha bidhaa za kiteknolojia katika maonesho hayo na wahitimu 36 waliofanya vizuri katika vyuo mbalimbali vya kihandisi nchini wametunukiwa zawadi mbalimbali ikiwa ni chachu ya kuwahamasisha wanafunzi nchini kupenda fani ya uhandisi.