Waandishi wa habari na wadau wengine wamepewa changamoto ya kuishawishi Serikali kuangalia uwezekano wa kusitisha uchimbaji wa madini ya uranium na mwingineo usiozingatia ulinzi wa afya za binadamu nchini.
Aidha, serikali inashauriwa kuweka mpango wa kugharimia mafunzo ya uchimbaji wa madini hayo kwa wazawa ili waweze kusimamia vizuri shughuli hizo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hazisababishi madhara kwa wananchi.
Changamoto hizo zilitolewa Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki na Mwezeshaji wa Sekta ya Mawasiliano Tanzania, Ndimara Tegambwage, katika mafunzo ya uwezeshaji kwa wadau wa habari mbalimbali kuhusu uchimbaji wa madini ya uranium na mengineyo.
Mafunzo hayo ya siku tatu yaliandaliwa na kufadhiliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) chenye makao yake makuu, Kijitonyama, Dar es Salaam.
Tegambwage alisema umefika wakati wa serikali kuona umuhimu wa utekelezaji wa kilio cha wananchi juu ya matatizo na athari zinazotokana na uchimbaji wa madini ya uranium na mengineyo unaofanywa na wawekezaji wa kigeni nchini.
“Uchimbaji wa madini ya uranium umetafitiwa na kuonekana kuwa hatari kwa binadamu, wanyama na mazingira, kutokana na kasi ya usambaaji wa mionzi yake mikali.
“Katika ripoti ya kitaalamu iliyoandaliwa na Jeshi la Marekani mwaka 1995 inaonesha madini ya uranium yanapoingia katika mwili wa binadamu husababisha madhara makubwa ya kiafya.
“Hatari ya uhusiano wa kemikali na mionzi itokanayo na madini ya uranium huingia katika mapafu au figo kwa kiwango cha 238 na huzalisha uotesho (thorium 234 protactinium and other uranium isotopes) unaosababisha mionzi aina ya Alpha na Beta ambayo husabisha saratani, kuua seli na kuharibu mbegu za kiume na kike, hivyo watoto wanaozaliwa na watakaozaliwa kuwa na upungufu wa uhalisia.
“Mfano madhara haya yapo katika nchi ya Japani kutokana na bomu la nyuklia lililopigwa katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945, ambayo ni zaidi ya miaka 60 ambapo madhara yake yapo hadi leo watoto wanazaliwa wakiwa vilema.
Alisema ni wajibu wa wadau kuhoji sababu za serikali kuendelea kutoa vibali vya kuchimba uranium nchini katika mazingira hatarishi na iwapo sheria na sera za uchimbaji madini zipo na zimefafanuliwa na kueleweka kwa wananchi.
Pia wadau wametakiwa kuhoji uhalisi wa kampuni ya Mantra ya Australia inayosemekana kuwa ndio mwekezaji wa uchimbaji wa madini ya uranium nchini isijekuwa ni kampuni hewa.
Alisema maswali hayo ni muhimu kwa kuwa yanalenga kuihamasisha serikali kuona umuhimu wa kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi, hasa wale waishio maeneo ambayo uchimbaji wa madini ya uranium unafanyika.
Serikali pia imetakiwa kumuenzi Mwasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alihimiza viongozi kuhakikisha raslimali za nchi yakiwamo madini zinatumika kunufaisha Watanzania ili waondokane na utegemezi unaowafanya kuwa watumwa wa wawekezaji wa kigeni.
Naye Mtafiti na Mshauri wa Mambo ya Mazingira na Maliasili, Mchungaji John Magafu alisema kwa kutoa mifano mbalimbali ya filamu alizotafiti toka maeneo tofauti kama vile vijiji vya Nyakabale mkoani Geita na Buhemba mkoani Mara na sehemu zingine kunakopatikana madini.
Alisema wananchi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa madini hayo yamewafanya baadhi yao kupoteza uzazi, kupungukiwa nguvu za kiume, kuathirika ngozi, kutoboka macho na wengine kufa, lakini viongozi husika hawajashughulikia malalamiko hayo.
“Wameshindwa kuwasaidia hata pale walipokuwa wanahitaji msaada wa matibabu kwa wale walioathirika kutokana na madini ya uranium, wanaambiwa wakajitafutie matibabu wao wenyewe,” alisema Mchungaji Magafu.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Kitengo cha Mazingira katika LHRC, Flaviana Charles, alisema ukiukwaji wa haki za binadamu katika sehemu za uchimbaji madini upo na unaendelea kutesa wananchi kwa kiwango kikubwa. Alitoa wito kwa wadau mbalimbali kuibana serikali itafute ufumbuzi wa matatizo hayo.