Wafungwa watano na walinzi watatu wameuawa katika majibizano ya risasi wakati wa jaribio la kutaka kutoroka katika gereza kuu katika mji mkuu Mogadishu. Wafungwa hao wanadaiwa kuwa ni wanachama wa Al-Shabaab.
Wafungwa watano wanaosemekana kuwa ni wanachama wa kundi wa wanamgambo la Al-Shabaab nchini Somalia na walinzi watatu wameuawa katika majibizano ya risasi wakati wa jaribio la kutaka kutoroka katika gereza kuu katika mji mkuu Mogadishu. Hayo yamesemwa na wakuu wa magereza na mashuhuda wa tukio hilo.
Al-Shabaab imekuwa ikifanya mashambulizi mengi ya mabomu na mashambulizi mjini Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo yenye machafuko, ingawa ni machache yamerekodiwa katika miezi ya hivi karibuni.
Serikali ya Somalia imeungana na wanamgambo wa koo za ndani kupambana na wanamgambo hao wa Kiislamu katika kampeni yake inayoungwa mkono na jeshi la Umoja wa Afrika pamoja na mashambulizi ya kutokea angani ya jeshi la Marekani ingawa mapambano yao yamekabiliwa na vikwazo vya kundi la Al-Shabaab ambalo mapema mwaka huu lilidai kuchukua udhibiti wa maeneo mengi katikati mwa nchi hiyo.