Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

ZAIDI ya Wafanyabiashara ndogo ndogo 137 wanaouza mbogamboga na matunda katika soko la Kilombero jijini Arusha wameondokana na adha ya kuuza bidhaa zao chini pamoja na kunyeshewa na mvua baada ya kuboreshewa mazingira kwa kujengewa vizimba vipya kwa ajili ya kufanyia biashara zao .

Aidha vizimba hivyo 137 vimejengwa kwa ufadhili wa Shirika linalojishughulisha na mambo ya usalama wa chakula la RIKOLTO na World Vegetable Centre,kwa ufadhili wa CIMMYT kupitia mradi wa AID -na Belgian Development Coorporation (DGD).

Akizungumza na wafanyabiashara hao Meya wa jiji la Arusha Maxmilian Iranghe wakati wa uzinduzi wa vizimba hivyo eneo la Garden –Soko la Kilombero amewataka wafanyabiashara hao kuvitunza ili viweze kuwa endelevu kwa ajili ya wengine kuweza kutumia kwa baadaye.

“Naombeni sana mhakikishe mnatunza vizimba hivi sambamba na kutunza mazingira ya soko hili ili kuwepo kwa usalama wa chakula kuanzia shambani hadi nyumbani.” amesema Meya .

Aidha ameongeza kuwa, endapo watatunza vizuri vizimba hivyo vizuri itakuwa ni chachu ya kuvutia wafadhili wengine kuja kuboresha eneo hilo la soko kwani bado uhitaji wa kuboreshewa mazingira ni mkubwa sana ikilinganishwa na mahitaji ya wafanyabiashara waliopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa programme ya Rikolto East Afrika ,Kain Mvanda amesema kuwa ,Kain Mvanda amesema kuwa mradi wa vizimba hivyo ndani ya Soko la Kilombero
ulianza mwezi agosti 2024,na umemalizika rasmi mwezi machi 2025 .

Amesema kuwa,waliunda kamati ya usalama wa chakula jijini Arusha ambapo wakaona kuna haja ya kuwajengea soko kutokana na mazingira yasiyorafiki wanayouzia kwani walikuwa wanauzia bidhaa zao chini kitendo ambacho sio afya kwa walaji.

“mfumo huo wa usalama wa chakula ni agenda mtambuka inayoendeshwa kwa wao kutoa ufadhili kwenye mnyororo wa thamani ya mazao ya mbogamboga na matunda ili mkulima aboreshe vipato na uzalishaji wenye tija.”amesema .

Awali Mkuu wa Soko hilo Jeremiah Katemi amesema kuwa,amefurahishwa sana na shirika hilo la Rikolto kwa kuwajengea soko hilo kwani kilikuwa ni kilio cha kila.siku hasa kipindi cha mvua wafanyabiashara walikuwa wanauzia kwenye matope jambo ambalo sio afya kwa walaji.

“Tunaomba wafadhili wengine wajitokeze kwa wingi kuja kutujengea soko letu kwani mahitaji bado makubwa kutokana na kuwa kuna wafanyabiashara zaidi ya 3,000 hapa kilombero ambao hawapo kwenye maeneo rasmi .”amesema Katemi.

Diwani wa kata hiyo ya Levolosi Augustine Matemu amesema kuwa kitendo hicho kilichofanywa na shirika hilo ni cha kuigwa na mashirika mengine kwani kinasaidia afya za walaji kuwa salama tofauti na hapo awali.

Aidha amesema kuwa, soko hilo la Kilombero linakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu hali inayowafanya wafanyabiashara wengi kuendelea kuuzia bidhaa zao chini na kupelekea kuwepo kwa tope hasa kipindi cha mvua.

“Tunaomba wafadhili zaidi kujitokeza kusaidia uboreshaji wa soko hilo lengo ni kuongeza usalama wa chakula kuanzia shambani hadi nyumbani kwa mlaji na hatimaye wafanyabiashara kuweza kufanya biashara zao katika hali ya usafi na usalama zaidi “amesema Matemu.

Naye Mwakilishi kutoka Shirika la utafiti wa ngano na mahindi (CIMMYT ) amewataka wafanyabiasha hao kuwa wao ni mabalozi wa kesho iliyobora kwa wenzao kuwa mfano mzuri wa utunzaji na kuboresha vipato vya ili kuvutia wenzao kupata sehemu itakayoboreshwa.

Tuendelee kuboresha mazingira ya masoko yetu ili kuweka vizuri suala zima la usalama wa chakula kuanzia kwa mkulima hadi mlaji nyumbani.