Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Pwani

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewapongeza wafugaji wa Kijiji cha Mpelumbe, Kata ya Gwata, Walayani Kibaha, mkoani Pwani kwa kujitolea kujenga bwawa la kunyweshea mifugo yao.

Waziri Ulega ametoa pongezi hizo hivi karibuni wakati alipowatembelea kuona juhudi wanazozifanya ambazo moja kwa moja zinaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya mifugo ili iwe na mchango mkubwa kwa taifa na mtu mmoja mmoja.

“Nawapongezeni sana, na nitakwenda kumjulisha Mhe. Rais kuhusu jitihada zenu hizi, kwa kweli mmefanya kazi nzuri sana na sisi wizara tunakwenda kuwaweka katika mipango yetu kuanzia mwezi wa 12 hadi wa kwanza mwakani tutawapatia kiasi cha Tsh. Milioni 50 ili ziwasaidie kuboresha bwawa hili mliloanza wenyewe kulitengeneza”, amesema

Aidha, Waziri Ulega alitumia nafasi hiyo pia kuwaelimisha juu ya Kampeni ya TUTUNZANE iliyozinduliwa na Mhe. Rais Samia mkoani Morogoro inayohamasisha ufugaji wa kisasa ikiwemo kulima malisho, kuchimba mabwawa na kutunza mazingira.

Halikadhalika aliwahimiza wafugaji hao kuwa na maeneo yao kwa ajili ya kulima malisho aina ya Juncao kwa ajili ya mifugo yao huku akiwakabidhi mbegu aina ya rhodes ili wapande katika maeneo yao.

Sambamba na hilo,pia, Waziri Ulega amempongeza Mfugaji wa Kijiji cha Gumba, Kata ya Gwata, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, Bw. Muhammadi Ragwa kwa jitihada kubwa aliyoifanya ya kuacha ufugaji wa asili na kufanya ufugaji wa kisasa wa kunenepesha mifugo ambao umemuwezesha kupiga hatua kubwa.

Waziri Ulega ametoa pongezi hizo alipomtembelea hivi karibuni mfugaji huyo katika eneo lake la ufugaji na kujionea maendeleo mbalimbali aliyoyafanya ikiwemo kujenga bwawa la kunyweshea mifugo yake, kujenga maghala ya kuhifadhia chakula cha mifugo na mashine ya kuchakata chakula cha mifugo yake.

Waziri Ulega amempongeza kwa hatua kubwa hiyo kwa kuwa anachokifanya ndio muelekeo ambao Serikali ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inataka wafugaji kote nchini kuuchukua, inahimiza wafugaji kubadilika kutoka katika ufugaji wa asili na kufanya ufugaji wa kisasa ikiwemo kuwa na maeneo yao ya kufugia.

Kufuatia maendeleo makubwa aliyoyaona kwa mfugaji huyo, Waziri Ulega amempatia mbegu za malisho na pia amewaelekeza wataalam kutoka wizarani kwake kuhakikisha wanajenga josho katika kijiji hicho ambalo litasimamiwa na Bw. Muhammadi kwa niaba ya wafugaji wote ikiwa ni kama motisha kwa mfugaji huyo na wengine pia.

“Ile mipango mizuri ya Rais, Mhe. Dkt. Samia ya kuboresha sekta ya mifugo inapaswa ielekezwe katika maeneo kama haya ya wafugaji waliopiga hatua kama Muhammadi kwa sababu inakuwa katika mikono salama”, amesema.

Akitoa taarifa fupi ya historia ya ufugaji wake, Bw.Muhammadi amesema yeye kiasili amezaliwa kwenye familia ya kifugaji na alirithi mtindo wa ufugaji kutoka kwa wazee wake ambao ni wa kuhamahama kutafuta maji na malisho.

Baada ya kupata changamoto nyingi zilizotokana na ufugaji wa kuhamahama ikiwemo magonjwa kwa mifugo aliamua kuacha mfumo huo na kuanza ufugaji wa kisasa wa kunenepesha mifugo ambao anasema umempatia manufaa makubwa ikiwemo kuwa na makazi ya kudumu ya familia yake na mifugo yake, kujenga miundombinu ya kufugia mifugo ikiwemo lambo la kunyweshea mifugo, maghala ya kuhifadhia chakula cha mifugo na mashine ya kuchakata chakula cha mifugo.