Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Iringa
WADAU wa mnyororo wa thamani katika sekta ndogo ya kuku wameonesha kuridhishwa na mafunzo ya ufugaji kuku kisasa yanayotolewa Kituo cha SilverLands Tanzania Limited (T-PEC).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kuku wameelezea namna sekta hiyo inavyochangia katika kuzalisha ajira sambamba na kutoa mchango chanya katika kukuza uchumi wa Taifa.
Wafugaji hao wamesema mafunzo hayo yataenda kutatua changamoto zinazoikabili tasnia hiyo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ujuzi na utaalam wa ufugaji.
Michael Nyagawa ambaye ni mfugaji mdogo wa kuku mkoani Njombe na mnufaika wa mafunzo hayo mbali ya kukipongeza kituo hiko ambacho ni miongoni wa wabia wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji nchini.
Kwa upande wake Ofisa Mwandamizi wa T-PEC, Alice Tendega amesema kituo hiko cha mafunzo kilianzishwa mwaka 2016 lengo likiwa ni kutoa mafunzo ya kuku kwa kina na kwa muda mfupi ili kuwainua wafugaji wadogo wadogo na mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Hadi sasa zaidi ya wanafunzi 3,500 wamepatiwa mafunzo katika fani tatu, ufugaji bora wa kuku wa nyama, ufugaji bora wa kuku wa mayai na namna bora ya ufugaji na uzalishaji wa kuku kwa ujumla.
Tunaendelea kutoa mafunzo haya kila mwaka, na hata kuongeza vituo vingine kulingana na uhitaji.” Alibainisha Tendega na kuongeza kuwa lengo lao ni kuzalisha vifaranga vya kutosha kwa ajili ya soko la ndani na la nje ya nchi sambamba na uzalishaji wa chakula bora cha kuku.
Naye Meneja wa SAGCOT Kongani ya Ihemi, Khalid Mgaramo amesema bado wafugaji wengi wa kuku wanafuga chini ya kiwango kutokana na ukosefu wa ujuzi na utaalam wa jinsi ya kufuga, mitaji ya uwekezaji, uzalishaji wa chakula bora cha kuku, gharama kubwa za chakula sambamba na viwanda vinavyochakata kuku na mazao yatokanayo na kuku.
“Kumekuwa na changamoto nyingi katika tasnia hii ya kuku sambamba na fursa ambazo hazijaweza kufikiwa ndio maana SAGCOT imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wabia wa maendeleo ikiwemo T-PEC yenye kituo cha utoaji mafunzo ya ufugaji wa kisasa wa kuku.
“SAGCOT inafanya kila jitihada kuhakikisha hayo mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yanawafikia wakulima, wafugaji na kuhakikisha yanatoa mchango stahiki katika kuwainua kiuchumi katika kongani ya Ihemi.” amesema Mgaramo.
Mgaramo amebainisha kuwa ubia mkakati wa kuku unaundwa na wabia 22 wakiwemo wafugaji wadogo wa kuku, sekta binafsi kama vile Silverlands, AKM Glitters, Tanfeed (Moragg), NMB, CRDB, Agrovets; sekta ya umma Asasi za Wanachama wa Sekta ya Kuku kama vile Tanzania Animal Feed Manufacturer Association (TAFMA), Tanzania Poultry Breeders Association, Poultry Layers Association.
Kwa mujibu wa takwimu za FAOSTAT, za mwaka 2017, Tanzania ilichakata takriban tani 104,000 za nyama ya kuku huku kiwango cha ukuaji wa jumla wa miaka 5 (CAGR) wa asilimia 4.
SAGCOT imekuwa chachu na muhamasishaji mkubwa katika kuwaunganisha wakulima wadogo, wafugaji wadogo na kuwajengea uwezo ili kuweza kutoa mchango stahiki katika sekta za kilimo mifugo na uvuvi kwa kuwafanya wadau kuingia katika kilimo biashara na kuweza kujenga uchumi himilivu na endelevu.