Tatizo la vifo vya wajawazito na watoto wachanga Tanzania limekuwa likisababisha majonzi makubwa kwa jamii, ongezeko la watoto wa mitaani na hata kupungua kwa nguvu kazi ya Taifa.
Ili Taifa changa kama Tanzania liweze kupiga hatua za haraka kimaendeleo, halina budi kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wake.
Licha ya kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa nchi zilizokubali kutekeleza mkataba wa kuimarisha huduma za afya duniani kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga ifikapo mwishoni mwa malengo ya milenia namba 4 (MDG4) mwaka huu 2015, jitihada zilizochukuliwa hazitoshi ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo.
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii za mwaka 2014 zinaonesha kwamba Tanzania ni nchi ya saba duniani kwa idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi, ambako takribani wajawazito 7,900 hufa kila mwaka, huku wastani wa watoto wachanga 40,000 wakipoteza maisha kila mwaka kabla ya kutimiza mwezi mmoja wa kuzaliwa.
Kama hiyo haitoshi, inakadiriwa kuwa watoto 100,000 hufa kila mwaka kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.
Kadhalika, watoto takribani 50,000 huzaliwa wakiwa wafu kutokana na sababu mbalimbali ambazo iwapo jitihada za makusudi zingechukuliwa mapema, zaidi ya asilimia 45 ya vifo hivyo visingeweza kutokea.
Pia asilimia 44 ya wasichana wanaofikisha umri wa miaka 19 nchini Tanzania huwa wameshapata ujauzito, bila kujali wapo shuleni au nje ya masomo.
Sensa ya Taifa ya mwaka 2012 inaonesha kuwa asilimia 54 ya Watanzania ni watu walio chini ya miaka 20 na hii inabainisha kuwa takribani miaka 15 hadi 20 ijayo idadi kubwa ya vijana wataingia umri wa uzalishaji kiuchumi.
Kutokana na hali hiyo, hatuna budi kutambua iwapo wagombea wa nafasi za urais na ubunge wamekata kiu ya wananchi katika kulizungumzia na namna watakavyolishughulikia tatizo kubwa la vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Kipindi tulichonacho ni cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa kumpata rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani.
Ukweli ni kwamba viongozi hawa wanakwenda kufunga mkataba kati ya watawala na watawaliwa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mkataba huo ni nyenzo muhimu sana ya kuhakikisha wagombea wote katika nafasi zao wanatambua wajibu wao na mahitaji ya jamii na kuyafanya kuwa ajenda stahiki katika majukwaa yao, ili wakichaguliwa waweze kuyatekeleza kikamilifu.
Afya ya mama na mtoto haijapewa kipaumbele cha kutosha, kutokana na kutokuwapo mfumo mzuri wa kutoa huduma stahiki kwa wajawazito ambao hufika kwenye huduma za afya na kukuta hali tofauti na matarajio yao.
Ni vyema sasa wagombea wanaotaka na wanaotarajia kuunda Serikali ya Awamu ya Tano wakatueleza kwa kina namna mada ya uzazi wa mpango itakavyowekwa, au itakavyoingizwa kwenye mitaala ya shule ili wanafunzi wa ngazi zote wajiandae kuwa wazazi wa baadaye kwa kuzingatia uzazi wa mpango.
Aidha, waieleze jamii iwapo watapata ridhaa hiyo suala la afya ya mama na mtoto watalishughulikia vipi ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali kuona suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele zaidi ikilinganishwa na masuala mengine.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya DSW, Mamaye Tanzania, Marie Stopes Tanzania, Pathfinder International, Umati na HDT yanabainisha kuwa tatizo la uzazi wa mpango nchini Tanzania bado ni changamoto.
Tafiti za mashirika hayo zinaonesha kuwa mimba zisizotarajiwa husababisha uwezekano mkubwa wa vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 9 ya vifo vinavyotokea nchini, na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka zaidi iwapo hatua za makusudi hazitatolewa katika jamii.
Uzazi wa mpango ni mkakati muhimu wa kuwasaidia wanawake kupanga muda wa kutosha kati ya uzazi na uzazi, kuzuia mimba katika umri mdogo na kuepuka mimba zisizotarajiwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), gharama za kuzuia ujauzito ni za chini zaidi kuliko gharama za matibabu yanapotokea matatizo wakati wa kujifungua.
Uzazi wa mpango unazipa uwezo familia na mtu binafsi kuchagua ukubwa wa familia, ambayo watamudu kuwekeza katika elimu na makuzi ya kila mtoto wao na kubaki na fedha za ziada, hatua inayoweza kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akinamama nchini, Dk. Moke Magoma, anasema kuna uwezekano mkubwa wa Tanzania kupiga hatua za haraka kimaendeleo iwapo jamii itapata uelewa wa kutosha kuhusu uzazi wa mpango.
“Ni muhimu sana kuwapo kwa huduma za afya ya mjamzito na mtoto mchanga, ambayo katika uhalisia wake inajidhihirisha kwa kila aliye hai sasa amepatikana kupitia mama yake kuwa mjamzito,” anasema Dk. Moke.
“Uzazi wa mpango ni muhumu sana hasa kwa wanawake kwa kuwa wanaweza kudhibiti uzazi, wanaweza kumaliza masomo yao,kufanya kazi wanazozitaka na kushiriki katika uamuzi wa kiuchumi na kisiasa.”
Dk. Moke anasema uzazi wa mpango ni njia bora zaidi katika uhai wa afya ya mama na mtoto na kwamba njia zote za kitaalamu za uzazi wa mpango hazina madhara kama baadhi ya watu ambavyo wamekuwa wakivumisha na kuwatia hofu wananchi.
“Kuna njia nyingi za kutumia uzazi wa mpango…lakini nikuhakikishieni kwamba njia za kitaalamu ni salama zaidi katika afya ya mama na hazina madhara kama baadhi ya watu wanavyodai…isipokuwa kuna ambao hupata maudhi madogo madogo na huisha baada ya muda mfupi,” anasema
Naye Dk. Msiima Mushumba kutoka Shirika la Marie Stopes Tanzania, anasema jamii inapaswa kutambua kuwa kuzaa watoto wengi bila mpangilio ni kuhatarisha maisha ya mama na kudumaza uchumi wa taifa.
Anasema kwa wastani familia inapaswa kuzaa watoto wasiozidi watano na kwamba kuanzia mimba ya sita na kuendelea huitwa mimba hatarishi ambapo anaitaka jamii kufuata njia za uzazi wa mpango.
Kadhalika, anabainisha kuwa wananchi ambao hawakufanikiwa kusoma wana kiwango kikubwa zaidi cha kuzaa kuliko waliosoma, kwa kuwa wengi wao hutambua umhimu wa kuzaa kwa mpango kuliko ambao hawakusoma.
Dk. Mushumba anasema jitihada za makusudi zinahitajika kupitia Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na jamii kwa ujumla, kuhakikisha huduma za uzazi wa mpango zinawafikia wanawake wote nchini kwa kuwa ongezeko la vijana ni aslimia 65 ikilinganishwa na wazee.
Pia Dk. Mushumba anaishauri Serikali kuongeza huduma za Bima ya Afya (NHIF) na CHF kwa wananchi wake, kutokana na jamii kubwa kukabiliwa na uelewa duni wa huduma hizo zinazosaidia kunusuru maisha ya mama na mtoto inapojitokeza shida wakati hospitali ikiwa haina dawa na vifaa.
Anasema mchango wa jamii katika mifuko hiyo huboresha sehemu za kutolea huduma za matibabu katika hospitali kwa wanachama wa mifuko hiyo, ambapo kwa kiwango kikubwa imechangia kupunguza kero ya upatikanaji wa dawa kwa wateja wake.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanachama wake kupata huduma bora za matibabu kutokana na ukweli kwamba mtu akiwa na afya njema ana nafasi kubwa ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) ikilinganishwa na wenye afya dhaifu.
Utafiti uliofanywa na wataalamu wa sekta ya afya nchini ulibaini baadhi ya mikoa imefanya vizuri katika huduma za Bima ya Afya ikiwamo Dodoma asilimia 22, Mbeya (24) na Singida (36) huku nyingine zikiwa nyuma zaidi ikiwamo Mkoa wa Geita ambao una asilimia 6 tu.
Akizungumzia suala la uzazi wa mpango, mgombea Ubunge wa Jimbo la Geita Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Peter Malebo, anasema iwapo atapata ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo, ajenda ya afya ya mama na mtoto ataipa kipaumbele cha kwanza kwa kuwa hakuna jambo linaloweza kufanyika pasipo kuwa na afya njema kwa jamii.
“Iwapo wananchi watanichagua kuwa mbunge wa jimbo hili, nitahakikisha naishauri Serikali kuweka kitengo maalum kwa ajili ya kuhudumia afya za wajawazito na watoto wachanga pekee tofauti na ilivyo hivi sasa,” anasema na kuongeza:
“Miongoni mwa mambo nitakayokomaa nayo ni kuhakikisha Serikali inaweka kwenye mitaala ya shule za msingi, sekondari na vyuo elimu ya uzazi wa mpango ili ifahamike kuanzia chini badala ya kuwaachia wananchi wenyewe iwapo watabaini inafaa huku vijijini wakiwa hawajui umuhimu wake.”
Hata hivyo, Malebo amesema vifo vinavyoendelea kutokea nchini Tanzania ni matokeo ya baadhi ya viongozi kutolipa kipaumbele suala la afya kutokana na idadi kubwa ya viongozi hao kutibiwa nje ya nchi wanapougua.
Naye, mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Costantine Kanyasu, amedai kwamba kuna haja kwa Serikali kutenga bajeti ya kutosha katika huduma za afya ili kunusuru maisha ya Watanzania ambao wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu wanapofika kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Amesema iwapo atapata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo, atahakikisha kunakuwa na mpango madhubuti wa kutoa elimu kwa jamii namna ya kutumia uzazi wa mpango kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuwa na familia bora na yenye watoto wenye akili.
“Uzazi wa mpango ni muhimu sana. Itambulike kuwa mtoto anayezaliwa kwa kufuata njia sahihi na kwa wakati sahihi hauguiugui, na mtoto asipouguaugua anakuwa na akili sana lakini pia humfanya mama kuwa na afya inayoweza kumsaidia kufanya kazi nyingine za uzalishaji mali,” anasema Kanyasu.
Naye mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kwa chama cha ACT-Wazalendo, Mugongo Fortunatus, anasema iwapo ataongoza jimbo hilo, atahakikisha anaungana na wabunge wengine kuishinikiza Serikali kutoa huduma stahiki kwa wajawazito na watoto wote kama ilivyokwishaahidi.
Anasema miongoni mwa mambo inayotarajia kuyafanya ni kuhakikisha ahadi ya Serikali ya kituo cha afya kila kata na zahanati kila kijiji yanatekelezwa kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuongeza wataalamu wenye ujuzi wa kuhudumia wanawake na watoto.
Anadai kuwa kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikiwahadaa wananchi kuwa itatoa matibabu bure kwa wajawazito na watoto wadogo, kitu ambacho ni uongo na kwamba wajawazito wanatozwa fedha na vifaa vya kujifungulia hulazimishwa kujinunua wenyewe.
“Nitahakikisha huduma za afya zinapatikana kwa vitendo, nitambana mkuu wa wilaya kama Serikali kuu, nitambana mkurugenzi wa halmashauri kama mtendaji mkuu wa halmashauri kuhakikisha fedha zote zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya afya zinafika kwa walengwa, badala ya kuzibadilishia matumizi na baadhi ya watumishi kujinufaisha wao binafsi,” anasema Fortunatus.
Hata hivyo, jamii inao wajibu wa kuwahoji wagombea wote namna watakavyolishughulikia suala hili, badala ya kusikiliza sera za wagombea kwenye mikutano ya hadhara na kuondoka zao.
Mwandishi wa makala hii ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI na anapatikana kwa namba 0767 404501/0658 404501.