Na Isri Mohamed, JamhuriMedia
Wafanyabiashara wawili Raymond Hyera (25) na Riziki Mohamed (30) wamefariki dunia wakiwa kwa mganga wa tiba za asili, Mtila Ausi maarufu Shehe Mtila, baada ya kupewa maji ya kuwawezesha biashara zao kufanya vizuri.
Baada ya kunywa maji hayo, wafanyabiashara hao ambao ni wakazi wa Mkoa wa Ruvuma walilegea na kupoteza maisha kisha mganga huyo na wenzake wakawazika kimya kimya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amesema wafanyabiashara hao hawakuonekana tangu Julai 31, 2024, ambapo taarifa zao rasmi ziliripotiwa katika Kituo cha Polisi Songea mkoani Ruvuma, mnamo Agosti 3, mwaka huu.
“Baada ya uchunguzi na mahojiano, mganga na wenzake walikiri wafanyabiashara hao kufika nyumbani kwao wakiambatana na mfanyabiashara mwenzao aitwaye Amini Sanga kwa lengo la kupata dawa za kuwawezesha biashara zao kufanya vizuri zaidi, waliwanywesha maji ambayo yaliwafanya walegee na kupelekea kupoteza maisha, baada ya kufariki, waliwachukua na kwenda kuwazika katika pori la Mdinguli, kijji cha Mtangashari, Tunduru kisha kuchukua fedha walizokuwa nazo Tsh. milioni ishirini na kugawana”
“Septemba 3, 2024, Mtila Ausi na Omary Abdallah waliwaongoza Polisi hadi walipowazika wafanyabiashara hao, ufukuaji ulifanyika na miili ya Wafanyabiashara hao ilikutwa, uchunguzi unaendelea kukamilishwa ukiwepo wa kisayansi ili taratibu nyingine zifuate” amesema Misime.
Kwa sasa Jeshi la Polisi linawashikilia Mtila Ausi (Mganga wa kienyeji), Omary Abdallah na Amini Sanga, uchunguzi Zaidi na taratibu za kisheria vikiendelea.