Watanzania 235 wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya nje ya nchi, wamekamatwa katika kipindi cha mwaka 2008 hadi mwaka 2012.
Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, Christopher Shekiondo, amebainisha hayo katika mazungumzo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.
Shekiondo amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika nchi mbalimbali zikiwamo Brazil, Kenya, China, Pakistan, Falme za Kiarabu na Mauritius. Amesema nchi yetu bado inakabiliwa na tatizo la dawa za kulevya, hasa bangi na mirungi ambazo hulimwa hapa nchini.
“Dawa nyingine kama heroin na cocaine huingizwa kwa wingi nchini, Serikali imefanya jitihada za kupambana na tatizo hili ikiwa ni pamoja na kuzikamata, kuziteketeza, kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa na kutoa elimu kwa umma,” amesema.
Kamishna huyo amesema washitakiwa wanne wameshahukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kilo nne za heroin katika mikoa ya Mtwara na Tanga. Kilo 97 za heroin ziliteketezwa katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na Lindi kati ya mwaka 2010 na 2012.
Ameongeza kuwa washtakiwa wengine watano wamehukumiwa miaka 25 baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha kilo 92 za heroin, mwaka 2012.
Juni 26 kila mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya. Siku hiyo uhimiza mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi.
Shekiondo amesema elimu hiyo hutolewa kwa njia mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari, Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Maonesho ya Wakulima ya Nanenane, Wiki ya Vijana na Kilele cha Mbio za Mwenge, Siku ya Ukimwi Duniani, Wiki ya Utumishi wa Umma na Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani