Na Stella Aron, JamhuriMedia
Wadau wa habari nchini wamependekeza kuongezwa kwa ya vipengele vinavyopaswa kufanyiwa marekebisho kwenye muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari, ili kuwezesha uwepo wa sheria itakayoleta tija katika sekta ya habari nchini.
Miongoni mwa vipengele ambavyo vinapendekezwa kurekebishwa katika muswada ambao tayari umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni, ni pamoja na utoaji wa leseni kwa vyombo vya habari kila mwaka, ambacho kinaweza kutumiwa vibaya na mamlaka kukwaza usajili wa chombo husika.
Deus Kibamba ambaye ni Mhadhiri wa Masuala ya Diplomasia pia Mjumbe wa Umoja wa Wadau wa Kupata Habari (CoRI), amesema pamoja na hatua nzuri iliyofikiwa katika mchakato wa mabadiliko ya sheria hiyo,baadhi ya vifungu vinahitaji kufanyiwa marekebisho kwani ni changamoto kwa sekta ya habari.
“Kati ya vipengele 65 vya sheria vilivyopendekezwa kufanyiwa marekebisho na wadau wa habari, ni tisa tu ambavyo serikali imevichukua na kuvijumuisha kwenye muswada uliosomwa bungeni,” amesema Kibamba na kuongeza:
“Mfano sheria ya kutoa leseni kila baada ya mwaka mmoja hii inachangia kwa mmiliki wa chombo fulani au mwandishi wa habari kuhofia kupata leseni tena kutokana labda kuandika habari ambazo kwa namna moja ama nyingine zilikuwa na changamoto.”
Kibamba alikuwa akizungumza leo Aprili 20,2023 kwenye mkutano wa wadau wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, kujadili maudhui ya muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, uliowasilishwa bungeni Februari 10,2023.
Suala la kutojumuishwa kwa mapendekezo ya wadau katika muswada pia limeungwa mkono na Wakili James Marenga ambaye amesema vipengele ambavyo vimefanyiwa kazi ni vile vinavyohusu kupunguzwa kwa adhabu zinazotolewa katika makosa yanayobainishwa kwenye sheria hiyo.
“Vipo vifungu ambavyo vilikuwa vinatoa adhabu ya kifungo cha miaka kumi jela au faini ya shilingi milioni, lakini mapendekezo yaliyowasilishwa bungeni yanapunguza adhabu hiyo na kuwa miaka mitano jela na shilingi milioni tatu na tano mtawalia,”anasema Marenga.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewaomba wabunge kutumia nafasi zao wa uwakilishi kuzingatia maoni ya wadau wa habari kwa kuingiza vipengele vilivyoachwa wakati watakapofanya marekebisho ya sheria hiyo ya huduma za habari.
“Nawaomba waandishi wa habari tuendelee kuandika kwa uwazi kuhusu uoungufu huu ili wabunge wetu waweze kufahamu kitu gani tunachoomba kiongezwe kwenye mapendekezo ya mabadiliko yaliyowasilishwa bungeni, ili mwishoni mwa siku tuwe na sheria inayojenga mazingira bora zaidi ya taaluma,” amesema Balile.