Hakuna nchi ambayo raia wake wameathirika kwa kutapeliwa fedha zao kupitia teknolojia za kwenye mitandao kama Uganda.

Wengi wamekwisha kufikia hatua ya kujiua baada ya kubaini kuwa wametapeliwa mabilioni ya fedha walizowekeza kupitia mitandao ya fedha za kidijiti (cryptocurrency).

Mmoja wao ni Ashraf Nusubuga, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere ambaye katika ujumbe aliouacha alieleza kuwa ameamua kujiua kutokana na sababu binafsi. Lakini Nusubuga hakujiua kwa sababu ya kusalitiwa na mpenzi wake au kwa sababu ya masomo. 

Kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 22 alijiua baada ya kupotea mamilioni ya fedha katika kampuni inayojihusisha na biashara ya cryptocurrency.

Aliwekeza fedha zake zote, baadhi akiwa amezikopa kutoka kwa marafiki, katika kampuni ambayo ilimuahidi kupata faida kubwa, lakini baadaye ikaja kubainika kuwa mfumo wake wa utendaji ni kama upatu.

Luke Oweyesigire, Naibu Msemaji wa Jeshi la Polisi jijini Kampala, anasema Nusubuga si mtu pekee ambaye amekumbwa na mikasa kama hiyo.

Kashfa kubwa kuhusiana na kampuni za cryptocurrency hivi sasa zinatikisa Uganda. Wakati kampuni hizo zinapoanzishwa, kwa kawaida wanatangaza faida kubwa ambayo ‘wawekezaji’ wataipata kutokana na uwekezaji wao. Hapo hufanikiwa kuwavuta watu wengi na kuifanya Afrika Mashariki kuonekana kuwa kitovu cha biashara ya cryptocurrency katika ukanda huu.

Lakini imebainika sasa kuwa kampuni hizo zimeutumia ujuha wa Waganda wengi kuhusiana na teknolojia ya cryptocurrency kuwatapeli.

Kukosekana kwa sheria au kuwepo kwa sheria hafifu kudhibiti teknolojia hii mpya katika eneo hili ni moja ya ababu zinazotajwa kuwaingiza watu wengi kwenye utapeli huu bila kujijua.

Sababu nyingine kubwa inayosababisha watu wengi waibiwe ni kukosekana kwa elimu miongoni mwa wananchi kuhusiana na cryptocurrency na masuala yanayohusiana na fedha za kidijiti.

Kashfa nyingine kubwa ya cryptocurrency nchini Uganda kutokea mwaka jana ilihusisha nchi nyingine zinazoendelea kama vile Japan, ambako Kampuni ya BITPoint ilipoteza dola milioni 28 za Marekani wakati matapeli nchini Uingereza na Uholanzi waliiba dola milioni 27 za Marekani kutoka kwa wateja wa Bitcoin, moja ya sarafu maarufu za mitandaoni huku mapateli wengine wa mtandaoni wakiiba dola bilioni 4.3 za Marekani kutoka kwa wateja mbalimbali.

Lakini Uganda ni miongoni mwa nchi ambazo watu wake wameathirika sana licha ya uchumi wake kuwa chini mno.

Takriban kampuni tano za cryptocurrency zimefungwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita nchini Uganda na kuondoka na jumla ya dola milioni 26 za Marekani zilizokuwa zimewekezwa na wateja. Waliotapeliwa wanahusisha wanafunzi, waumini wa makanisa ya kilokole, wanajeshi, watumishi wa serikali na wengineo.

Robert Bakalikwira, Ofisa Upelelezi anayefuatilia kesi hizi, anakadiria kuwa kwa ujumla, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Waganda wapatao 200,000 hivi wamepoteza kiasi cha dola bilioni moja za Marekani kwa matapeli hao mtandaoni, kiasi ambacho ni sawa na asilimia nne ya pato la taifa la dola bilioni 28 za Marekani kwa mwaka.

Kinachotokea Uganda ni tofauti na kinachotokea katika nchi nyingine, hasa za Magharibi. Wakati katika nchi hizo nyingine matapeli huingia mitandaoni na kuiba fedha kwa kutumia teknolojia, Uganda watu hutapeliwa kwa kupewa ahadi za uongo na kampuni. Kampuni hizo huwarubuni Waganda kwa kuwaonyesha faida kubwa watakayoipata wakiwekeza fedha zao. Mara nyingi ahadi hizo huwa ni za uongo. Baada ya mamia ya watu kuwekeza, kampuni hizo hufunga shughuli zake na kutokomea.

“Tumepokea kesi nyingi sana za watu kutapeliwa kupitia cryptocurrency feki,” anasema Fred Enanga, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Uganda. “Tunawashauri wananchi kujiepusha na kampuni za mtandaoni ili wasitapeliwe kirahisi,” anaongeza.

Kauli ya serikali yahojiwa

Watu wameanza kuhoji hatua ambazo serikali inazichukua kukabiliana na hali hii. Wananchi wengi wanaamini kuwa serikali na taasisi zake zina wajibu na zinapaswa kuwa na uwezo wa kuwakinga wananchi dhidi ya utapeli kama huu. Lakini serikali ilikwisha kuunda timu ya watu 10 kuchunguza suala hili. Baada ya ripoti hiyo kutolewa, tayari taarifa zimeshaanza kutolewa kwa umma, kuwaonya watu dhidi ya kampuni kama hizo.

Taarifa hizo zinaweka bayana kuwa Benki Kuu nchini Uganda na serikali kwa ujumla wake hazitambui teknolojia ya cryptocurrency.

Hata hivyo, wakati serikali haina sheria mahususi au kanuni kwa ajili ya suala hilo, bado haijatangaza kuwa ni kinyume cha sheria kuanzisha kampuni ya cryptocurrency nchini Uganda.

Wakizungumza bungeni mapema mwaka huu, baadhi ya wabunge walibainisha kuwa Kwame Rugunda, mtoto wa Waziri Mkuu, Ruhakana Rugunda, ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa CryptoSavannah, kampuni inayotoa ushauri kuhusiana na masuala ya cryptocurrency.

Museveni achochea

Rais Yoweri Museveni wa Uganda anaweza kuwa amechochea wananchi wengi kujiunga na kampuni hizo baada ya kutoa kauli iliyoonyesha kuwa yeye anaiunga mkono teknolojia hiyo. Katika hafla moja jijini Kampala Januari 2017, ambapo Gavana wa Benki Kuu, Emmanuel Mutebile, alisema haiamini sana teknolojia hiyo, Rais Museveni alimponda hapohapo na kubainisha kuwa Mutebile ni mmoja wa watu wahafidhina ambao hawataki kubadilika na akasisitiza haja ya kuiweka teknolojia hiyo mbele katika dunia ya sasa.

Watu wengi wa kawaida nchini Uganda, ambao elimu yao kuhusiana na masuala haya ya teknolojia ni ya chini sana, waliichukulia kauli hii ya rais kuwa kama ruhusa iliyotolewa kwa shughuli hizo nchini mwao. 

Wakaanza kuziamini shughuli hizo, hasa ikizingatiwa kuwa alisema ni mtu ambaye anafahamu mambo mengi kuhusu Uganda. Huo ukawa mwanya kwa kampuni safi na za kitapeli kuingia nchini Uganda.

“Museveni anahusika katika haya yanayowatokea Waganda wengi hivi sasa,” anasema Ken Wamala anayeishi mji wa Masaka, ambaye ametapeliwa dola 41,000 za Marekani.

Kampuni zinazotajwa kuwatapeli watu mamilioni ya fedha ni pamoja na Dumanis Coins, ambayo ilifunga shughuli zake Disemba 3, 2019, kiasi cha shilingi za Uganda milioni 2.7. Zaidi ya watu 10,000 walikuwa wamewekeza fedha zao katika kampuni hiyo.

Polisi tayari wamekwisha kumkamata mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo na msako wa wakurugenzi wengine wanne bado unaendelea.

John Kalevu, ambaye duka lake lipo jirani na zilizokuwa ofisi za Dumanis Coins, anasema alifika dukani kwake siku moja na kukuta milango ya ofisi hizo za cryptocurrency ikiwa wazi lakini ndani hakukuwa na mtu wala kitu chochote.

Ofisi nyingine, Global Cryptocurrencies, ilifungwa Novemba, Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Andrew Kagwa, alikamatwa baada ya msako wa wiki mbili. Zaidi ya watu 10,000 walikuwa wamewekeza fedha zao jumla ya dola milioni 8.2 za Marekani katika kampuni hiyo.

“Kampuni nyingine, Lion Cryptocurrency, ilifunga shughuli zake Oktoba 2019, ikiondoka na dola milioni 5.4 za Marekani zilizowekezwa na Waganda 17,000,” anasema Henry Musagala, mpelelezi kutoka Jeshi la Polisi.

One Coin, ni kampuni nyingine iliyowatapeli Waganda wengi. Ilikusanya kiasi cha dola milioni 6.8 za Marekani kutoka kwa Waganda 12,000. Kampuni ya D9 ilifunga shughuli zake ikiwa na kitita cha dola milioni 3.2 za Marekani ilizozikusanya kutoka kwa watu 9,000. 

Kampuni nyingine za cryptocurrency ambazo zilifunga shughuli zake na kuwaacha Waganda wengi wakiwa wanaugulia hasara ni pamoja na Team, Dutch International, Finetegry na Fital-Science.

Watumishi matatani

Watumishi wa kampuni hizi hawakuachwa salama. Mathalani, Sheila Nassali, ambaye ni muuguzi, anasimulia jinsi mkurugenzi wa Global Cryptocurrency alivyomshawishi ajiunge na kampuni yake kama mhudumu na mteja. Alipata mshituko pale mkurugenzi huyo alipopotea, akimuacha yeye akikabiliana na wateja wenye hasira ambao walikuwa wanadai fedha zao.

Patrick Mweheire, Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Mabenki Uganda anasema: “Waganda watakuwa salama zaidi wakiwekeza fedha zao kwa kununua ng’ombe kuliko kujiingiza kwenye ulimwengu wa cryptocurrency.”

Kwa upande mwingine, wataalamu na watumishi wa zamani wa kampuni hizi wanasema ujinga miongoni mwa Waganda wengi kuhusiana na masuala ya teknolojia hii ya cryptocurrency si tatizo pekee. 

Muzamiru Kigundu, ambaye aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Lion Cryptocurrency kabla haijafungwa, anadai kuwa maofisa wengi wa serikali ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni hizo ambazo zinaibuka kama uyoga nchini Uganda. Jambo hilo linawafanya Waganda wengi wa kawaida waziamini kampuni hizo.

“Kwa kawaida wakurugenzi wa kampuni hizi hupanga ofisi zao katika majengo mazuri na maarufu na wao wenyewe huendesha magari ya bei mbaya kuonyesha kuwa shughuli hiyo inazalisha utajiri mkubwa,” anasema.

Rushwa yachangia

Kukithiri kwa rushwa nchini Uganda kunatajwa kama moja ya sababu za kuibuka kwa kampuni hizi za kitapeli. Katika orodha inayotolewa na taasisi ya Transparency International, Uganda inatajwa kama nchi ya 160 kwa rushwa duniani.

Kutokana na kukithiri kwa rushwa, baadhi ya kampuni feki zilisajiliwa ingawa hazikutimiza vigezo na masharti ya usajili.

“Sababu kubwa ya kuibuka kwa kampuni feki za cryptocurrency ni rushwa,” anabainisha Prof. Joseph Bogere, Mhadhili wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Makerere.

Hata hivyo, mwisho wa yote, ni viongozi wa serikali na taasisi za ulinzi ambazo ndizo zenye wajibu wa kuhakikisha Waganda wanalindwa dhidi ya utapeli huu. Solomon Male, mchungaji wa kanisa, anasema kuwa hilo halionekani kutokea na kuwafanya wananchi maskini kuendelea kuibiwa na matajiri.

Cryptocurrency barani Afrika

Nigeria ni nchi barani Afrika ambayo inatajwa kuwa watu wake wamejikita sana kwenye masuala ya cryptocurrency. Takwimu za google zinaonyesha mathalani mwezi Aprili mwaka jana, Jiji la Lagos liliongoza kwa idadi ya watu waliokuwa wanaulizia kuhusu bitcoin mtandaoni.

Watu wengi wanaamua kutafuta suluhisho mtandaoni baada ya kuudhiwa na mifumo ya malipo iliyopo hivi sasa, ambayo inawazuia watu wengi kuitumia kufanya malipo au kupokea fedha. Mathalani, raia wengi wa Nigeria walichukizwa baada ya mfumo maarufu wa malipo, PayPal, kuwazuia kupokea fedha wanazotumiwa kutoka nje ya nchi yao kutokana na nchi hiyo kuwa na watu wengi wanaotajwa kwenye mipango ya utapeli.

Kwa kuwa watu hawana njia ya kutuma na kupokea fedha, wengi wanalazimika kutumia njia ambazo zinawagharimu fedha nyingi sana na wakati mwingine hazina usalama wa kutosha.

Ndiyo maana watu wengi barani Afrika wakaanza kuamini mifumo ya cryptocurrency, kwani awali iliwasaidia sana kufanya biashara kwa wepesi na sehemu nyingine yoyote duniani.

Utafiti umebaini kuwa biashara ya cryptocurrency imeshamiri sana barani Afrika ikilinganishwa na maeneo mengine duniani. Kiasi cha asilimia 5.5 ya watu wazima ambao wanatumia intaneti duniani kote wanatumia aina fulani ya fedha za kidijiti, lakini kuna nchi tatu barani Afrika ambazo zipo juu ya wastani huu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Hootsuite ya mwaka 2019, asilimia 10.7 ya raia wa Afrika Kusini wanajihusisha na biashara ya cryptocurrency, kikiwa ni kiasi kikubwa kuliko nchi nyingine yoyote. Nigeria inafuatia ikiwa na asilimia 7.8 na Ghana ina asilimia 7.3.

Makala hii imetafsiriwa kutoka mtandao wa OZY.