Wafanyakazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wametakiwa kufanya kazi kwa ueledi na kuzingatia maadili huku wakiepuka ubaguzi wa aina yoyote katika utekeleaji wa majukumu yao.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Aprili 27, 2023 na Katibu Mkuu Ikulu, Mululi Mahendeka alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa wafanyakazi hao unaofanyika kwa siku mbili Bunju, Dar es Salaam,

Mahendeka amesema kwa moja ya changamoto zinazoukabili mfuko huo ni baadhi ya wanasiasa kupotosha lengo halisi ya Mfuko na kuhusisha kazi zake na itikadi za kisiasa na ukabila.

Amesema kwa kuwa wako wanasiasa, kwa malengo wanayoyajua wao, wamekuwa wakieneza habari potofu kuwa kazi wa Mfuko zinahusiana na ikitadi za kisiasa, ni jukumu la wafanyakazi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa kufuata taratibu zilizopo na hivyo kuepuka ubaguzi wa itikadi za kisiasa, kidini na kikabila.

Katibu Mkuu Ikulu, Mululi Mahendeka

“TASAF ni taasisi ya Serikali na hivyo inafuata taratibu za kiserikali. Hakikisheni mnafanya kazi kwa bidi ueledi na maarifa. Fuateni miongozo ya Serikali ikiwemo kutunza siri za Serikali,” amesema.

Ameitaka menejienti ya TASAF kutambua majukumu yake na kuyatekeleza kwa ukamilifu , kutembelea miradi katika mamlaka za utekelezaji, kuzungumza na walengwa na kujua changamoto zao ii iwe rahisi kuzitatua. “Fanyeni kazi sawasawa na jina la mfuko na muweke kipaumbele kwa maendeleo ya jamii,” amesasa.

Amewataka kwafanyakazi kutunza rasilimali za taasisi ikiwemo magari, kompyuta. mifumo na kompyuta mpakato na kufanya kazi zilizopo na kulingana na sera kukidhi matarajio ya Serikali kwa mfuko huo

“Mambo ya uendeshaji wa miradi yameainishwa vizuri katika andiko la mradi lililosainiwa kati ya Serikali na wadau wa maendeleo. Someni andiko la mradi kwa makini ili mjue mnachotarajiwa kufanya,” amesema.

Akitoa shukurani kwa Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya TASAF, Peter Ilomo amesema Kamati yake na Menejimenti inazingatia maelekezo hayo na wakati wa mkutano kama huo watatoa mrejeshokuhusu utekelezaji wa maelekezo.