Fitina na pekepeke ni tabia zinazofanana, zinazoelewana na zina nguvu ya kuvunja mipango ya maendeleo iliyopo na kubomoa mafanikio yaliyopatikana kwa gharama kubwa ya mapenzi, hisani, maarifa, nguvu, utu na umoja.

Tabia hizi hazizuki mithili ya uyoga msituni, bali huandaliwa na mtu au watu wakati wa malezi na makuzi ya mtoto na hukomaa ujanani. Ni tabia zenye mazoea ya kufanya jambo fulani ndani ya utaratibu na desturi iliyokubalika.

Mtu au familia inayopenda fitina au upekepeke na kuamini hiyo ndiyo tabia nzuri, ukweli wanafanya uadui na kusababisha watu kutoelewana miongoni mwao. Katika mazingira kama haya wapenda utulivu na amani huwa shakani kwa sababu nyoyo zao zinajaa chuki na wasiwasi.

Ukiiangalia fitina katika umbo lake utaona imerembwa na chuki, uchongezi, chokochoko, uhasama na uchonganishi. Na ukiiangalia pekepeke katika umbo lake nayo imepambwa na chokochoko, uchongezi, uchonganishi na usengenyaji. Tabia hizi ni hatari kwa jamii.

Tabia hizi ni kama sumu yenye uwezo wa kudhuru au kuua inapoingia akilini na mwilini mwa mtu. Mfitini au mpekepeke hutumia muda wake kusambaza sumu na kuhatarisha maisha ya ndugu, rafiki, jamaa hata mpenzi wake. Akisha kuumiza, hutafuta huruma kwa wananchi aonekane hana baya alilotenda.

Mfitini au mpekepeke hufanya mambo matatu ili uweze kumwamini na apate nafasi ya kukudhuru. Mosi, hujifanya mcheshi na mwingi wa tabasamu. Pili, hujenga hali ya upendo, hisani na utii. Tatu, hujitolea kusuluhisha mambo na kutetea upatikanaji wa haki.

Usiku na mchana mpekepeke hufanya kila hila kuchongea watu, akiwa na shabaha anayoilenga ya kuwatenga na kuwaweka mbalimbali. Anaifanya kazi hiyo majumbani, michezoni na kazini. Ukweli hatatulia iwapo hajafanikisha malengo yake.

Mfitini hayuko mbali na wewe. Ana sura jamili na maneno matamu. Asemayo usiyashike. Ni mzandiki na sakubimbi. Atakufanyia ya hisani na wewe huna wasiwasi naye. Utampa kila kitu na siri yako kumwambia, bado yeye hataridhika mpaka akugawe na akutose.

Leo, wafitini na wapekepeke wameingia dimba la mambo ya haki na siasa na kutumia demokrasia na haki za binadamu kama turufu ya utetezi kwa watu wanaoona hawapati haki na demokrasia ya kweli. Kumbe dimba lenyewe lina wazandiki wanaojitambua na watetezi wakubwa wa masilahi ya mabara yao. Wanayumbisha nchi zinazoendelea zisipate maendeleo.

Wale wa kutoka Bara la Afrika eti wanashindwa kupima uzito wa haki na dhuluma katika mizani. Eti hawawezi kufafanua na kuona ukweli wa miradi ya maendeleo inayoshughulikiwa na serikali zao. Wanachoona ni demokrasia tu, tena kwa macho yenye makengeza.

Ndani dimbani wamo viongozi wa jamii na wasomi waliobobea katika taaluma zao: kama vile siasa, dini, diplomasia, utawala, sheria na uchumi. Cha kushangaza Waafrika hawa wanajidhalilisha utu wao na elimu zao. Wanajiumbua bila ya kujijua mbele ya wenzao wa mabara mengine. Hao wenzao wanawasikiliza na wanawatazama. Akili kichwani mwao.

Waafrika hawa wanashindana na kukinzana katika kutafuta fasiri, sababu, umuhimu na fasili ya elimu, demokrasia, uongozi na utawala bora. Huku wakitetea mali za Afrika ziporwe zaidi na wajanja. Na wao wakipachikana ujinga. Wanasahau msemo wa wahenga usemao: “Wajinga ndio waliwao.”

Hii ina maana kwamba ukizubaa au kudakia kufanya mambo bila kuyachambua vema utaishia kunyonywa au kudhulumiwa. Viongozi na wasomi wetu wa Afrika mnatupeleka wapi? Hivi ile dhamira ya viongozi waliopigania kupata uhuru wa nchi zetu na ukombozi wetu Waafrika iko wapi?

Waafrika wenzetu mnaokubali na mnaopenda tabia ya fitina na upekepeke mmepungukiwa nini katika maarifa yenu? Elimu ya kutosha mnayo, hata ng’ambo mmekwenda kuishi na mkarudi. Kipi bado cha ajabu kwenu? Kumbukeni, “Mtu kwao.” Watazameni wenzenu katika dimba wanavyolinda mali zao.