Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kuanzia Mwaka wa Fedha 2024/25 kuwalipa waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi nchini posho za madaraka kutokana na kazi kubwa wanayofanya ya kusimamia utoaji wa huduma bora za afya, utawala pamoja na usimamizi wa miradi.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo Februari 14, 2024 wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wafawidhi wa Vituo vya kutolea huduma za Afya ngazi ya msingi uliofanyika Jijini Dodoma.
“Waganga wafawidhi mnastahili kulipwa posho ya madaraka, mnafanya kazi kubwa kwenye vituo vya kutolea huduma ninyi ndio madaktari, wafamasia, wataalam wa maabara, mnasimamia ujenzi wa miradi ya Serikali hakika mnastahili kulipwa posho hii.” Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watumishi wanakuwa na mazingira wezeshi ya kufanya kazi pamoja na motisha kazini hivyo Serikali ya Rais Samia na yeye pamoja na Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa Mhe. Mohammed Mchengerwa watahakikisha wanaenda simamia suala hilo ili waganga wafawidhi wa vituo waanze kupata posho za madaraka.
Hata hivyo Waziri Ummy amewataka Waganga wafawidhi kuhakikisha wanaendela kusimamia ubora wa huduma za afya katika vituo wanavyovisimamia, kusimamia vyema miradi ya maendeleo inayofanyika katika vituo vyao na kuhakikisha watumishi walio chini yao wanafanya kazi kwa ufanisi ili kutimiza azma ya Serikali ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.