Wadau mbalimbali wa habari wameeleza kusikitishwa kwao na kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.
Gazeti la Mwananchi limefungiwa kwa siku 14 wakati Mtanzania limefungiwa kwa siku 90.
Adhabu hiyo imetokana madai ya kuwa magazeti hayo yamekuwa yakiandika habari na makala zinzolenga uchochezi na uhasama hali inayosababisha wananchi kukosa imani kwa vyombo vya dola.
Mmoja wa wadau wa habari ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, aliliambia JAMHURI kuwa adhabu hiyo ni kubwa kulinganishwa na kosa lenyewe.
“Huu ni msiba wetu sote. Kufungia gazeti miezi mitatu ni maumivu makali sana. Kampuni zimekopa benki. Kurejesha mikopo kunatokana na matangazo.
“ Ajira za mamia ya watu kuanzia vyumba vya habari hadi wauza bidhaa mitaani wanaumia. Naiomba serikali ipunguze makali ya adhabu hizi.
“ Ni kali mno jamani. Chonde chonde chonde Serikali, adhabu hizi ni kali mno. Zipunguzwe,” amesema mdau huyo.
Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa Idara ya Habari ilieleza kuwa Gazeti la Mwananchi lilichapisha habari iliyosema kuwa “Mishahara mipya serikalini 2013” kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri haukupaswa kuchapishwa Magazetini na “Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali.
Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam. Jambo ambalo halikuwa la ukweli.
Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti. Serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake hakiwezi kupitisaha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.
Gazeti la Mtanzania imefungiwa kutokana na kuchapisha kichwa kisemacho “Urais wa damu”, Juni 12 mwaka huu katika toleo Namba 7344 na makala isemayo “Mapinduzi hayaepukiki” na “Serikali na Serikalia inanuka damu”