*Wanuia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Jamii ya wafugaji wa Kimaasai katika wilaya za Longido, Ngorongoro, Monduli (Arusha), na Simanjiro wanakabiliwa na wakati mgumu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea.
Kwa miaka ya karibuni, hali ya tabianchi imekuwa mbaya. Kuna wakati mvua zinakosekana, na wakati mwingine zinanyesha kwa wingi. Miongoni mwa matatizo makubwa yanayotishia uhai wa mifugo na wafugaji wenyewe ni kupungua kwa majani yanayofaa kwa mifugo.
Kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuwanusuru wafugaji na mifugo yao. Mwaka 2000 mmoja wa wafugaji hao kutoka Shirika la Haki Kazi, Alais Morindat, alianzisha mradi kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuwasaidia wafugaji wenzake ili wakabiliane na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Alianzisha mkakati huo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Longido na hatimaye kuzishirikisha halmashauri zilizotajwa hapo juu. Miongoni mwa kazi kubwa ni kuwapa semina za mafunzo viongozi wa mila, jinsi ya kutunza ardhi, thamani ya ardhi, jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuhamisha mifugo wakati wa kiangazi na masika.
Pia mafunzo yanalenga kuzuia kilimo kisichozingatia kanuni za utunzaji ardhi, na ujenzi holela wa maboma. Viongozi wamekuwa wakisambaza elimu hiyo kwa wafugaji.
Morindat anajivunia mafanikio makubwa kutokana na mradi huo. Hata hivyo, amekuwa akiendelea kufanya mikutano kwa wazee wa mila na viongozi wa halmashauri hizo.
Kwenye mikutano hiyo, pamoja na kujadili namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pia hujadili masuala mbalimbali ya kudumisha mila na utamaduni, kujenga mshikamano, na kuzingatia suala la elimu kwa watoto wa jamii ya wafugaji.
“Kipindi cha mwaka 2009/2010 wafugaji walipoteza asilimia 70 ya mifugo yao ambayo ilikufa kwa kukosa malisho. Hatutaki jambo hili lijirudie, ndiyo maana tunatoa mafunzo kwa wafugaji ili waweze kupambana na ukame, uhaba wa chakula pamoja na majanga mengine kama mafuriko,” anasema Morindat.
Anaongeza; “Tunatoa elimu kwa viongozi wa mila wa jamii ya Kimaasai ili waweze kutoa elimu hii kwa jamii zao kwa sababu hawa viongozi wana ushawishi mkubwa kwa wananchi wanaowaongoza. Hili litasaidia kuinua uelewa wa wafugaji juu ya mabadiliko hayo na namna ya kukabiliana nayo.”
Hivi karibuni wafugaji kutoka wilaya hizo waliendelea kupatiwa elimu hiyo iliyoratibiwa na Morindat, lengo kuu likiwa ni kujadili faida za kuwa na idadi ya mifugo wanayoweza kuimudu kuitunza na wakati huo huo kuyalinda mazingira kwa nyakati za kiangazi na za masika.
Mbunge wa Longido, Michael Laizer, anasema kuwa mafunzo hayo ni muhimu mno kwani yanawakutanisha wafugaji kutoka wilaya za wafugaji katika mikoa ya Arusha, na Wilaya ya Simanjiro. Anasema hatua hiyo inawafanya wawe kitu kimoja katika kutafuta mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwa na mifugo yenye tija.
Anasema kuwa katika wilaya hizo kumekuwapo mabadiliko, tofauti na miaka iliyopita kwani hivi sasa ardhi imezidi kuwa finyu kutokana na watu kujenga makazi na kufanya shughuli za kibiashara. Kwa mtazamo wa mbunge huyo, hali hiyo inasababisha maisha ya wafugaji yawe ya shaka.
“Kuna tatizo la matumizi mabaya ya ardhi, unakuta ardhi ya wafugaji inatumika kwa shughuli za kilimo, makazi au uwekezaji; jambo ambalo linazua migogoro. Wakati umefika sasa wa kuhamasisha mpango wa matumizi bora ya ardhi,” anasema.
Laizer anawataka wafugaji wawe na subira pale kunapojitokeza mabadiliko ya tabianchi. Anasema wanapohamisha mifugo kwenda kwenye nyasi, wanapokutana na wenzao wasianzishe vita na umwagaji damu, na waache aina zote za ubaguzi.
‘’Jamani nawaomba tudumishe umoja wetu, tusiruhusu umwagaji damu na uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya ardhi kwani najua bado suala la ardhi ni tatizo, nawaomba mtakapobaini tatizo hilo tukae chini tujadili ni jinsi gani ya kulitatua,’’ anasema Lekule.
Anasisitiza elimu miongoni mwa jamii ya wafugaji wenyewe pamoja na watoto wao.
“Kupitia elimu kuna uwezekano wa kujua mambo mengi na hata jinsi ya kuchukua hatua katika kutetea haki zao,” anasema.
Anaongeza kuwa wazazi wana wajibu mkubwa wa kuwaelimisha watoto jinsi ya kudumisha mila zao, kwani imebainika kuwa wapo watoto ambao wakienda kwende masomo hupoteza utamaduni wao kwa kuvaa nguo zisizo za kimaadili na wengine kulowea mijini.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, James ole Millya, akielezea mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wafugaji wilaya hiyo na wenzao wa Arusha, anasema unasababishwa na ukosefu wa mipaka inayoeleweka.
“Sisi hapa Longido tunao mgogoro kati ya wafugaji wa hapa na wafugaji wa Arusha kwani wamekuwa wakiingiliana mipaka kwa malisho. Hivyo, Serikali inapaswa kulifanyia kazi ili wananchi watambue mipaka na kumaliza migogoro,” anasema Millya.
Anawashauri wafugaji kuwa pamoja na ufugaji, wajikite kuwekeza zaidi katika kufanya kazi nyingine zenye kuwapa tija badala ya kujielekeza kwenye mifugo tu.
Amewataka wafugaji waendelee kuipatia mifugo yao chanjo sahihi kutoka Shirika la Chanjo la Vetagro ambayo imeonekana kuwa na faida kubwa kwa afya za mifugo. Mkuu huyo wa Wilaya amewaonya wote wanaofanya utapeli kwa kuwahadaa wafugaji. Imebainika kuwa wafugaji wanadanganywa na kupatiwa chanzo feki, jambo ambalo limesababisha wengi kupoteza mifugo.
Kwa upande wao, viongozi wa mila kutoka wilaya hizo wamesema kuwa ardhi za malisho za jamii hizo zimekuwa zikichukuliwa na kubadilishwa matumizi.
Kwa sababu hiyo, wamesema wanakosa maeneo ya kutosha kwa ajili ya malisho. Wameiomba Serikali ilitafutie ufumbuzi ili kuepuka migogoro.
Mbirias Oleringa kutoka Kijiji cha Endulen wilayani Ngorongoro, na Ngaya Samuria kutoka Wilaya ya Longido, ni miongoni mwa viongozi wa kimila waliohudhuria semina hiyo.
Wanaiomba Serikali iangalie namna ya kulinda ardhi za malisho ili kulinda ustawi wa jamii zao ambazo zinategemea zaidi ufugaji kuendesha maisha yao.
Kwa pamoja, washiriki wa semina hizo waliweka mikakati ya kulinda ardhi na kuhakikisha hawaiuzi holela ili iweze kusaidia vizazi vyao vijavyo.