Watu wenye matatizo ya macho takribani 700 wamefanyiwa uchunguzi na kati ya hao wagonjwa 300 waliobainika kuwa na matatizo ya macho wamefanyiwa upasuaji na kurejeshewa hali ya kuona vizuri.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mpango wa Huduma za Macho kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Bernadetha Shilio wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya afya ya macho duniani kilichofanyika mapema leo katika viwanja vya Nyerere jijini Dodoma.
“Siku ya afya ya macho duniani ina lengo kuu la kuhamasisha utekelezaji wa dira ya kimataifa ya kutokomeza upofu unaozuilika ifikapo mwaka 2020, na kutathmini haki ya kuona kwa wote ambapo mwaka 2003 serikali ya Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani katika kutekeleza azimio hilo”. Alisema Dkt. Shilio
Dkt. Shilio amesema Serikali ya Tanzania inashirikiana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya afya ya macho ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa jamii, kutoa huduma za uchunguzi wa macho pamoja na kufanya upasuaji kwa wagonjwa ambao watabainika kuwa na matatizo.
Pia Dkt. Shilio ameiasa jamii ya kitanzania kuzingatia kanuni sahihi za utunzaji wa macho ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza na kusababisha uono hafifu na kupelekea upofu.
“Matumizi ya rangi na kope bandia kwenye ukingo wa macho, kuvaa miwani bila kupima, kutumia dawa za mgonjwa mwingine wa macho bila ushauri wa daktari, kutokula vyakula bora vyenye virutubisho na kutokua na tabia ya kupima macho angalau mara moja kwa mwaka vimetajwa kuwa visababishi vikubwa vya kuathiri afya ya macho” alisema Dkt. Shilio.
Aidha, Dkt. Shilio amesema sambamba na huduma za macho pia kumekua na huduma za uchunguzi na ushauri kwa magonjwa yasiyoambukiza jijini Dodoma, jumla ya watu 400 walifanyiwa vipimo vya sukari, shinikizo la damu na kiwango cha unene. Ambapo asilimia 3 wamekutwa na kiwango cha juu cha sukari, asilimia 47 wamekutwa na shinikizo la juu la damu na asilimia 50 wamekutwa na unene uliopitiliza kiwango.
Kwa upande wake Mgonjwa aliyepata huduma za macho Jijini Dodoma Bi.Veronica Maganga ameishauri serikali kuendelea kutoa elimu, kusogeza na kutoa huduma za macho na uchunguzi wa magonjwa mengine karibu na wananchi ili kuzuia magonjwa yanayoweza kuleta madhara iwapo hayatachunguzwa mapema na kutoa matibabu sahihi.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea huduma hii kwani wengi tumepata matumaini ya kuona tena kwa uono mkubwa ila wangefanya huduma hii iwe endelevu mpaka vijijini ili kuwanusuru wenye matatizo ya macho” alisema Bi. Veronica.
PICHA NA WIZARA YA AFYA