Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAFANYAKAZI wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wametoa msaada wa vifaa tiba kwa hospitali ya Wilaya ya Kigamboni na hospitali ya Rufaa ya Temeke vyenye thamani ya shilingi milioni 49 ikiwa ni sehemu ya kusherehekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Akizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Rasilimali Watu wa Mamlaka hiyo, Bi Mwajuma Konga kwa niaba ya wanawake hao amesema kuwa hiyo ni kawaida ya TPA kusherehekea siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa misaada mbalimbali sehemu zenye uhitaji makubwa.
“Leo tumeleta vifaa tiba mbalimbali vya aina 15 kwa ajili ya hospitali hizi mbili za Wilaya ya Kigamboni pamoja na Temeke ambapo miongoni mwa vifaa hivyo ni pamoja na mashine ya mionzi (X-ray) ,vitanda vya wagonjwa, machela ya kubebea wagonjwa na sabuni za unga na za maji,” alisema Bi. Konga.

Vifaa vingine ambavyo vilikabidhiwa ni pamoja na mashine ya kupima kiasi cha oksijeni kwenye damu, mashine ya kutoa joto kwa watoto wachanga waliotoka kuzaliwa na bambino za watoto na za akina mama waliootoka kujifungua.
“Hii yote ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza malengo endelevu (SDG’s) kwa upande wa sekta ya afya ,” alisema Bi Konga.
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Hospitali ya Kigamboni, Mkuu wa wilaya hiyo, Bi Halima Bulembo mbali ya kuwashukuru wafanyakazi wanawake wa TPA, alisema vifaa hivyo vitatumika katika kazi iliyokusudiwa, ili Watanzania wengi wakanufaike hususani wakazi wa kigamboni kwa kupata huduma bora za matibabu.
“Siku ya Wanawake Duniani ina malengo ya kutambua mafanikio yao na kuwasaidia wale wenye uhitaji katika jamii na ndiyo maana wanawake wa TPA wameamua kuja kuwainua wanawake wa Kigamboni” alisema Bi Bulembo.

Aidha, Bi Bulembo alimtaka Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt Lucas Ngamtwa kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kufanyiwa marekebisho punde yanapohitajika ili vidumu kwa muda mrefu na vitumike kuwasaidia wanawake na watoto wa wilayani humo.
Naye kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dkt AnnaMary Rugakiza aliwashukuru wafanyakazi wanawake wa mamlaka hiyo, kwa msaada wa vifaa hivyo akisisitiza kuwa vitatumika katika kuwasaidia Watanzania hususani wakazi wa wilaya ya Temeke hasa wanawake na watoto.

“Vifaa hivi vimekuja muda muafaka kwani vitaongeza ufanisi wa matibabu kwa wagonjwa wanaofika hospitali hapa kupata huduma na hivyo kupunguza vifo vya mama na mtoto” alisema, Dkt Rugakiza.
Hata hivyo, Dkt Rugakiza aliwaomba wadau wengine kuiga mfano wa TPA kusaidia watu wenye uhitaji hususani wanawake wanaojifungua kwani kuna baadhi yao hawana uwezo wa kulipia matibabu kutokana na sababu mbalimbali.
Mamlaka hiyo imekuwa na utaratibu wa kusaidia taasisi mbalimbali kama sehemu ya kurudisha kwa jamii (CSR) katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Mwaka jana, TPA iligharamia ukarabati wa jengo la hospitalli ya Temeke la wagonjwa wa figo pamoja na kununua vifaa tiba ambavyo viligharimu zaidi ya shilingi milioni 450 na kutoa kadi za bima ya afya 500 kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika hospitali tofauti tofauti katika Mkoa wa Dar es Salaam.