Mwishoni mwa Februari, wakati nikisafiri kutoka Wilaya ya Mvomero kuelekea Kilombero, nilipofika mjini Morogoro, niliingia kwenye basi linalofanya safari kati ya Morogoro na Ifakara.
Nilikata tiketi katika basi hilo saa 9:30 alasiri, lakini ndani ya hilo basi nilikutana na abiria waliokata tiketi saa tatu asubuhi. Kila aliyekuwa anakata tiketi pale alikuwa akidanganya muda wa kuondoka kwa basi husika. Waliokata tiketi saa tatu asubuhi waliambiwa basi lingeondoka saa nne na mimi wakati ninakata tiketi saa 9:30 niliambiwa kuwa basi linaondoka saa 10:00 jioni.
Kilomita mbili baada ya kuondoka stendi kuu ya Morogoro saa 11 jioni; kondakta akatutangazia kwamba basi hilo halitaendelea na safari ya Ifakara kwa sababu abiria ni wachache. Akadai kuwa kutokana na uchache wa abiria tuliomo ‘haitawalipa’ kulipeleka basi huko.
Walichofanya wakakodi basi dogo na kutwambia tuingie humo. Kwa bahati mbaya sana idadi ya abiria tuliokuwa kwenye basi la awali ikawa kubwa kuliko viti vya hili basi dogo. Abiria wengi waliokosa viti wakalazimika kusimama wakati tiketi zao zilikuwa zinaonesha namba za viti kwa basi la awali.
Abiria tusio na makuu ndiyo tulioingia kwenye basi lile dogo, lakini kuna ambao ‘waliwasha moto’ kuhusu uhuni waliofanyiwa na wakakataa katakata kubadilishiwa gari. Nilisikia mmoja akisema maneno yafuatayo kwa hasira na ukali:
“Kama ingekuwa basi limeharibika ningekubali, lakini mnaleta uhuni wa kusema eti haitawalipa, kwani mnavyoomba leseni SUMATRA si mlijua kuna siku mtapata abiria na siku nyingine mtakosa? Imeandikwa wapi katika leseni ya kuwa abiria wakiwa wachache katika basi, safari iahirishwe? Nitakufa na ninyi ili niwafundishe adabu muache kutuonea. Mnadhani Watanzania wa siku hizi ndiyo wale wa zamani wa kuwapelekesha kama maboga?”
Baada ya kuona pamekuwa ‘pa moto’, wafanyakazi wa lile basi kubwa ilibidi wawavute pembeni wale ‘waliowasha moto’ na kuzungumza nao. Sielewi walifikia mwafaka gani lakini abiria wale walishikilia msimamo wa kutoingia kwenye basi dogo. Tuliondoka Morogoro saa moja kasorobo usiku huku abiria wote wakiwa wanalalamika.
Katika kiti nilichokaa ndani ya basi dogo, kulikuwa na mama ambaye baada ya kumsalimia alinieleza kuwa anaona sura yangu kama si ngeni kwake. Nilipomweleza kuwa huenda aliniona kwenye Gazeti la JAMHURI, alishtuka mno na kusema, “Hee, kumbe wewe ndiyo Sanga? Wawoo!”
“Kila wiki nazisoma makala zako.” Kisha akauliza kwa hisia kali, “Kwanini hujawapigia kelele hawa wahuni (wenye basi) wakati wewe ni mwandishi? Hivi unajua ungejitambulisha kwao na kuwapiga mkwara, wangeogopa sana na wasingefanya uhuni waliotufanyia?”
Niliendelea kuzungumza na yule mama, lakini kwa swali lake la hisia nilimjibu, “Wakati abiria wote mlikuwa mkipiga kelele na kulilaani hili basi, mimi fikra zangu zilikuwa kwa mmiliki wa hili basi. Huko aliko nina uhakika hafahamu kuwa vijana wake wanamuharibia biashara. Katika masuala kama haya huwa ninafunga kinywa changu na kusali nikimwombea mjasiriamali mwenye biashara husika.
“Kwa sababu ninafahamu kama mwenye basi hili angekuwapo hapa asingetumia lugha ya kibabe, asingeonesha ukaidi na asingekubali kuona jina la basi lake linachafuliwa.” Nikaendelea kumweleza, “Siwezi kutumia uwezo wangu wa kuandika kwa ajili ya kuchafua biashara ama kampuni za wengine hata kama wamekosea vipi.”
“Ninaamini kuwa kuwalinda wajasiriamali wenzangu ni aidha kuandika mema yao, ama kukaa kimya kwa makosa yao. Msimamo wa kukaa kimya inapotokea uvurundaji kama wa lile basi lililotushusha, unaweza kuonekana ni kutokuwajibika; lakini sikufichi mama yangu; kabla sijaandika chochote kuhusu biashara ama kampuni yoyote; huwa kwanza najiuliza hivi:
“Je, hiki ninachoandika kama ningekuwa ni mimi, biashara yangu ama kampuni yangu inaandikwa hivi, ningejisikiaje? Majibu ya swali hili ndiyo yanayotengeneza makala zangu zote za biashara na uchumi unazozisoma. Nafahamu kuwa viatu vya ujasiriamali ni vizito; mtu anaweza kukurupuka kukusema vibaya pasipo kufahamu ikiwa wewe unahusika moja kwa moja ama la. Nipo makini sana na kalamu yangu.”
Nilishuka Kilombero na yule mama aliendelea na safari ya Ifakara, lakini safari ile ilinifanya kutafakari na kuwahurumia wajasiriamali wengi. Nikaikumbuka kampuni nyingine ya mabasi ambayo siku hizi siioni tena. Wafanyakazi wa kampuni ile enzi zile ikiwa kileleni, iking’aa walikuwa na nyodo kupindukia.
Siku moja nilikuwa na ndugu yangu mfanyabiashara aliyepo Tunduma na tukafika katika ofisi zao kukata tiketi za kwenda Dar es Salaam. Tukaambiwa tiketi zimeisha.
Baadaye nilikuja kuambiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi yale walikuwa na mtindo wa kumtazama mtu mavazi na mwonekano wake kabla ya kumpa tiketi. Ukivaa rafurafu hupewi tiketi! Kitendo hiki kilisababisha watu wengi kuhisi wanadharauliwa na hivyo wakaanza kusambaza maneno mabaya kuhusu mabasi yale.
Kilichotokea! Kuna wakati basi la watu sabini lilikuwa likiondoka stendi likiwa na abiria saba tu! Katika mazingira kama haya ambayo unaendesha kampuni ama biashara kwa hasara haiwezekani ukastahimili katika soko.
Kwenye ujasiriamali wafanyakazi ni pasua kichwa kweli kweli. Uzembe, ujinga na upumbavu wa wafanyakazi wengi umesababisha wajasiriamali wengi kutoendelea, kuyumba ama kufilisika kabisa.
Unaweza kutafuta mtaji kwa jasho jingi na ukaanzisha duka, unamweka mfanyakazi auze hapo lakini wengi hawawi waaminifu. Kama ni duka anaweza kuanza kufuja mali ama kuiba. Shemeji zangu Wahehe huwa wana msemo huu, “Mtu anakuja kuomba kazi akiwa ananyenyekea na kuweka mikono nyuma, lakini akishapata anaanza kuiweka mbele na anaweza kukufokea hata wewe bosi wake!”
Kwa hawa wafanyakazi wazembe, jambo baya kuliko yote ni pale inapotokea hawaheshimu, kuwathamini wala kuwajali wateja. Wafanyakazi ‘vimeo’ huwa hawana uchungu na biashara yako, iwe unauza ama huuzi, iwe unapata hasara ama faida, hawajali! Wanachojali wao ni mshahara wao unaowalipa tu!
Usiombe biashara yako ikaingia kwenye tanuri la kusemwa vibya, utajuta. Mathalani, lile basi lililotufanyia uhuni pale Morogoro kila abiria alikuwa akijiapiza kuwa hatalipanda tena na wengine wakaweka nadhiri ya kuwajulisha ndugu, marafiki na jamaa zao kuhusu ubaya wa basi lile kwamba halifai kupandwa. Unatarajia nini kwa majaaliwa ya kampuni ile kama si kushuhudia kupungua kwa abiria wanaopanda mabasi yake?
Kama hili tumeshalifahamu ya kuwa wajasiriamali tuna hatari ya wafanyakazi wazembe kutufilisi, je, tufanyaje? Kulalamika haitatusaidia! Kusema tumwachie Mungu ni uzembe! Kuendelea kuvumilia ni kujirudisha nyuma! Tupende ama tusipende wajasiriamali tunalazimika kuchukua hatua za makusudi za kutuwezesha kuwa na wafanyakazi bora watakaojenga biashara pamoja nasi na si wale wanaobomoa.
Nilichogundua ni kuwa wajasiriamali wengi hatujui namna ya kuajiri na kuwafundisha wafanyakazi. Wengi wetu huwa tunazoazoa bora wafanyakazi. Kinachotuponza ni kupenda vya dezo. Tunapenda kuwabeba ndugu zetu wa karibu bila kujali ubora wao, ilimradi tu tuwe tunawalipa kidogo ama kutowalipa kabisa.
Fikiria wewe unamiliki basi ama duka, halafu unamuweka ndugu yako asiye na uwezo wala vigezo vya kufanya kazi kwa ustadi, unatarajia nini? Sana sana ataanza kujitukuza na kujiona yeye ndiye kila kitu katika biashara husika. Hata majigambo yake kwa wengine itakuwa ni cheo chake cha undugu kwako.
Inabidi ufike wakati mjasiriamali unapopiga hesabu za biashara yako halafu unatafuta wafanyakazi wa kiwango na vigezo kuhimili biashara yako. Hakuna maana ya kusema eti unabana matumizi ya kuwalipa watu mishahara ilhali unaelekea kufilisika.
Nimewahi kueleza namna ya kuwatendea wafanyakazi tunaowaajiri katika makala iliyokuwa na kichwa, “Mjasiriamali na sayansi ya kuajiri.” Mara zote nimekuwa nikiwatahadharisha wafanyabiashara na wajasiriamali kuepuka mtego wa kuwa wadhulumaji kwa wafanyakazi wao.
Mara zote mfanyakazi unayemwajiri katika biashara zako huwa anafahamu kiwango cha faida unayozalisha. Kitendo cha wewe kumlipa kiduchu kinazalisha sumu mbaya sana. Matokeo yake ni kukuibia, kupoteza morali wa kazi na hatimaye kuwavuruga wateja wako.
Nihitimishe kwa kuwasihi wajasiriamali kuwa makini tunapoajiri watu katika biashara zetu, kwa sababu wengine wanaweza kugeuka mawakala wa shetani kutufilisi. Niwatakie kila la heri katika mapambano ya kiujasiriamali
[email protected], 0719 127 901